Marehemu Kassim Karuona, mmoja wa wapiga rythm waliokuwa bora Tanzania |
Lakini leo tuzungumzie gitaa la rythm. Chombo hiki bado kinapigwa katika bendi nyingi lakini umaaarufu wake umeshuka sana. Naona wapigaji wake hawapewi umuhimu, na unaweza kuingia katika asilimia 90 ya bendi ukamuona mpiga rythm lakini husiki anapiga nini kutokana na kelele zinazoruhusiwa kuendelea katikati ya muziki. Katika kipindi cha miaka ya 60 na 70, gitaa hili lilikuwa na umuhimu mkubwa na wapigaji wake waliweza kubuni staili zao wenyewe. Kati ya wapiga rythm maarufu namkumbuka Satchmo, hilo ndio lilikuwa jina la kisanii la Harrison Siwale mpiga rythm wa Jamhuri Jazz, yeye alikuwa na staili peke yake ya kupiga rythm, sikumbuki kusikia mtu mwingine akipiga rythm ya aina yake kabla ya hapo. Rythm yake ilitawala nyimbo za Jamhuri wakati huo. Kumbuka wimbo kama Mganga no 1 na 2, au Blandina. Marehemu Mzee Kasim Kaluwona nae alikuwa na staili tofauti ya upigaji uliyoifanya Tabora Jazz kuwa na staili yake peke yake, kumbuka gitaa lake katika wimbo Asha, au Dada Lemmy. Charles Kazembe akiwa na Morogoro Jazz anakumbukwa katika upigaji wa rythm kwenye nyimbo kama Wajomba Wamechacha, yeye alifuata upangiliaji wa nyuzi za gitaa kama alivyokuwa anafanya Vata Mombasa wa Lipualipua, yaana kuweka nyuzi mbili zenye unene sawa katika gitaa lake, uzi namba 1 na namba 4. Hao ni wachache tu kulikoweko na wengi marufu, wote wakijitahidi kuwa na staili yao, Butiama Jazz ilikuwa tofauti na Western Jazz, au mipigo ya Mzee Chachil wa Urafiki. Kama nilivyosema hapo juu katika kipindi hiki huko Zaire kulikuwa na mipigo mbalimbali ya gitaa la rythm, ikiwemo kitu kipya kilichoanzishwa ambapo katika ufungaji wa nyuzi ,wapiga rythm wakauondoa uzi namba nne na kuweka uzi namba moja, hivyo kukawa na nyuzi namba moja 2 katika gitaa, hapo ndipo akina Vata Mombasa wakaweza kuleta utamu mpya katika upigaji wa rythm. Wakati huo Orchestra Kiam wakawa wanajivunia kupiga rythm kwa spidi kali sana,vibao kama Kamiki, Bomoto ni ushahidi wa kazi hizo. Utamu wa ufungaji wa nyuzi kwa staili hii uliweza kusikika vizuri katika gitaa lililopigwa mwanzo kabisa wa wimbo Andoya. Leo vionjo vya upigaji huo vinarudi kwa njia ya ajabu sana. Vikundi vya taarab vimeanza 'kuachia rythm' gitaa moja kubaki linapiga peke yake, japo wao hupiga gitaa la solo lakini staili ni ile ya enzi, na ukweli Taarab wameteka wapenzi wengi wa dansi. Ni ushauri utakaofaa kwa bendi zetu kurudisha hadhi ya gitaa hili katika bendi zao.
Bwana Kitime wote uliowataja hapo juu nawaheshimu sana, lakini kwangu mimi Lele Nsundi (RIP) wa Orchestre Kiam ndiye mpiga rhythm hodari zaidi aliyewahi kutokea Afrika. Ukisikiliza upigaji wake ni vigumu kuamini kama alikuwa akitumia vidole kuchazara gitaa. Huyu ni kama alikuwa na mashine katika mikono yake. Lele katika rhythm, Djuke kwenye solo na Kady katika bass waliifanya Orchestre Kiam kuwa na safu bora zaidi ya magitaa nchini Congo na barani Afrika kati ya mwaka 1974 na 1977. Hawa walikuwa ni vichaa. Hebu sikiliza vipaji vyao katika Mbale (http://www.youtube.com/watch?v=uo6Mct1CXoE), Memi (http://www.youtube.com/watch?v=9owhTXIDhvk), Moni Afinda (http://www.youtube.com/watch?v=RV1n6sfjJBE) na Kamiki (http://www.youtube.com/watch?v=a7hPwOGChmA).
ReplyDeleteNi kweli na mimi nakubali kuwa bendi za dansi sasa inabidi zirudi katika muziki wa Kitanzania.Yaani kila bendi sasa inajitahidi kuiga na kupiga vionjo vya kicongo..Labda ni wakakti muafaka kuanza kufundisha muziki wa kibongo mashuleni na vyuoni sasa ili tuokoe muziki wetu.Kaka Kitime napenda sana jinsi unavyochambua na kutoa utaalam wa hali ya juu katika suala la muziki wa Afrika...Inabidi uandike kitabu ili kizazi kijacho kibaki na hazina ya uelewa wako.
ReplyDeleteBwana Kitime charles Kazembe hakupigia Morogoro jazz bali alipigia Super Volcano na Marehemu Rex[Mbaraka Mwinshehe],wajomba wamechacha Rithim gitaa lilipigwa na Samson Gumbo Kazingoma.
ReplyDelete