Wednesday, July 4, 2012

Paul Daniel Gama, Mwanamuziki wa Central Jazz na Dodoma Jazz Part 2


Katika jitihada zake za kujifunza gitaa la bezi alikuwa kila mara akiwahi mazoezi na kujaribu kujifunza gitaa la bezi. Hilo lilikuwa gumu mpaka pale bendi  ya Lake Jazz Band ilipotembelea Dodoma. Bendi hiyo wakati huo ikiwa na wanamuziki kama Shem Karenga  akiwa anapiga gitaa la bezi, Mzee alum ambaye alikuwa na ulemavu wa macho, mwanzo alikuwa akipiga gitaa la solo na baadae akahamia kupiga gitaa la rhythm wakati gitaa solo lilikuja kupigwa na jamaa aliyeitwa Kally. Kutokana na simulizi ni wazi kuwa wanamuziki wa kutoka Burundi walikuwa wengi sana nchini wakati huo. Pia katika bendi hiyo alikuweko Mzee Juma Kitambi, mtunzi wa wimbo maarufu wa Rangi ya Chungwa.
Gama Bassist Dodoma Jazz
Gama alichukua nafasi hii kumfuata Mzee Salum ili aweze kumfundisha gitaa. Kwa kuwa wanamuziki wengine walikuwa wakitoka kwenda kutembea Mzee Salum alibaki nyumbani na hivyo Gama alichukua nafasi hiyo kumnunulia sigara Mzee Salum ana kumsihi amfundishe gitaa nae alifanya hivyo na Gama akatokea kuwa mpiga bezi mahiri.
Katika kipindi hiki akatokea mfanya biashara Mohamed Omar Badwel, huyu alikuwa na gereji na studio ya kupiga picha, aliweza kwenda Mombasa na kurudi na seti ya vyombo na kuanzisha Dodoma Jazz Band. Gama akahama Central Jazz Band na kujiunga na wanamuziki wengine walioanzisha Dodoma Jazz. Band ilianza ikiwa na mpiga solo Hassan Mursali mwanamuziki mweny asili ya Malawi, siku hizo ikiitwa Nyasaland alikuwa ndie mpiga solo, lakini aliwaacha baadae na kujiunga na NUTA Jazz Band, upigaji wake wa solo unaweza kuusikia katika kusikiliza kibao kimoja maarufu cha NUTA, kilichoitwa Dunia Njema Kukaa Wawili.
Hasan alikuwa mtu wa kuhama hama hatimae alipoteza uwezo wa kusikia jambo ambalo lilihusishwa na kuhamham kwake kwani ushirikina ulitawala sana wakati huo, kama maelezo yanayofuata yanavyoonyesha. Dodoma Jazz ilikuwa pia inafanya ziara katika sehemu nyingi , kama vile Iringa, Mbeya ,Tabora, Dar es Salaam na kadhalika, lakini safari moja ya kwenda Kilosa ilifanyika ikiwa na lengo la kumfuata Abel Barthazal aliyekuwa akipiga katika bendi ya Kilosa Jazz. Bendi  ilipokelewa vizuri na wakafanya maonyesho yao Kilosa na hatimae kuondoka na Abel. Siku chache baade wakati huo Mzee  Mohamed Omar, mwenye bendi alikuwa kasha mnunulia suti kadhaa Abel, ukaja ugeni toka Kilosa wakiwa na barua yenye maelezo kuwa ikiwa Abel Hatarudi Kilosa, mmoja wa wanamuziki wa Dodoma Jazz atafariki, na barua hii ililetwa kwa mkono na mjumbe ambae alisisitiza wakishaisoma mbele yake ndio anaondoka. Abel alirudishwa Kilosa mara moja.
Baada ya hapo aliyekuwa meneja wa bendi Ramadhan Waziri alitumwa Burundi kwenda kutafuta wapigaji, siku alipokuwa anarudi na wapigaji wapya akakutana kwenye treni na Rashid Hanzuruni, mpiga solo mahiri sana ambaye upigaji wake husikika katika wimbo  Napenda nipate lau nafasi
Hanzuruni alikuwa kaiacha Tabora Jazz baada ya  kutokea ugomvi mkubwa ambapo alipoteza meno kadhaa, hivyo alikuwa kwenye hilo treni akielekea Dar es Salaam kumfuata mpigaji mwenzie Samba ambae alikuwa NUTA Jazz. Ramadhani aliweza kumshawishi hanzuruni akabaki Dodoma Jazz ambako alikaa kwa muda na hatimae akaja kuchukuliwa na Sama ili aingie NUTA Jazz, ndoto hiyo haikufanikiwa kwana NUTA alikuweko mpigaji mahiri  Hamisi Franco, hii ndiyo ilipelekea Hanzuruni kwenda Western Jazz Band



1 comment: