Maneno Uvuruge(kushoto), na marehemu Mawazo Hunja mwenye trumpet |
Maneno Uvuruge ni moja ya wanamuziki
waliotoka katika familia ya wanamuziki ya ukoo wa Uvuruge. Kaka zake Jumanne,
Stamili, na Huluka ni kati ya wapiga magitaa walioheshimika sana katika jamii
ya wanamuziki wa bendi Tanzania.
Jumanne Uvuruge ambae alikuwa mkubwa wa
akina Uvuruge wote, ndie aliyetunga kibao maarufu cha Georgina, kilichopigwa na
Safari Trippers na kuimbwa na Marijani Rajabu. Siku zake za mwisho za maisha
Jumanne alikuwa anajishughulisha na kupata riziki yake kwa kuzunguka katika
mabaa mbalimbali na gitaa na kupiga maombi mbalimbali ya wanywaji, na kisha
kuhama na kuelekea baa nyingine. Hayakuwa maisha rahisi.
Maneno Uvuruge hana kumbukumbu ya jinsi
gani Jumanne alijifunza gitaa, lakini anajuwa kuwa Stamili alifundishwa na
Jumanne. Anakumbuka zaidi jinsi Huluka alivyojifunza kwani ndie alikuwa kaka
yake waliefuatana kuzaliwa. Huluka alijifunza gitaa kwa kuanza kuchonga gitaa
lake mwenyewe, aliiba mishipi ya kuvulia ya baba yake na ndio zikawa nyuzi za
gitaa lake, siku babake alipogundua wizi huo alivunja vunja gitaa na kumkataza
asiguse mishipi yake tena, lakini akamwelekeza inakonunuliwa, Huluka alitafuta
pesa na kwenda kununua mishipi na kuendelea na gitaa lake la kopo. Wakati huo
Huluka alikuwa anasoma, naye Maneno akaanza hamu ya kutaka kujua kupiga gitaa akawa
anaiba gitaa la kaka yake kila alipoenda shule, ilikuwa ni ugomvi kila
alipokata nyuzi kwani alikuwa bado anajifunza. Jumanne na Stamili wakaanza
rasmi kumfundisha gitaa Huluka nae akalijua vizuri sana. Si muda mrefu baadae
nae akaanza rasmi kumfundisha mdogo wake. Maneno anasema wimbo wa kwanza kakake
kumfundisha ni ile rhythm ya wimbo Novelle Geneation wa Orchestra Lipualipua,
wimbo huu ulikuwa ni kipimo muhimu kwa wapiga rythm enzi hizo. Freddy Benjamin
ndie aliyemshauri kujiunga na Bendi. Alimkaribisha UDA Jazz ambako alikuwa
akiimbia na pamoja na kuweza kupiga gitaa alifanyiwa mizengwe na mpiga rhythm
aliyekuweko na ambae pia alikuwa katibu wa bendi. Freddy alimuombea kazi Super
Rainbow iliyokuwa na makao yake makuu pale Sunlight Bar Mwananyamala B. Na hapo
akakutana na wanamuziki kama Hatibu Iteytey, Nuzi Ndoli, Rocky, Mzee Bebe,
Akina Eddy Sheggy walikuwa bado hawajajiunga na bendi hii wakati huo.
Bwana balozi. Hivi Kiniki Kieto ni mtanzania ama mcongo, najuwa aliimbia Vijana na Maquis. Kwa sasa yuko wapi?
ReplyDelete