KASSIM KARUONA |
MAKALA HII ILIYOANDIKWA January 2, 2009, NA NYINGINE NYINGI KUHUSU TABORA UTAWEZA KUZISOMA-uyui.wordpress.com/
Aliwashangaza
wengi kwa Gita lake la Rythm lililo ongoza baadhi ya nyimbo kama dada Helena,
chakula kwa jirani na nyinginezo
Watu wengi Tabora walimfahamu kwa jina la Kassim rhythm hata wasisumbuke
kujua jina la baba yake
Tabora, Dar na Kigoma vyakumbwa na wingu zito la simanzi.. kifo chake
chatonesha donda la marehemu Hanzuruni, Wema Abdalla, Msafiri Haroub, Issa
Ramadhani na Halfani Juma
________________________________________________________________________
Kifo mara zote huja kwa kushitukiza, ndivyo zilivyokuja taarifa za
kifo cha marehemu mwamamuziki mkongwe Kassim Hassani Kaluona maarufu kama
Kassim Rythm aliyefariki dunia siku ya Jumatano ya novemba 22, 2006 Jijini.
Marehemu alikuwa ni mwanamuziki wa Tabora Srar zamani Tabora Jazz au
Segere matata iliyokuwa na makazi yake kule Tabora Lumumba kwenye makutano ya
mitaa ya Rufita na mtaa wa Fundi. Kwa sasa Bendi hiyo inaitwa Tabora
Star.
Taarifa za kustua za msiba
Ingawa taarifa hizo zilikuwa zimeenea Jijini tangu siku iliyofuatia
ya Alhamis majira ya mchana wengi walizipata taarifa za kifo cha Kassim rythm
katika vipindi vya michezo na kwenye taarifa za habari za
televisheni.Ilishitua. Nilimuangalia Mzee Shem Ibrahim Karenga alipokuwa akitoa
taarifa za msiba kwenye Luninga, alikuwa amekosa ile nuru yake. Hilo
lilitegemewa kama ambavyo imewatokea watu waliokuwa wakimjua marehemu Kassim
walipopata taarifa za kifo chake. Kwa Mzee Shem Karenga hili ni pigo kubwa na
ni zaidi, alikuwa na marehemu katika kazi na walikuwa maswahiba wakubwa kwa
zaidi ya miaka 30. Umri wa mtu mwenye familia.
Wasifu
Sikumfahamu sana marehemu zaidi ya kuzifahamu kazi zake.
Siwezi kujinadi kuwa nilifahamu. Tulimfahamu marehemu Kassim kwa kumuona
kama ni mwanamuziki mtanashati, au mfua uji kwa lugha za enzi hizo. Jukwaani
hata nje ya jukwaa hakuwa muongeaji kama marehemu Msafiri haroob
aliyekuwa Hakuwa mzungumzaji sana. Zamani wakati nasoma Tabora enzi zile
za miaka ya sabini tulikuwa tunakwenda kuangalia mazoezi ya Segere
Matata. Wakati ule watoto au wanafunzi hatukuruhusiwa kuingia Dansini
hivyo mara nyingi kama kulikuwa na dansi tuliishia nje . tuliusikiliza
muziki kwa nje na mara nyingi tulikaa katika baraza ya mama mmoja maarufu sana
Tabora mama Adeni. Mama yake (Ismail Aden Rage huyu wa Moro star). Mama huyu
alikuwa na Hoteli iliyoitwa Tanzania Hotel iliyokuwa mtaa wa Rufita. kwa wale
wanaojua Tabora na hulka zake, katika hoteli ile kulikuwa na Baraza kubwa sana
ya kahawa. Tanzania hoteli ilikuwa pua na mdomo kutoka Lumumba uliokuwa
ukumbi wa Tabora Jazz.
Hamu ya kwanza enzi hizo ilikuwa ni kuwajua wanamuziki. Hao ndio
walikuwa nyota wetu stars. Vijana wa sasa nyota wao ni kina Eminem. Basi hapo
ndipo nilimfahamu marehemu Kaka Kassimu na tangu enzi zile mpaka wakati
nilipokuwa namuona alikuwa unaweza kusema hazeeki. Baada ya miaka 20 alibaki
kuwa na umbo lile lile na sisi wengine tutaanza kuonekana kama tunalingana naye
umri.
Kassimu alibaki marehemu Issa Ramadhani na Mzee Kitambi walipoenda
Msondo na Msafiri alipoenda Paselepa
Nakumbuka mwaka 1978 Bendi ya Msondo walikuja Tabora
walipoondoka baada ya kumaliza ziara yao baadaye zikaja habari kuwa
Marehemu Issa Ramadhani (Baba Isaya) na Mzee Hamisi Kitambi walikuwa wamekuja
Dar na kwamba wamejiunga na Msondo. Kuna watu walilia kama kafa mtu kwa kuhama
kwa wanamuziki hao.wakati ule hakikuwa kitu cha kawaida. Nakumbuka kuna rafiki
yangu mmoja Mohammedi Hassan Kaombwe aliuliza kwani na Kassimu naye kaondoka!
Alipojibiwa kuwa Kassimu yupo hajaondoka watu wote wakatuliza mioyo. Huyo ndio
marehemu kassimu. Msondo Ngoma katika miaka ya 1980 ilinuniwa na wakazi wengi
wa Tabora kwa kuwachukua wanamuziki Issa na Mzee Kitambi.
