Wednesday, April 3, 2013

HISTORIA FUPI YA JAMHURI JAZZ BAND JJB


Kwa mara ya kwanza niliwaona 'Live', Jamhuri Jazz Band wakipiga katika ukumbi wa Community Centre Iringa, ukumbi maarufu kwa wenyeji wakati huo kwa jina la Olofea senta (Welfare Centre). Ni vigumu kuelezea jinsi nilivyokuwa najisikia kwani nilikuwa sidhani kama kutakuja kuweko na wanamuziki wanapiga vizuri namna ile. Lakini katika wote mpiga rythm guitar Harison Siwale, aliyejulikana kwa jina la Satchmo, alikuwa na anabakia kuwa mpiga gitaa aliyenifurahisha kuliko wote. Kwanza alikuwa na staili ya peke yake, na mpaka leo nikisikiliza nyimbo zake kama vile Blandina, Mganga no 1, Maria bembeleza mwana au Ewe ndege, nabaki kusifia kuwa huyu bwana alikuwa na kipaji cha pekee. Kuna rafiki yangu aliwahi kumuuliza wakati ule huwa anapataje mawazo ya kupiga gitaa lake kwa staili ile? alijibu kuwa huwa anajaribu kupiga sauti za viumbe mbalimbali wa porini katika gitaa lake.
Wanamuziki waliokuwa katika bendi ya Mkwawa High School,  Manji, Sewando, Danford Mpumilwa, Askofu Kakobe watakumbuka jinsi walivyoweza kupata nafasi ya kupiga pamoja na bendi hii kila ilipokuja Iringa mjini, maana hizo ndiyo zilikuwa taratibu wakati huo lazima bendi kubwa ikija, wanamuziki wadogo huomba Kijiko, na kama unaweza kuimba au kupiga vizuri unaachiwa nafasi ili muhusika akatafute mpenzi. Bendi ikifika katika mji, kama mji ule una bendi basi nao watapata nafasi ya kushirikiana na wageni.  Bendi hii ilianza kwenye miaka ya 50 ikiwa ikijulikana kama Yanga Nyamwezi Band, Kiukweli ilikuwa ni Young Nyamwezi Band, bendi iliyokuwa imetengenezwa kwa ajili ya Vijana toka Tabora waliokuja kukata mkonge katika mashamba ya mkonge yaliyokuweko Tanga miaka hiyo. Na baada ya Uhuru ikajulikana kama Jamhuri Jazz Band, kifupi JJB japo kifupi hicho baadae kilidaiwa kuwa kilikuwa kifupi cha jina mwenye bendi Joseph Bagabuje. Wakati wa uhai wa Jamhuri Jazz bendi Tanga kulikuwa kuna waka moto kwa vikundi maarufu katika Afrika ya Mashariki kuwa vyote katika mji huo. Atomic Jazz, Amboni Jazz, Lucky Star, Black Star. Kwa vyovyote Tanga ulikuwa mji wa starehe wakati huo, hasa ukikumbuka kuwa kulikuweko na bendi nyingine ambazo hazikuwa maarufu labda kutokana na aina ya muziki zilizokuwa zinapiga. Kama vile ile bendi ya Magoa The Love Bugs ambayo ndiyo hatimae ilikuja kuwa The Revolutions na sasa Kilimanjaro Band
Mbaruku Hamisi,Abdallah Hatibu, Zuheni Mhando

Eliah John, Alloyce Kagila, Musa Mustafa

Yusuf Mhando, Joseph Bagabuje, Rajabu Khalfani


George Peter, Harrison Siwale, Wilson Peter

2 comments:

  1. Yaani wee acha tu bwana John Kitime kwa kunikumbusha enzi hizo; na huo wimbo wa Mganga- wee si umezungumzia gitaa la ridhimu la Harrison Siwale? Sasa hilo gitaa lilikua likipigwa nafikiri kumalizia kipindi fulani cha muziki kwa salaam kabla ya taarifa ya habari ya saa mbili jioni. Hiyo ridhimu ya Mganga ni kama "saini" (signature) au ishara fulani. Leo tungeita hiyo "jingle" yaani ingeuzwa kwa bei ya juu sana na kutumiwa na TV na kumfanya jamaa tajiri. Mimi n'likua naipenda hiyo sehemu ya kati ya Mganga wakati Ridhimu linaingia kiasi ambacho ilinipa mshawasha na mahanjam hadi nikatunga wimbo nikauita "Sawa Sawa" kutokana na zile hisia kali. Kazi unayofanya kuelezea haya mambo na kuweka picha ni hazina kubwa. Ingefaa hizi makala zako na picha uzichape pia kitabu. Hii ni ghala na maktaba ya vizazi vijavyo. Pia ... Zisomwe na wengi zaidi wasiopata fursa ya kutumia tarakilishi (kompyuta) maana aghali.

    ReplyDelete
  2. Hakika jamhuri jazz ndio chimbuko LA wanamuziki nguli kama Wilson kinyonga na nduguze ambao waliitikisa Kenya na simba wa nyika,hakika naupenda sana ule wimbo wa shingo ya upanga...

    ReplyDelete