Tuesday, January 3, 2012

Wanamuziki wapata pigo jingine mpiga solo Sakul Minori afariki akiwa safarini Zanzibar

Sakul enzi za uhai wake, nyuma yake ni Kejeli Mfaume


Katika hali ya kutia huzuni kabla hata wiki moja haijapita toka mpiga bass mahiri Andy Swebe ameaga dunia ghafla, mpiga solo wa Cassava Band Sakul ameaga dunia ghafla wakati wakiwa kwenye ziara fupi huko Zanzibar. Akielezea mkasa mzima kiongozi wa bendi hiyo Kejeli Mfaume alieleza kuwa ghafla jana Sakur alisema anajisikia vibaya, alianza kuhangaika akilalamika tumbo linamuuma, na kwa kuwa walikuwa katika hoteli ya kitalii iliyombali na hospitali walijaribu kufanya jitihada za kumfikisha hospitali lakini alifia njiani. Mipango inafanyika ya kurudisha mwili Dar es salaam kwa maziko. Sakur Minori mzaliwa wa Sumbawanga ambaye alikuwa na ulemavu wa macho alikuwa mpiga solo mahiri, mwimbaji pia mzuri sana ambaye pamoja na bendi hii ya Cassava ameshawahi kupigia bendi ya Seven Blind Beats ambayo ilikuwa bendi yenye wanamuziki wasioona watupu, ameshapigia Tabora Jazz, na Jambos ya Mwanza, na bendi kadhaa nyingine. Mungu amlaze pema peponi.

1 comment:

  1. Pole kwa wafiwa wote,hiyo yote ni kazi ya mungu.

    Pia uncle kitime nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kusikiliza ombi langu la muda mrefu la kibao cha tancut "kumbe nimemkaribisha nyoka" nashukuru umekiweka kwenye play list,machozi yananitoka kwa kweli nawalilia kyanga songa na kassaloo!

    ReplyDelete