Kazi zake
Hapa ndipo niliposema kuwa nimezifahamu na kuzisikiliza sana kazi zake hii
ni kwa sababu niliipenda sana Segere matata, segua segua. Niliupenda pia muziki
wake wa uliokuwa na mahadhi ya kimanyema na kisonge. Mahadhi ambayo hata
marehemu Marijan alikuwa anapiga.
Alishiriki kupiga gita la rythms katika nyimbo karibu zote huku
Shemu Karenga akipiga gita la solo na kuimba pamoja na kina marehemu
Msafiri Habob aliyehamia Paselepa bbadaye miaka 1980. Marehemu Kassimu alipiga
gita la rythm jinsi anavyotaka. Kwa wale wataobahatika kusikiliza wimbo wa dada
helena uliopigwa na Tabora Jazz wanaweza kuelewa ninachozungumzia, gita lake
ndio lilikuwa kiongozi katika wimbo huo. Nyimbo nyingine ni pamoja na Halima,
Kilimo, Chakula kwa Jirani, Alhamdulilah, kazi ya kulima ndio maisha ya watu
wote, samba yasika, dada Remi, dada Asha na 1 na na 2, dada zena, dada Helena
jitulize, Ruth, belaombwe, hasira hasara, uliopigwa kwa staili ya
kavasha na nyingi nyinginezo nyingi ukiwemo merina nihurumie. Zainab,
akasema kuwa
Kiigizo kwa wanamuziki chipukizi
Moja kati ya sifa za wanamuziki wa zamani aliwemo marehemu Kassimu ni kuwa
kiigizo. Wakati ule Tabora na hata mikoa ya jirani kama Kigoma , Rukwa na
Shinyanga kila kijana alipenda awe kama Kassim, Shemu, Athuman Tembo au Salum
Luzila.
Wapo vijana wengi waliofuatia ambao muziki wa kaka zao kina Kasimu
uliwavutia. Orodha ni ndefu, kina Juma Banduki aliyekuwa mpiga kinanda wa Mkote
Ngoma na hatimaye Sikinde, kina Madaraka Moris (kiwembe), Kibonge, kina
Fransis aliyeanza kupiga gita akiwa na sare za shule ya Kazima sekondari
lakini akaweza kumudu masomo na muziki, yupo kaka yangu Rehani Juma
(Profesa wa munisa ndesa) na wengineo wengi ambao walivutiwa na kazi za
wanamuziki hawa wakongwe kina kasimu.
Buriani Kassim
Kassim umetangulia mbele ya haki ambako sisi sote tunakuja huko. Kwa kiasi
nilichofahamu kazi yako isingekuwa haki kuacha kukuandikia taazia hii ewe
kassim rythm. Kuna siku nilishawahi kumuambia komredi wangu mmoja anayeandikia
Gazeti moja maarufu la wiki hapa nchini kuwa itafika siku watu watauliza hivi
Shaaban Robert, Hukwe Zawose, Athuman Khalfan, Mathias Mnyapala, Abbas Mzee,
Juma Kilaza, Salim Abdalla, Patrick Balisidya au Marijan Rajab na Saleh
Ramadhan Mwinamila ndio kina nani?
Kassim kama mashujaa wenzako mmelifanyia kazi kubwa Taifa hili
kupitia sanaa na ubunifu wenu, mkaitangaza nchi hii (njii hii) ndani na
nje ya mipaka yake. Mmefanya kazi kubwa lakini kama wenzako mmeondoka kimya
kimya. Ndivyo walivyo watu wenye matendo makuu. Tuliwakumbuka kwa siku mbili
tatu baadaye tukashika hamsini zetu. Tunayajua zaidi mashairi ya shake Spear ya
mwaka 1600 kuliko mashairi ya Saadan Kandoro. Haya ni makosa makubwa. Tunapaswa
tuwakumbuke mashujaa wetu ninyi kama kielelezo cha shukurani. Wakati wengine
waliopo Marekani sasa hivi wanatafuta asili zao root. Sisi angalau
tunaijua asili yetu basi tuanzie hapa. Buriani kassim, Msiba wako nimeutumia
kama jukwaa la kuelezea kile kilichiokuwa kinaniganda kwa siku nyingi. Nisamehe
kwa hilo. Tunakuombea duaa wakati huu tunauanza mwaka 2009.Buriani..
Nayathamini sana unayotuasa sisi wanamuziki wapya,yatubidi tuyatafakari na kuyafanyia kazi kwani ni mara chate sana kumpata mtu kama wewe kitime kutuelimisha.Hivi sasa vyombo vya habari kama magazeti,TV,Radio kuna rushwa tupu,ambayo na yenyewe kwa kiasi kikubwa inaumaliza mziki wa dansi kwani hela za kuhonga uwe nazo ili usikike hili nitakuomba uianzishe mada hii kwa mapana na uwazi,Enzi za wakongwe ulowataja kulikua hanuna Rushwa kwenye yombo vya habari kama ilivyo sasa!!Nakuomba tusaidiane maana jamaa watatumaliza kabisa sisi wasanii wa Ukweli!!Muziki wa Dansi tunaupenda na ndio maana tukaichagua kuwa kazi sasa hawa watu wanaomiliki hivi vyombo vya habari na wafanya kazi wao mtazamo wao uko kinyume na maadili kwa kupenda Rushwa ili kazi za wanamuziki zisikike!!
ReplyDelete