Asubuhi ya leo nimepigiwa simu ambayo imenipa taarifa
iliyobadili sana mtazamo wangu kuhusu historia ya wanamuziki wa Tanzania.
Nimepigiwa simu na aliyenipigia akajitambulisha kuwa anapiga
simu kutoka Shirati Na kuwa aliwahi kuwa mwanamuziki zamani sana. Mheshimiwa
huyu ambaye ananambia enzi hizo alikuwa akiitwa Papaa Kabaka alikuwa mpiga
tumba wa bendi iliyokuwa inaitwa Geita
Success, imekuwa ni mara yangu ya kwanza kujua kuhusu bendi hii. Kwa kadri
ya Papaa Kabaka, bendi hii ilitokana na wanamuziki wa Kikongo waliotoka Orchestra Super Veya, bendi iliyokuwa na makao yake makuu jijini
Mwanza na ilitamba sana katika Kanda ya Ziwa mwanzoni mwa miaka ya sabini.
Ikumbukwe pia kuwa kuwa Super Veya ilitokana na kumeguka kwa Orchestra Fauvette, ambapo
kundi jingine lilimeguka na kwenda kuweka makao yake Moshi na kujiita Zaire
Success, na hatimae kupata tawi jingine lililojulikana kama Bana Afrika Kituli
palepale Moshi.
Jambo lililonipamtazamo mpya wa historia ya wanamuziki wa
Tanzania ni kuwa mpiga solo mmojwapo wa Geita Success alikuwa Mnaijeria ambae
aliyenisimulia alikumbuka jina lake moja tu la Pius, ni mara ya kwanza kusikia
kuwa kulikuwa na mwanamuziki kutoka Afrika Magharibi kuwepo nchini wakati huo,
wengi wa wanamuziki wageni walitoka Kongo, na wengi kutoka kusini mwa nchi hii,
Zambia, Zimbabwe, Malawi, na Afrika ya Kusini. Ni wazi kuna mengi yamejificha
katika historia ya muziki wa nchi hii kutokana na kutokuwa katika kumbukumbu za
maandishi.
Bendi hii ya Geita Success ilikuwa ikifanya maonyesho yake
kwenye ukumbi wa Hostel za Council wakati huo, sijui kumekuweko na maendeleo
gani ya ukumbi huo kwa sasa, hasa ukichukulia kuwa kumbi karibu zote za
serikali nchini zimeguezwa matumizi, lakini hiyo ni makala nyingine kabisa.
Papaa Kabaka hakukaa muda mrefu Geita Success, japo kuwa
anakumbuka kupokea bendi kamaJamhuri Jazz na hata Mbaraka na bendi yake na kama
ilivyokuwa kawaida zamani bendi mwenyeji ilipiga nyimbo mbili au tatu na bendi
wageni wakaendelea na show.
Papaa Kabaka
alihamia Mara Jazz ambako kadri ya aliyenieleza Ahmad Kipande pia alipitia
bendi hii akawa akipiga solo na Abdallah Ndege Mkenya aliyetokea Kindu Jazz ya
Kenya (hapa nina wasiwasi na kumbukumbu hii kuhusu Ahmadd Kipande kuna hitajika
ushahidi zaidi, na pia kuna mkanganyiko je alikuwa kiongelea Mara Jazz au
Musoma Jazz?) Baadhi ya wanamuziki wengine ambao walikuwa wakipiga kipindi
hicho ni Sosi Nyabi akipiga rhythm gitaa na kuimba, Kimaya Obange akipiga Bass Gitaa. Aliyenipa
taarifa hii kwa sasa anaitwa Simon Otieno ambaye kwa sasa ni Mchungaji pale
Shirati
No comments:
Post a Comment