Katika
mfumo wa awali bendi, ambao uliigwa toka Cuba, zilikuwa zikitumia magitaa matatu, Solo, Rythm na
Bass. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu huku rythm ikiwa na sauti
nzito kidogo ya kati, na mwisho Bass likiwa na sauti nzito kuliko
magitaa mengine. Kimuundo gitaa la rythm na la solo hakuna tofauti. Yote
yana nyuzi 6,lakini katika kutyuni kwenye amplifier, gitaa la rythm
hunyimwa treble kiasi na kuongezewa bass kiasi ili kuwa zito na si kali kama gitaa la solo, ambalo
huwa na treble zaidi ya magitaa mengine, na pia hujitokeza zaidi. Inasemekana kaka yake Dr Nico Kasanda,
ndie aliyeanzisha mtindo wa kuongeza gitaa la nne lililoitwa second
solo, au wenyewe wakiliita Mi solo. Hili lilikuwa likipigwa kwa mifumo mbalimbali katika bendi mbali
mbali. Bendi nyingine zilitumia second solo kama gitaa lililokuwa
linajibizana na solo, na bendi nyingine lilikuwa linajibizana na rythm.
Bendi ya Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza liliongeza ubunifu na
kuongeza gitaa la 5 na kuliita chord guitar.
Leo tuzungumzie
gitaa la rythm. Chombo hiki bado kinapigwa katika bendi nyingi lakini
umaaarufu wake umeshuka sana. Katika kipindi cha miaka ya 60 na 70,
gitaa hili lilikuwa na umuhimu mkubwa na wapigaji wake waliweza kubuni
staili zao wenyewe na kufanya bendi kuwa na utamu tofauti na bendi nyingine. Kwa upande wa Kongo wapigaji kama Mpia Mongongo au Porthos wa Conca success ya Johhny Bokelo Isenge, Vata Mombasa wa Lipua lipua na wengine wengi kila moja alibuni staili yake na kufanya kila bendi kuwa na utamu tofauti, hapa kwetu Satchmo,
hilo ndio lilikuwa jina la kisanii la Harrison Siwale mpiga rythm wa
Jamhuri Jazz, yeye alikuwa na staili peke yake ya kupiga rythm,
sikumbuki kusikia mtu mwingine akipiga rythm ya aina yake kabla ya hapo.
Rythm yake ilitawala nyimbo za Jamhuri wakati huo. Kumbuka wimbo kama
Mganga no 1 na 2, au Blandina. Marehemu Mzee Kasim Kaluwona nae alikuwa
na staili tofauti ya upigaji uliyoifanya Tabora Jazz kuwa na staili yake
peke yake, kumbuka gitaa lake katika wimbo Asha, au Dada Lemmy. Charles
Kazembe akiwa na Morogoro Jazz anakumbukwa katika upigaji wa rythm
kwenye nyimbo kama Wajomba Wamechacha. Hao ni wachache tu kulikoweko na
wengi marufu. Katika kipindi hiki huko Zaire kulikuwa na mipigo
mbalimbali ya gitaa la rythm, ila kitu kipya kikaanzishwa ambapo katika
ufungaji wa nyuzi ,wapiga rythm wakauondoa uzi namba nne na kuweka uzi
namba moja, hivyo kukawa na nyuzi namba moja 2 katika gitaa, hapo ndipo
akina Vata Mombasa wakaweza kuleta utamu mpya katika upigaji wa rythm. Wimbo wa Kumbora wa BAT ni wimbo ambao rythm ilipigwa kwa staili hiyo na nyimbo nyingi za wakati wa mwanzoni mwa miaka ya sabini zilipigwa na rythm iliyofungwa nyuzi za stail hiyo.
Wakati huo Orchestra Kiam wakawa wanajivunia kupiga rythm kwa spidi kali
sana,vibao kama Kamiki, Bomoto ni ushahidi wa kazi hizo. Utamu wa
ufungaji wa nyuzi kwa staili hii uliweza kusikika vizuri katika gitaa
lililopigwa mwanzo kabisa wa wimbo Andoya. Leo vionjo vya upigaji huo
vinarudi kwa njia ya ajabu sana. Vikundi vya taarab vimeanza 'kuachia
rythm' gitaa moja kubaki linapiga peke yake, japo wao hupiga gitaa la
solo lakini staili wanayoipiga ni ya gitaa la rythm enzi ya miaka ya sabini. Jambo ambalo ni wazi watu bado wanapenda sana staili hiyo, japo bendi zinaonekana kuitupa staili hiyo. Siku hizi kelele huwa nyingi kiasi
unaweza ukatembelea bendi 3 ukaona mtu anapiga gitaa la rythm lakini
husikii, kwa hiyo hata thamani ya rythm katika bendi haipo, hata wanamuziki wanaojisifu kwa kupiga rythm ni wachache wengi hudai wao wapiga gitaa bila kutaja rythm kwani inaonekana ni chombo kisicho muhimu.
Ingawa Vata Mombasa aliwika sana miaka ya 70 kama mpiga rhythm was Lipua Lipua, kuna jamaa aliyekuwa akijulikana kama Lele Nsundi. Huyu ndiye aliyepiga rhythm katika nyimbo zote za Orchestre Kiam enzi hizo. Huyu na mpiga solo Djuke walikuwa ni combination kali sana. Walifanya balaa katika kibao Moni Afinda.
ReplyDeletehttp://www.youtube.com/watch?v=RV1n6sfjJBE
Hayo mapicha ya magita yanazuia maandishi kusomeka!
ReplyDeleteNimerekibisha nategemea unaweza kusoma kama bado nitaarifu mkuu
ReplyDelete