|
Shaw Hassan Shaw |
Kwa wapenzi wa nyimbo za Vijana Jazz Band hakika watakuwa wanakumbuka vile
vipande vya kinanda vilivyokuwa vikianzisha zile nyimbo mbili
alizokuwa akiimba Kida Waziri, Penzi Haligawanyiki na Shingo feni. Mpigaji wake alikuwa Shaw Hassan Shaw Rwamboh. Mwanamuziki huyu
alizaliwa tarehe 25 September 1959, Dar Es Salaam. Alianza kujifunza kupiga gitaa na wenzie kando
ya Ziwa Tanganyika huko Kigoma, wakitumia magitaa ya tajiri mmoja
aliyekuwa na meli ya uvuvi. Alipokuja Dar es Salaam akakutana na
mwanamuziki Zahir Ally Zorro, Zahir ndiye aliyeboresha upigaji wake wa
gitaa kiasi cha kukubaliwa na Patrick Balisidya kupiga gitaa la rythm
katika bendi yake ya pili PAMA Band, chini ya Afro70.
|
Shaw Hassan Shaw wa kwanza kulia aliyenyoosha mkono. Mwendeshaji wa blog hii John Kitime wa kwanza aliyesimama kushoto. Hapa wakiwa Stadium Morogoro wakingojea onyesho la kumkaribisha Nelson Mandela. |
Ni
chini ya malezi ya Patrick alipojifunza kupiga Keybords (Kinanda).
Baada ya hapo aliacha muziki na kujiunga na Dar Technical College.
Lakini 1980 alijiunga na Vijana Jazz kama mpiga Keyboards, alishirikiana
na wanamuziki wengi lakini wengi kwa mapenzi ya Mungu, wametangulia mbele ya haki.
Baadhi ya waliobaki kati ya aliyokuwa nao wakati huo ni John Kitime, Kida Waziri, Saad Ally Mnara, Hamisi Milambo, Huluka Uvuruge, Hassan Dalali,
Hamza Kalala na Rashid Pembe. Mwaka 1990 alijiunga na Orchestra Safari
Sound, chini ya Maalim Muhidin Gurumo (MJOMBA) na Marehemu Abel
Baltazar, hapa alikutana na akina Benno Villa Anthony na
Mhina Panduka (Toto Tundu) .Aliacha bendi baada ya miezi sita tu,
mwenyewe anasema, ‘….kutokana na muhusika kutozingatia mkataba wangu…’.
Alihamia Zanzibar na kujiunga na bendi iliyokuwa ikipiga Mawimbini
Hotel, hakukaa sana kwani Washirika Tanzania Stars walimwita. Hapa
akakutana na mwalimu wake wa gitaa Zahir Ally, Ally Choki, Musemba wa Minyugu,Tofi
Mvambe, Abdul Salvador na wengine, ilitokea kutoelewana baina ya
wanamuziki na yeye kama kiongozi wa bendi ilibidi aachie ngazi kuepusha
bendi kuzidi kujichanganya. Baada ya hapo Kanku Kelly ambaye ni mume wa
dada wa mke wake alimuita ajiunge na Kilimanjaro
Connection Band. Anasema Kanku alimvumilia sana kwa kuwa alikuwa
hajawahi kufanya kazi ya kukopi nyimbo za wanamuziki wengine wakubwa
duniani, hatimae akaweza kujiendeleza na kuweza kumudu kupiga vitu vikubwa, bendi hii ya Kanku ilikua inazunguka kwa kupiga muziki hotel
mbalimbali katika nchi za Malaysia, Singapore, Indonesia, Thailand na Japan jambo ambalo
lilifanya aone kila kitu ni kigeni kila alipokwenda. Katika bendi hiyo alishirikiana na
akina Kanku Kelly, Mafumu Bilal, Maneno Uvuruge, Burhan Adinan, Shomari
Fabrice, Bob Sija, Fally Mbutu, Raysure boy, Delphin Mununga na Kinguti
System. Baadaye Shaw, Kinguti na Burhan Muba waliamua kuanzisha kundi
dogo wakitumia sequencer keyboards na kumuaga Kanku Kelly. Group hili
lilijiita Jambo Survivors Band, bendi ambayo itakumbukwa kwa ule wimbo Maprosoo ulioimbwa na MlasiFeruzi ambao
uliokuwa katika album ya MAPROSOO.
|
Mlasi feruzi |
Baada ya hapo bendi ikaanza kuzunguka
nchi mbalimbali ikipiga katika mahotelini. Kupitia muziki Shawa amekwisha fika Oman , Fujairah,
U.A.E, Singapore, Malaysia na Thailand. Shaw anasema
wanamuziki ambao hatawasahau kwa kuwa wamemfikisha alipo ni Zahir Ally
Zorro, Marehem Patrick Balisdya, Waziri Ally, Kinguti System, Burhan
Muba na Kanku Kelly. Kituko ambacho hawezi kusahau ni nchini Malasyia wakati
akiwa na Kanku Kelly na ikiwa ni mara ya kwanza kwake kupiga muziki akiwa amezungukwa
na watu weupe watupu. Anasema nyimbo zote zilipotea kichwani akawa hakumbuki hata nyimbo moja aliyokuwa kafanyia mazoezi
No comments:
Post a Comment