Mawazo Hunja kwenye trumpet, Maneno Uvuruge kwenye gitaa |
Maneno Uvuruge ni
moja ya wanamuziki waliotoka katika familia ya wanamuziki ya ukoo wa
Uvuruge. Kaka zake Jumanne, Stamili, na Huluka ni kati ya wapiga magitaa
walioheshimika sana katika jamii ya wanamuziki wa bendi Tanzania.
Jumanne
Uvuruge ambae alikuwa mkubwa wa akina Uvuruge wote, ndie aliyetunga
kibao maarufu cha Georgina, kilichopigwa na Safari Trippers na kuimbwa
na Marijani Rajabu. Siku zake za mwisho za maisha Jumanne
alikuwa anajishughulisha na kupata riziki yake kwa kuzunguka katika
mabaa mbalimbali na gitaa na kupiga maombi mbalimbali ya wanywaji, na
kisha kuhama na kuelekea baa nyingine. Hayakuwa maisha rahisi.
Maneno
Uvuruge hana kumbukumbu ya jinsi gani Jumanne alijifunza gitaa, lakini
anajuwa kuwa Stamili alifundishwa na Jumanne. Anakumbuka zaidi jinsi
Huluka alivyojifunza kwani ndie alikuwa kaka yake waliefuatana kuzaliwa.
Huluka alijifunza gitaa kwa kuanza kuchonga
gitaa lake mwenyewe, aliiba mishipi ya kuvulia ya baba yake na ndio
zikawa nyuzi za gitaa lake, siku babake alipogundua wizi huo alivunja
vunja gitaa na kumkataza asiguse mishipi yake tena, lakini akamwelekeza
inakonunuliwa, Huluka alitafuta pesa na kwenda kununua mishipi na
kuendelea na gitaa lake la kopo. Wakati huo Huluka alikuwa anasoma, naye
Maneno akaanza hamu ya kutaka kujua kupiga gitaa akawa anaiba gitaa la
kaka yake kila alipoenda shule, ilikuwa ni ugomvi kila alipokata nyuzi
kwani alikuwa bado anajifunza. Jumanne na Stamili wakaanza rasmi
kumfundisha gitaa Huluka nae akalijua vizuri sana. Si
muda mrefu baadae nae akaanza rasmi kumfundisha mdogo wake. Maneno
anasema wimbo wa kwanza kakake kumfundisha ni ile rhythm ya wimbo
Novelle Geneation wa Orchestra Lipualipua, wimbo huu ulikuwa ni kipimo
muhimu kwa wapiga rythm enzi hizo. Freddy Benjamin ndie aliyemshauri
kujiunga na Bendi. Alimkaribisha UDA Jazz ambako alikuwa akiimbia na
pamoja na kuweza kupiga gitaa alifanyiwa mizengwe na mpiga rhythm
aliyekuweko na ambae pia alikuwa katibu wa bendi. Freddy alimuombea kazi
Super Rainbow iliyokuwa na makao yake makuu pale Sunlight Bar
Mwananyamala B. Na hapo akakutana na wanamuziki
kama Hatibu Iteytey, Nuzi Ndoli, Rocky, Mzee Bebe, Akina Eddy Sheggy
walikuwa bado hawajajiunga na bendi hii wakati huo.Keppy Kiombile Bass, Maneno Uvuruge Rythm, Makuka Second solo, Juma Choka Drums, Lubaba Solo enzi ya Maquis |
Katika
kipindi ambapo Maneno Uvuruge alikuwa akipigia Super Rainbow ndipo Eddy
Sheggy na Emma Mkello walipojiunga, hawa hukumbukwa sana kwenye bendi
hii kwa ajili ya ule wimbo Milima Ya Kwetu, pia nae Banza
Tax akajiunga kipindi hiki. Na kule Mabibo bendi ya Mambo Bado ilipata
msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo wanamuziki wake Juma
Choka mpiga drums, Lodji Mselewa na Nana Njige pia wakajiunga na kundi
na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana Assossa aliweza kuifufua tena
Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari
bendi ilikuwa iko katika hali mbaya kwani Assossa aliacha tena akiwa
katika harakati ya kuunda bendi mpya na Mambo Bado ikafa rasmi. Juma
Choka akamtaarifu Maneno kuwa Urafiki Jazz kuna nafasi ya kazi na hapo
akenda na kusailiwa na Ngulimba wa Ngulimba, Marehemu Mzee Juma Mrisho,
Urafiki nayo ilikuwa katika siku zake za mwisho lakini bado yule mpiga
solo mahiri Michael Vicent alikuweko. Kipindi hiki pia waliingia Mohamed
Gota gota na Hussein Jumbe. Maneno Uvuruge sasa alianza kufahamika kwa
wanamuziki wengine kuwa ana uwezo mkubwa na bendi zikaanza kumsaka, na
kuanzia hapo amekuwa hatafuti kazi bali anatafutwa. Bendi ya kwanza
kumchukua ilikuwa ni Maquis, alichukuliwa ili awe mpiga gitaa la rhythm,
aliwakuta wapiga rhythm wawili, huko, Mbwana Cox na Makuka. Akawa
mwanamuziki wa Maquis wakati huo wapiga solo wa bendi hiyo walikuwa ni
Nguza Viking, na Mzee Lubaba.
Mwanamuziki
Belly Kankonde akakutana na Marehemu Mzee Mwendapole na kuamua kuipa
uhai bendi ya Afrisongoma. Kankonde akawashawishi wanamuziki wenzie
wanne wa Maquis, Maneno Uvuruge (guitar),Kiniki Kieto(mwimbaji), Comson
Mkomwa(saxophone) na Keppy Kiombile(bass) wakahamia Afrisongoma. Maneno
hakukaa muda mrefu kwani Nguza alimfuata yeye na Comson na kuwarudisha
Maquis , na kwa kuwa walikuwa wamekwishapokea fedha za Mzee Mwendapole
kesi ilifika polisi na ikalazimu Maquis warudishe fedha hiyo. Lovy
Longomba alijiunga na Maquis nae hakukaa muda mrefu Mwendapole
akamshawishi akaunde upya kundi la Afrisongoma ambalo katika awamu ya
kwanza liliishia kurekodi mara moja na kutokuwa na maendeleo. Lovy pia
tena akamuondoa Maneno na kuhamia nae Afrisongoma.
Wakati
huo Mosesengo Fan Fan yule mpiga gitaa mahiri aliyetoka kwa Franco na
kupigia Matimila na Makassy alikuwa amehamia Uingereza na akawa amemtaka
Kiniki Kieto awashawishi Maneno Uvuruge, Keppy Kiombile, na Vivi Kapaya
wamfuate,lakini mpango huo uliishia kwa Kiniki na Vivi kuendelea na
Fanfan wakati Maneno na Keppy wakahamia Afrisongoma wakiwa na Lovy.
Wanamuziki kadhaa walihamia Afriso wakati huo wakiwemo Kalamazoo, na
Mzee Mponda ambae baada ya kutoka Msondo alikuwa kapita Sikinde na
akatua Afrisongoma. Na hapo ndipo msondo wakamchukua Maneno kwa mara ya
kwanza. Alikaa kwa muda na rafiki zake akina Benno Vila Anthony wakaweza
kumshawishi ahamie Sikinde. Baada ya muda si mrefu Nguza akamfuata
ili kumshawishi ajiunge na Orchestra Sambulumaa. Ilikuwa ni ushawishi
wa Skassy Kasambula na Emmanuel Mpangala aliyekuwa mkurugenzi wa bendi
ndio ulioweza kumfanya Maneno ahamie Sambulumaa
No comments:
Post a Comment