Katika miaka ya 70 mwishoni kulikuweko na mgogoro mkubwa
kati ya Tanzania na Kenya, mgogoro ambao ulifikia hata kufunga mipaka kati ya
nchi hizi mbili. Malumbano makali ya kisiasa yaliendelea katika vyombo vya
habari vya nchi hizi mbili, na ilifikia kuwa kila upande ulilaani siasa za nchi nyingine, kati ya
malumbano ninayoyakumbuka ambayo yaliyokuwa yakiendelea katika radio ni pale Tanzania ilipoiambia
Kenya kuwa ni nchi ya Manyang'au yenye utaratibu wa ‘Man eat man society’, nao Kenya wakajibu Tanzania ni nchi
ya ‘Man eat nothing society’. Vibonzo vya magazeti ya Kenya vilijaa picha za
kejeli kwa nchi ya Tanzania, na kibonzo kimoja kikionyesha kiongozi wa China Mao Tse Tung akiwa amempakata Mwalimu Nyerere, wakati Mzee Kenyatta akionekana
akitoka mbio kali, viliiudhi sana serikali ya Tanzania.
Nia ya madhumuni ya habari ninayoandika hapa ni Je, siasa
ilihusika katika kutoa maelezo ya kifo cha Mbaraka Mwinyshehe?
Katika miaka yote kutokana na maelezo yaliyotolewa na vyombo
vya habari vya Tanzania, ilionekana kuwa kama Mbaraka angepewa matibabu
aliyostahili angeweza kupona, na kuwa kilichosababisha kifo chake ni kunyimwa
damu kwa kuwa Mbaraka alikosa fedha za kulipia damu katika hospitali aliyokuwemo.
Katika chambua chambua zangu nimepata nakala ya maelezo aliyotoa mwanamuziki
mmoja Mtanzania aliyeshuhudia ajali na kushiriki hata kuwaita wanamuziki wa
Mbaraka kwenda hospitali aliyofia marehemu yananipa picha tofauti na niliyokuwa
nayo miaka yote.
Zebedee Japhet Kinoka au maarufu kama Super Zex ni
mwanamuziki wa siku nyingi sana ambae pamoja na bendi nyingine aliwahi kupigia
Amboni Jazz, Salna 5 Brothers za Tanga na Villa Negro iliyokuwa na maskani Mombasa japo
iliongozwa na wanamuziki kutoka Tanga.
Kwa maelezo yake mwenyewe mwazoni mwaka 1979 aliamua
kuvuka mpaka na kwenda Mombasa katika kutafuta maisha kimuziki. Siku ya tarehe
12 Januari 1979 alikuwa anatoka maeneo ya Kisauni kumtembelea Mtanzania mwenzake
aliyekuwa na hoteli huko, ambaye
pia walitoka kijiji kimoja Malamba
huko Tanga. Anasema alipofika karibu na Kongoya Church aliona gari aina ya Peugot 404 nyeupe ikitoka
upande wa Bush Bar na kwa spidi kali ikaenda na kuligonga roli moja lililokuwa likitokea upande mwingine. Ilikuwa mchana kiasi kama saa 7 hivi. Watu
wakakimbilia kungalia ajali akiwemo yeye. Na mara moja akamtambua Mbaraka na
kuwambia watu kuwa huyo ni mwanamuziki Mtanzania anaitwa Mbaraka Mwinyshehe.
Katika gari lile kulikuweko watu watatu Mbaraka alikuwa amekaa mbele pamoja na dereva. Dereva na pasenja aliyekuwa nyuma walikufa palepale, ikalazimika kuanza kukata mabati ili kumuondoa
Mbaraka aliyekuwa amebanwa miguu katika gari lile lililoharibika, yeye alikuwa bado hai. Wakati
kazi hiyo inaendelea Zebedee alikimbilia Kengeleni Bar ambapo Jamhuri Jazz Band
( Bendi ya Watanzania) ilkuwa ikipiga muziki nakuwambia kuwa mwenzao kaumia
sana, nao wakatoka mbio, wakiwemo akina Harrisson Siwale. Mbaraka aliweza
kutolewa kwenye gari na kupelekwa kwenye hospitali ya Makadara. Zebedee pia akatumwa
kuwafuata wanamuziki wa bendi ya Super Volcano ambao wakati huo walikuwa wakipiga Zambia
Bar, wanamuziki walipofika hospitali wakaambia watoe damu na wakaanza kukwepa kutoa damu kwa
visingizio mbalimbali. Muda si mrefu Mbaraka Mwinyshehe akafariki. Mbaraka
alifarika 12 Januari 1979 akiwa na umri mdogo wa miaka 34 tu. Hakuna maelezo popote ya huyu shahidi kuwa kukosekana kwa pesa ndio kilikuwa sababu ya kifo cha Mbaraka
Kwanza ifahamike kuwa ni Tanzania iliyofunga mpaka wake na Kenya. Mpaka kati ya nchi hizi ulikuwa wazi upande wa Kenya. Ni kweli siasa zilitawala sana kifo cha Mbaraka ambaye alionekana katika macho ya baadhi ya watawala wa enzi hizo kuwa ni msaliti pale alipokwenda nchi ya 'Manyang'au' kutafuta maisha. Pamoja na mchango wake mkubwa, Mbaraka hakupewa heshima inayostahili katika mauti. Lakini Mbaraka alikufa akiwa katika harakati za kutafuta maisha yake mwenyewe na ya familia yake.
ReplyDeleteDu inasikitisha ndugu mola hawasamee hawa jamaa
ReplyDelete