Wiki
hii nilipata bahati ya kutembelea mji wa Tanga, mji ambao sifa zake zilianza kusikika kuanzia
enzi za utawala wa Wajerumani, jiji ambalo shule ya kwanza ya serikali ilijengwa
hapa enzi hizo hizo za utawala wa Wajerumani, jiji ambalo liliendelea kukua sana
kutokana na kilimo cha katani na hivyo kukusanya vijana toka kila kona ya nchi
kuja kutafuta kazi katika mashamba makubwa ya katani wakati huo. Tanga mji
ambao kutokana na uwingi wa vijana wakati huo, shughuli za burudani ya muziki nazo
zilifikia kiwango cha juu kuliko sehemu nyingi Tanzania.
Ukizungumzia
historia ya muziki wa dansi, huwezi kukwepa kuzungumzia Tanga, kwani historia
inatueleza kuwa kabla ya kuanza vikundi vya muziki wa dansi kulianzishwa klabu
za kucheza dansi. Klabu hizo zikitumia muziki wa santuri, wanachama wake
walicheza na hata kushindana kucheza muziki kwa mitindo mbali mbali ya kigeni ikiwemo
waltz, tango, chacha, rumba na kadhalika. Klabu za kwanza nchini zilianzia
Tanga. Kulikuwa na klabu kama Young Noverty miaka michache baada ya vita ya
kwanza ya dunia, wakati huo nchi ya Tanganyika ikiwa bado changa kabisa. Mtindo
huu wa vilabu vya dansi ulienea na baadae kuingia Dar es Salaam na miji mingine
iliyokuwa imeshaanza wakati huo. Vilabu hivi ndivyo baadae vikaanzisha vikundi
vya kwanza vya muziki wa dansi. Hata majina ya vikundi hivyo vya kwanza
yalihusiana na klabu za burudani za wakati huo. Kulikuwa na vikundi kama Coast
Social Orchestra, Dar es Salaam Social Orchestra na kadhalika. Hivyo mji wa Tanga ulikuwa katika ndoto
za vijana enzi hizo. Kwa vile vijana wengi walikusanyika katika jiji hili nchi,
kulianzishwa pia klabu ambazo zilikuwa kwa ajili ya vijana waliokuwa wakitoka
kabila moja. Klabu hizo zikiwa na nia ya wananchama wao kusaidiana katika shida
na raha, na vilabu hivi pia vilikuwa ni sehemu muhimu katika kutoa burudani kwa
vijana waliotoka sehemu moja. Kati ya klabu hizi kulikuweko na klabu iliyoitwa
Young Nyamwezi, kama jina lake lilivyo ilikuwa ni klabu ya vijana kutoka
Unyamwezini. Hatimae mwaka 1955 klabu hii ilianzisha bendi yake iliyoitwa Young
Nyamwezi Band, bendi hii ilikuja kukua na baada ya Uhuru ilibadili jina na
kuitwa Jamhuri Jazz Band. Hakika kwa vijana waliokuwa wapenzi wa muziki miaka
ya 60 na 70 ilikuwa lazima uifahamu Jamhuri Jazz Band, muziki wake, au kwa
lugha ya enzi zile, ‘vibao’ vyake vilijulikana Afrika ya Mashariki nzima. Bendi
hii ilikuwa ikibadili mitindo ya upigaji wake na kupiga katika mitindo ya
‘Toyota’ na hatimae ‘Dondola’. Aliyekuja kumiliki bendi hii, ambayo wapenzi
wake pia waliita JJB alikuwa Joseph Bagabuje, kulikuwa hata maelezo wakati fulani kuwa JJB ilikuwa kifupi
cha Joseph Jazz Band na si Jamhuri Jazz band. Kama ilivyokuwa kawaida ya bendi
za wakati ule Jamhuri Jazz Band ilisafiri sana na kufanya maonyesho katika kila
kona ya nchi yetu, jambo hilo pamoja na kuwa bendi hii ilirekodi na kutoa
santuri kupitia kampuni za kurekodi za Kenya na pia kurekodi nyimbo zake katika
radio ya Taifa uliifanya bendi hii kuwa maarufu sana. Upigaji wa aina ya pekee
wa gitaa la rhythm wa bendi hii, ambao uligunduliwa na Harrison Siwale, maarufu
kwa jina la Sachmo, uliigwa na wapiga magitaa ya rhythm wengi nchini. Uimbaji
wa kutumia waimbaji wawili tu, uliopendelewa na bendi za Tanga wakati huo
ikiwemo bendi nyingine maarufu wakati huo, Atomic jazz Band, ulikuwa ni wa aina
yake pia. Jamhuri Jazz Band pia ndio kilikuwa chanzo cha bendi maarufu ya Simba
wa Nyika na bendi zilizozaliwa baada ya hapo. Nilibahatika kukutana mtu
aliyekuweko siku ya kwanza ya safari ya kuja kuzaliwa kwa Simba wa Nyika,
hakika ni hadithi yake ilikuwa ya kusisimua. Inasemekana kuwa siku hiyo Jamhuri
Jazz Band ilikuwa imekodishwa kwa ajili ya kupiga kwenye harusi kule Muheza.
Wanamuziki walikuwa wakilazimika kukusanyika katika jengo la klabu lililokuwa
Barabara ya 15 ili kupata usafiri wa kwenda Muheza. Siku hiyo wanamuziki wengine walikusanyika lakini
George na Wilson Peter, Luza Elian a wengine wachache hawakuonekana, baada ya
upelelezi mfupi ikajulikana kuwa wamejificha au wameondoka mjini Tanga, hivyo
ikalazimika kutafuta wanamuziki viraka wa haraka haraka kuweza kufanikisha
onyesho la siku hiyo, msimuliaji alinambia kuwa japo yeye hakuwa mwanamuziki
bali shabiki tu wa bendi aliweza kupanda jukwaani na kuimba katika harusi hiyo,
hali haikuwa mbaya kwani alijitokeza mteja mwingine akitaka bendi ikapige kwenye
harusi yake pia, lakini ombi lake lilikataliwa kwani wanamuziki walijua kuwa
hawakuwa kwenye kiwango chao. Na baada ya hapo kikaanza kipindi kigumu kwa
Jamhuri Jazz Band kujitahidi kurudisha hadhi na ubora wa bendi, na pia ikaanza
safari iliyokuja kubadili historia ya muziki wa dansi Afrika mashariki kwa
vijana hawa waliotoroka kuelekea Arusha ambako walianzisha Arusha Jazz Band na
hatimae kuvuka mpaka na kuingia Kenya ambako walianzisha Simba wa Nyika
ambayo mafanikio yake yanatingisha
hisia za wapenzi wa muziki wa dansi mpaka leo.
No comments:
Post a Comment