Saturday, September 7, 2013

RIDHWANI PANGAMAWE TOTOO


Ridhwani Pangamawe alianza muziki katika bendi ya JUWATA akiwa na umri mdogo wa miaka 15 mnamo mwaka 1979. Ridhwani alizaliwa katika familia iliyokuwa ya wanamuziki, baba yake Mzee Pangamawe alikuwa mwanamuziki katika bendi iliyokuwa maarufu pale Iringa iliyoitwa Highland Stars bendi hii ilitikisa sana miak ya mwisho ya sitini na mwanzo wa 70, na kwa kuwa mazoezi yalikuwa yakifanyika nyumbani kwao hata mama yake pia alikuwa anaweza kupiga gitaa, na alipenda sana muziki. Kaka yake, Zuberi Pangamawe,  pia ambae nilimfahamu akiwa RTC pale Iringa alikuwa pia akijua kupiga gitaa na alikuwa kipa mzuri wa timu ya RTC mwanzoni mwa miaka ya 70. Ridhwani aliaanza kuonyesha kipaji cha kupiga kinanda akiwa bado mdogo sana wa umri kama miaka mitano ambapo kaka yake Zuberi alimkuta kwa mara ya kwanza akipiga kinanda, ambacho mwenyewe Ridhwani husema alikuwa akipenda kupiga kila aliporudi shule hata ule wakati wa mchana alipokuwa akirudi kula chakula cha mchana alikuwa lazima aguse kinanda, tabia ambao anazeeka nayo ya kupenda kufanya mazoezi sana. Baada ya kumaliza shule ya msingi Iringa alikuja Dar es Salaam ili aweze kuendelea na masomo ya sekondari, wakati akiwa hapa kaka yake aliwaambia wajomba zake ambao ndio walikuwa wenyeji wake kuwa Ridhwani ana uwezo wa kupiga kinanda. Katika kipindi hichohicho Waziri Ally Kisinger, aliacha bendi ya JUWATA  na kurudi kwenye bendi yake ya awali ya The Revolutions(sasa Kilimanjaro Band), hivyo pakawa na pengo la mpiga kinanda kwani wakati huo bendi kubwa zote zilikuwa na mpiga kinanda, na wimbo wa Kakere Sogea Karibu ulikuwa ndio unatamba katika anga za Afrika Mashariki kwa utamu wa kinanda cha Waziri Ally, hivyo basi Msondo walianza mkakakati wa kupata mpiga kinanda, wapiga vinanda kadhaa mashuhuri wa  wakati huo walijaribu bahati zao kujiunga na bendi hii wakiwemo Kassim Magati na hata Ally Tajruna ambaye alipigia bendi hiyo kwa mwezi mzima. Wajomba zake Ridhwani, ambao walikuwa wapenzi wakubwa wa Msondo na walikuwa wakiishi jirani na Mzee Joseph Lusungu walimfuata Mzee huyo na kumtaarifu kuwa wana mdogo wao ambae anaweza kupiga kinanda na Ridhwani akakaribishwa Msondo kufanyiwa usaili na kukabidhiwa kwa Mzee Mponda ili aweze kumsaili, kwa kuwa alikuwa hajawahi kugusa kinanda cha umeme, kwani alikuwa akitumia kinanda cha kujaza upepo alibabaika kidogo na Mzee Mponda alimuacha na kutokumchukulia maanani, lakini wakati huo bendi ilikuwa ikifanya mazoezi ya wimbo Dunia Uwanja wa Fujo charanga kali lililohitaji umakini, akawa ameachwa anaendelea kwenye chumba kimoja anapigapiga kinanda peke yake, ule uhuru ukamfanya awe jasiri akaanza kupiga nyimbo alizokuwa anafahamu, jambo lililowavutia wanamuziki wenzie waliomsikia kiasi cha kuacha mazoezi na kumfuata na kumtuza pesa, jambo ambalo si rahisi kwa mwanamuziki mgeni ambaye alikuwa hajawahi hata kupigia bendi yoyote kabla ya pale, na tena wakiwa mazoezini.
(Picha kwa hisani ya www.viwanjani.blogspot.com)
Mara moja wanamuziki walikubaliana kuwa ajiunge nao. Aliendelea kupiga nyimbo zilizoachwa na Waziri, na kuchukuliwa rasmi kama mwanamuziki wa Msondo,  kwa vile alikuwa bado mdogo kwa umri na umbo, akapewa jina la utani Totoo. Wimbo wake wa kwanza kurekodi akipiga kinanda ulikuwa wimbo Zhuleka utunzi wa Shaaban Dede. Bahati mbaya baada ya muda si mrefu kinanda kikaharibika na kwa muda wa zaidi ya miaka miwiwli akawa  hapigi tena kinanda, akahamia kwenye magitaa, alianza na kupiga second solo, ambapo ujuzi wake unasikika katika nyimbo kama Kaka Selemani, Siwema, kisha akawa pia anapiga bezi, katika wimbo Msafiri Kafiri alikuwa akipiga bezi lakini Mzee Mponda akaondoka katika bendi wiki moja kabla ya siku ya kurekodi na ndipo akahamia katika gitaa la solo na kulipiga vizuri sana katika wimbo huo. Hatimaye 1994 akaanza tena kupiga kinanda baada ya bendi kupata vyombo vipya. Akarekodi nyimbo kadhaa ukiwemo wimbo wa Olee. Ridhwani hajawahi kuhama katika bendi hii na mwenyewe anasema hana mpango wa kuhama kwa kuwa anaona kwa kweli hakuna tofauti kubwa katika kuhama bendi. Kati ya nyimbo ambazo aliwahi kupiga anazozipenda ni Queen Kasse

No comments:

Post a Comment