Keppy Kiombile Bass, Maneno Uvuruge Rythm, Omary Makuka Second solo, Juma Choka Drums, Lubaba Solo guitar |
Katika kipindi ambapo Maneno
Uvuruge alikuwa akipigia Super Rainbow ndipo Eddy Sheggy na Emma Mkello
walipojiunga, hawa hukumbukwa sana kwenye bendi hii kwa ajili ya ule wimbo
Milima Ya Kwetu, pia nae Banza Tax akajiunga kipindi hiki. Na kule Mabibo bendi
ya Mambo Bado ilipata msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo
wanamuziki wake Juma Choka mpiga drums, Lodji Mselewa na Nana Njige pia wakajiunga
na kundi na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana Assossa aliweza kuifufua tena
Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari bendi
ilikuwa iko katika hali mbaya kwani Assossa aliacha tena akiwa katika harakati
ya kuunda bendi mpya na Mambo Bado ikafa rasmi. Juma Choka akamtaarifu Maneno
kuwa Urafiki Jazz kuna nafasi ya kazi na hapo akenda na kusailiwa na Ngulimba
wa Ngulimba, Marehemu Mzee Juma Mrisho, Urafiki nayo ilikuwa katika siku zake
za mwisho lakini bado yule mpiga solo mahiri Michael Vicent alikuweko. Kipindi
hiki pia waliingia Mohamed Gota gota na Hussein Jumbe. Maneno Uvuruge sasa
alianza kufahamika kwa wanamuziki wengine kuwa ana uwezo mkubwa na bendi
zikaanza kumsaka, na kuanzia hapo amekuwa hatafuti kazi bali anatafutwa. Bendi
ya kwanza kumchukua ilikuwa ni Maquis, alichukuliwa ili awe mpiga gitaa la
rhythm, aliwakuta wapiga rhythm wawili, huko, Mbwana Cox na Makuka. Akawa
mwanamuziki wa Maquis wakati huo wapiga solo wa bendi hiyo walikuwa ni Nguza
Viking, na Mzee Lubaba.
Mwanamuziki Belly Kankonde
akakutana na Marehemu Mzee Mwendapole na kuamua kuipa uhai bendi ya
Afrisongoma. Kankonde akawashawishi wanamuziki wenzie wanne wa Maquis, Maneno
Uvuruge (guitar),Kiniki Kieto(mwimbaji), Comson Mkomwa(saxophone) na Keppy
Kiombile(bass) wakahamia Afrisongoma. Maneno hakukaa muda mrefu kwani Nguza
alimfuata yeye na Comson na kuwarudisha Maquis , na kwa kuwa walikuwa
wamekwishapokea fedha za Mzee Mwendapole kesi ilifika polisi na ikalazimu
Maquis warudishe fedha hiyo. Lovy Longomba alijiunga na Maquis nae hakukaa muda
mrefu Mwendapole akamshawishi akaunde upya kundi la Afrisongoma ambalo katika
awamu ya kwanza liliishia kurekodi mara moja na kutokuwa na maendeleo. Lovy pia
tena akamuondoa Maneno na kuhamia nae Afrisongoma.
Wakati huo Mosesengo Fan Fan yule
mpiga gitaa mahiri aliyetoka kwa Franco na kupigia Matimila na Makassy alikuwa
amehamia Uingereza na akawa amemtaka Kiniki Kieto awashawishi Maneno Uvuruge,
Keppy Kiombile, na Vivi Kapaya wamfuate,lakini mpango huo uliishia kwa Kiniki
na Vivi kuendelea na Fanfan wakati Maneno na Keppy wakahamia Afrisongoma wakiwa
na Lovy. Wanamuziki kadhaa walihamia Afriso wakati huo wakiwemo Kalamazoo, na
Mzee Mponda ambae baada ya kutoka Msondo alikuwa kapita Sikinde na akatua
Afrisongoma. Na hapo ndipo msondo wakamchukua Maneno kwa mara ya kwanza. Alikaa
kwa muda na rafiki zake akina Benno Vila Anthony wakaweza kumshawishi ahamie
Sikinde. Baada ya muda si mrefu Nguza akamfuata ili kumshawishi ajiunge na
Orchestra Sambulumaa. Ilikuwa ni ushawishi wa Skassy Kasambula na Emmanuel
Mpangala aliyekuwa mkurugenzi wa bendi ndio ulioweza kumfanya Maneno ahamie
Sambulumaa.
Kitime hebu nikumbushe nyimbo za Matimila ambamo Mose Se Sengo 'Fan Fan' amepiga solo. Halafu ule wimbo wa Makassy 'Zimbabwe" nani kapiga solo maana gita lililopigwa humo ni hatari tupu.
ReplyDelete