Picha iliyopigwa Uingereza wakati Salome alipoenda huko na Shikamoo Jazz Band. Toka Kushoto Marehemu Salome Kiwaya, Marehemu Papa Wemba, na Marehemu Bi Kidude Mungu awalaze pema. |
Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa za msiba wa Mama
Salome Kiwaya, mwanamuziki mkongwe. Taarifa zilinifikia kuwa Salome amefariki
katika ajali ya gari iliyotokea Dodoma sehemu za Meriwa. Nilimfahamu Salome kwa mara ya kwanza mwaka 1987, wakati nikiwa bendi ya Tancut Almasi Orchestra, tulipopiga kambi Dodoma Hotel
kwa muda wa miezi mitatu, tukitoa burudani kwanza kwa wajumbe wa mkutano wa Kizota, kisha wenyeji wa mji wa Dodoma. Katika kufahamiana kipindi hicho, tuliweza hata kupiga wimbo wake mmoja ulioitwa Tuhina, uliokuwa ukiimbwa na Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa, ambao nao ni marehemu. Siku moja nilipita mtaani Dodoma na
kununua kanda za muziki wa Salome, nilizipenda sana nyimbo zake na nikamuahidi kuwa ningejitahidi
kuzipeleka kwa watu wenye uwezo wa kuendeleza kazi zile. Nilizipeleka kanda kwa Ronnie
Graham, Mscotch mmoja mwenye upenzi na uelewa mkubwa wa muziki wa Kiafrika na
hasa rumba, na huyu Mscotch ndie aliyewezesha kuanzishwa kwa bendi ya Shikamoo Jazz Band.
Baada ya kuzisikia nyimbo zile akaamua kuwa Salome asindikizane na bendi ya
Shikamoo kwenye ziara yao ya Uingereza kama muimbaji wa kike. Salome alienda
Uingereza na aliporudi ndipo alipoanza kununa vyombo na kuunda kundi la Saki
Stars, ikiwa ni kifupi cha Salome Kiwaya Stars. Mume wake Mzee Kiwaya nae ni
msanii maarufu aliyekuwa kiongozi wa kikundi cha Utamaduni cha CDA miaka hiyo ya 80.
Kuanzia hapo nimekuwa karibu sana na Salome, miaka ya 90 wakati nikiwa
Mwenyekiti wa CHAMUDATA, Salome ndie alikuwa mwenyekiti wa chama hicho katika
mkoa wa Dodoma baada ya mkutano mkubwa wa wanamuziki uliofanyika mwezi June
1998, kule Bagamoyo, ambapo wanamuziki 265 waliweza kukusanyika pamoja na kukaa
siku nne katika mji wa Bagamoyo wakifanya warsha za fani mbalimbali za muziki.
Katika miaka ya karibuni Salome alishughulika na sanaa ya urembo akiwa wakala wa Miss Tanzania kwa kanda ya Kati na kuweza kutoa MIss Tanzania mmoja, baadae aliingia katika siasa na kufikia kuwa Mwenyekiti wa UWT wa Mkoa wa Dodoma, lakini aliendelea na muziki katika maisha yake
yote.
Mungu Amlaze Pema Salome Kwaya. Ucheshi wako hatutausahau.
JOHN KITIME
JOHN KITIME
No comments:
Post a Comment