Waziri Ally akipiga kinanda Lucky Star |
Katika miaka ya 50
wanawake tisa wa Tanga walijikusanya na kuanzisha kikundi cha
kuimba walichokiita Raha til Fuad maana yake Raha ya Moyo. Akina mama hawa
chini ya bibie aliyeitwa Mama Akida au aka Mama Lodi, waliendesha kikundi chao
wakiwa wanaimba nyimbo za Siti Binti Sadi na tungo zao ambazo waliimba katika
melody ya nyimbo za kihindi zilizotamba wakati huo. Kundi hili liliendelea na
kuanza kuruhusu wanaume kujiunga hasa wakiwa wapiga vyombo, akiwemo mtoto wa Mama
Akida, Akida Jumbe hatimaye alijiunga na kundi hili kama mpiga accordion kwenye
mwaka 1962. Kundi hili ambalo baadae lilikuja kuitwa Young Noverty, liliendelea
mpaka kukaweko na mgawanyiko uliozaa kundi la Shaabab Al Waatan. Hapa ndipo
kukaanza mtindo wa kuweko kundi pinzani jambo ambalo kwa njia ya ajabu sana
likawa linadumu kiasi cha miaka kumi kumi. Miaka ya 1960s Young Noverty na
Shabaab al Waatan, miaka ya 1970 Lucky Star Musical Club na Black Star Musical Club,
miaka ya 1980 Golden Star Taarab na White Star Taarab, miaka ya 1990, Babloom Modern Taarab na
Freedom Modern Taarab. Taarab ya Tanga ndo haswa inastahili kuitwa modern
Taarab, kwani wao hawakufuata taarab ile iliyoletwa Zanzibar enzi ya Sultan
Seyyid Barghash, makundi la taarab ya Tanga yalikuwa madogo na vyombo vyake vilikuwa
pamoja na Gitaa la besi, gitaa la solo, drums bongos ,akodion au kinanda, nyimbo zao zilikuwa fupi na si ndefu kama za Kizanzibari., nyimbo zilitegemea
mipigo ya ngoma za asili za kumbwaya na chakacha na hata baadaye mitindo kama
rumba,bossa nova ilitumika kama mapigo. Na Taarab ya Tanga ndio iliyoanzisha
moto wa vikundi vya taarab Tanzania Bara. Moshi kulikuwa na New
Alwatan, AzimioTaarab, na Blue Star Taarab , Arusha-Blue Star Taarab, Dodoma-Dodoma
Stars, Kondoa –Blue Stars, Mbeya-Magereza Kiwira, Mwanza-Ujamaa Taarab, Bukoba wakiwa na Bukoba Stars, na muendelezo huu uliingia mpaka Burundi kutokana na mwana
muziki mmoja alie julikana kama Athmani Mkongo, alitoka Burundi na bendi yake
kufika Tanga akawa mwanamuziki mahiri wa Taarab na hata kuipeleka kwao
Burundi na kukaanzshwa huko vikundi kadhaa vya Taarab.
Kitine wewe nihazina, maana habari kama hizi tungezipata wapi, jamani blog zinasaidia na hasa za watu kama hawa ambao wanatupa vitu vyenye kujenga, kuelimisha na kutukumbusha, Tupo pamoja mkuu
ReplyDeleteKitine kazi yako ni nzuri sana. Asante. Ombi langu ni kuwa; makala hizi ziambatane na nyimbo zao. Kwa makala hii weka za Black Stars na Lucky Stars; sauti za Bi Shakila na Bi Sharmila ziko so unique.
ReplyDeleteDuuh!
ReplyDeleteEee bwana Kitime huyo anaepiga KII BOD ni KIIZINJA?
Duh! Watu wanatoka mbali!
Naaam.. ❤❤❤
ReplyDelete