Bendi ya Orchestra Makassy chini ya Mzee Makassy, iliingia nchini
ikitokea Uganda ikitwa Jamboz mwaka 1975 ilianza kupiga katika sehemu
mbalimbali Dar es Salaam ikiwemo ukumbi maarufu wa New Africa. Ukumbi wa
Hunters Ubungo ulikuwa ndio ukumbi wa nyumbani wa bendi hii. Wapigaji maarufu
kama Mose Se Sengo maarufu kwa jina la Fan Fan pia ailipitia katika bendi hii
wakati akiwa nchini hapa ambapo pamoja na bendi hii pia alipigia Super
Matimila. Kati ya waimbaji maarufu waliokuwa katika bendi hii wakati wa mwishoni
ya miaka ya sabini ni Isihaka Baharia Gobby, Dingituka Molay, Mbombo wa Mbomboka na
Mzee Makassy mwenyewe. Mwezi September 1977, jambo la kusikitisha sana
lilitokea, mwanamuziki Gobby aliuwawa katika mazingira ya kusikitishwa,
alichinjwa kama kuku. Kuna maelezo mbalimbali kuhusu siku hii na siku
zilizofuata.
Kadri ya habari toka kwa mmoja wa wanamuziki ambaye
anasema anakumbuka siku yule jamaa alipochukuliwa kwenda kuuwawa, kuwa ilikuwa
Jumapili na bendi ya Makassy walikuwa
wamekwisha toka kupiga dansi la mchana la siku hiyo, mwanamuziki huyo ambaye
kwa wakati huo alikuwa bendi ya Western lakini alikuwa kwenye masikani ya
wanamuziki wa Makassy, yaliyokuwa kwenye maeneo ya Hunters Club ambako kulikuwa
na vyumba vya wanamuziki kikiwemo chumba cha Gobby. Kwa maelezo ya mwanamuziki
huyu, alikuja mtu aliyekuwa akifahamiana na marehemu na akamwomba waondoke wote
na hiyo ikawa ndio mara ya mwisho kuonekana maiti ilikutwa barabara ya kuelekea
ya Bagamoyo, ikiwa imechinjwa.
Mpenzi wa muziki maarufu aliihadithia hivi, ‘Hii
stori naikumbuka kama imetokea jana. Kabla ya kifo chake nilimuona Marehemu
Gobby akipiga kwenye harusi na Mzee Makassy kwenye ukumbi wa FFU Ukonga. Siku
chache baadaye akauawa na maiti yake ikaokotwa maeneo ya Kunduchi. Miaka
hiyo tulikuwa tunaishi Maweni Street, Upanga nyuma yetu Mtaa wa Aly Khan
alikuwa anaishi Ofisa wa Ubalozi wa Zaire. Ubalozi wa Zaire ulikuwa Mtaa wa
Maliki mkabala na Makao Makuu ya Skauti. Siku ya kifo cha Gobby na wiki
iliyofuatia palikuwa na bonge tension baina ya Wanamuziki wa Kikongo na Wakongo
wengine pale nyumbani kwa Ofisa wa Ubalozi na Ubalozini kwao Mtaa wa Maliki.
Kesi ya kuuawa Marehemu Gobby iliisha kimya kimya nadhani ni kwa sababu za
diplomasia ambapo ulihusisha ofisa wa ubalozi na kifo cha Marehemu Gobby.
Nina hakika kwa asilimia nyingi sana baada ya kuuawa
Marehemu Gobby ndipo Marquiz walipopiga ile nyimbo ya Wandugu Tuwe Na Huruma.
(Wimbo huu ulitungwa na King Kiki ambaye amekuwa akikana kuwa wimbo huo haukuwa
na uhusiano na kifo hicho). Marehemu Gobby alikuwa
bonge la show man jukwaani: alikuwa mwimbaji na mchezaji mzuri sana pia alikuwa
mlimbwende sana na kofia zake za Jackson Five, Mashati ya Slim fit ya mikono
mirefu, mabugaluu na viatu vyake vya laizoni. Alikuwa na staili yake moja ya
kucheza na kurusha mguu kuzunguruka microphone na wakati mwingine kufanya kama
anajikata ngwala na kupiga hatua za upesi upesi kama anakimbia huku kasimama
pale pale alipo! Walikuwa wakifanya vituko vyao jukwaani na Marehemu Remmy
akiwa kwenye tumba hata kucheza ilikuwa vigumu kwa kuwastaajabia! kama aliweza
kukamata macho yetu kina kaka kwa namna ile basi aliweza kuteka macho na nyoyo
za kina dada kwa namna nyingine zaidi! Hii issue sidhani kama kuna mtu
aliyetaka kuhusiana nayo kwa jinsi ilivyokuwa complicated. Siyo wanamuziki hata
polisi wakati ule hawakutaka kutoa taarifa rasmi ya yale mauaji na sidhani kama
kuna mtu alipandishwa kizimbani kujibu mashtaka! Hata hapa tunapoandika sote
tunaizunguka zunguka! Si ajabu kabisa Mzee Kikii kusema nyimbo hii ilitokea tu
ikatungwa baada ya mauaji ya Marehemu Gobby.’ Wengi wanaozungumzia mkasa huu
hukubaliana kuwa sababu ilikuwa ni wivu wa mapenzi. Kuna wengine husema
mwanamuziki huyu ambaye pia alikuwa fundi cherehani mzuri alianza urafiki na
mke wa Afisa wa Ubalozi wa nchini kwao na ndio maana aliuwawa, lakini meneja wa
kundi hilo wa wakati huo aliwahi kunambia kuwa katika kesi iliyowahi kufanyika kabla
ya kifo hicho kibaya kwa tuhuma hizo na yeye mwenyewe akiweko, Gobby alikana
kuwa na uhusiano na mama huyo, na alisisitiza kuwa alikuwa na uwezo wa kupata
wapenzi wengine wengi tu akiwa kazini kwake, hivyo hakuwa na sababu na kufuata
mke wa kiongozi wake. Ni hivi juzi tu mpenzi mwingine wa muziki wa wakati huo
akanambia kisa cha kuuwawa Gobby ni wivu wa mapenzi na mpenzi mwenyewe alikuwa
anaitwa Hidaya aliyekuwa akiishi Upanga karibu na shule ya Shaaban Robert. Haya
ni wazi bado mapengo ni mengi katika mkasa huu. Lolote jipya litakalopatikana
katika mkasa huu tutalimwaga hapa.
No comments:
Post a Comment