HARRISON SIWALE, MBARAKA MWINYSHEHE MWALUKA NA ABDUL MKETEMA |
Nimetoka
kuongea na Mzee mmoja ambaye nilimuomba anitafutie habari za Harrison Siwale aka ‘Satchmo’, ambaye alikuwa mpiga
rhythm mahiri na maarufu sana katika miaka ya sabini, Harrison alikuwa na
staili ya pekee ya upigaji wa gitaa wa kudokoa nyuzi na kupata aina ya pekee ya
mlio wa gitaa. Kati ya nyimbo ambazo upigaji huu unasikika ni katika nyimbo za
Jamhuri Jazz Band kama vile Mganga 1
na 2, Blandina na kadhalika. Pamoja na bendi nyingine Harisson aliwahi
kupigia Atomic na Jamhuri Jazz Band zote za Tanga, na kisha kuvuka mpaka na
kuwa na makazi Mombasa kwa muda mrefu ambako aliendelea na muziki. Kwa kadri ya
maelezo niliyopewa leo na huyu Mzee niliyemuomba anitafutie habari ili nijue yu
wapi huyu mwanamuziki siku hizi? Haya ndio aliyonambia.
Baada ya kufa kwa yale
makundi ya Simba wa Nyika na Les Wanyika, Harrison Siwale alianza kupiga muziki
wa Injili katika eneo la Kilifi. Akawemo katika kundi lililokuwa likifanya
maonyesho yake katika miji mingi ikiwemo Mombasa na Nairobi. Umahiri wake wa
kazi ukamfanya mwenye vyombo vya hilo kundi alilokuwemo Harrison kumuamini sana
na kumuachia awe kiongozi wa kundi hilo na kuwa huru kuzunguka sehemu
mbalimbali. Inasemekana Harrison akapata tamaa ya kuingia mitini na vyombo
vile, hivyo ghafla akapotea. Taarifa zikamfikia mwenye vyombo kuwa vyombo vyake
viko njiani kuvushwa kungia Tanzania kupitia mji wa Lungalunga. Mwenye vyombo
akaweka mtego hapo na Harrison akakamatwa hapo akiwa na vyombo hivyo, kesi
ilifika mahakamani na akahukumiwa kifungo cha miaka mitatu. Baada ya hapa kuna
hadithi mbili, moja ikisema alifia gerezani Shimo la Tewa, na nyingine ikisema
alifariki baada ya kumaliza kifungo chake.
Je,
nini hasa kilitokea? Najaribu kuwasiliana na watu mbalimbali kupata hadithi
zaidi kuhusu mwanamuziki huyu.
No comments:
Post a Comment