Asia Darwesh kwenye kinanda pembeni yake ni Johnny Rocks kwenye drums. Haba wakiwa Bandari Grill- New Africa Hotel-enzi za Ngoma za magorofani |
MAKALA HII IMEANDIKWA NA MWANDISHI FRED MOSHA
Jina Asia Daruwesh, sio jina geni kwa mashabiki wa muziki
Tanzania na pengine Afrika mashariki kwa ujumla. Huyu Dada anaweza kutajwa kama
mpiga kinanda wa kwanza kabisa mwanamke kuwahi kutokea kwenye rhumba letu la
kitanzania ingawa siku za nyuma kuliwahi kuwa na bendi ya akinamama watupu
ikiitwa Women Jazz ambayo kuanzia magitaa, masaxphones na kuimba walikuwa
akinamama watupu. Asia Daruwesh alizaliwa mwaka 1964. Ingawa alikuwa na asili
ya Zanzibar, maisha yake kwa kiasi kikubwa yalikuwa Zambia kuanzia utotoni hadi
anakua na huko ndiko alikopata inspiration ya kuwa mwanamuziki. Kwa hapa kwetu
Tanzania, jina la Asia Daruwesh lilisikika kwenye safu ya mwanzo kabisa ya King
Kikii mwaka 1984 akiwa na Kikii mwenyewe, Mumba Kisi, Kapelembe Coco, Samba Wa
Mikalay, Zahoro Bangwe, Mohamed Idd Control, Matei Joseph na wengine.
Alishiriki kupiga kinanda kwenye nyimbo kadhaa za bendi hii iliyokuwa ikitumia
mtindo wa Embalasasa Shika Break kama Kinyume, Dodoma Capital, Njimina, Mimi na
we, Kibwanange, Malalamiko na nyingine kadhaa huku nyimbo kama Lamanda na
Kitoto chaanza tambaa akimuachia Ally Hemed Star huyuhuyu ambaye leo
anajulikana kama muimbaji na mtunzi mzuri wa Taarab. Hata hivyo mwaka 1986
mwishoni aliihama bendi hiyo na kujiunga kwenye safu ya mwanzoni ya MK Group
wakati huo. Nyimbo karibu zote za kuanzia toleo la kwanza hadi la tatu la MK
Group amepiga kinanda yeye. Hassan Rehani sijui anakumbuka nini ukimtajia MK
Group!! Mwaka 1989 alikuwa miongoni mwa wanamuziki wanne walioihama MK Group na
kwenda kuasisi Bicco Stars. Angekuwemo na Joseph Mulenga katika group hii
lakini alirudi nyuma. Akiwa Bicco aliungana na akina Kinguti System, Fresh
Jumbe, Athuman Cholilo Mashida, Seif Rengwe, Sid Morris, Mafumu Bilal, Andy
Swebe Ambassadeur na wengine Katika bendi hii ndiko alikotunga wimbo wake wa
kwanza wa Bwana Kingo na pia akashiriki kuimba na ameimbisha wimbo huo. Mwaka
1992 alianzisha bendi yake mwenyewe akiita Zanzibar Sound ikitumia mtindo wa
Wesaka Dance akiwa na akina Bob Gad William, Hezron Ludala ama Bob Ludala,
Fariala Mbutu, na baadaye akina Mohamed Idd Control na Shaban Lendi. Wimbo
Banana ambao baadaye Bob Gad alikuja kuurudia akiwa na Twanga Pepeta
ulirekodiwa kwa mara ya kwanza na bendi hii. Aidha wimbo Hadija ambao Fariala
alikuja kuurudia na Kilimanjaro Connections ulirekodiwa nao huku Ludala akiwa
muimbaji Kiongozi. Kufariki dunia kwa Asia Daruwesh ama kwa jina la utani Super
Mama mwaka 1995 ndiko kulikohitimisha safari ya bendi hii. Ni hayo tu
No comments:
Post a Comment