

Kutokana na miji kuwa
ndio ilikuwa inaanza, watu wengi kutoka maeneo mbalimbali walihamia mijini na
kujaribu kutafuta wenzao waliotoka sehemu moja na kuwa na vikundi vya
kusaidiana au kuwaunganisha, kwa taratibu hizo watu wa sehemu mbalimbali
walianzisha bendi wakazipa majina ya wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji
Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na
kadhalika.
Iddi Nhende aliyekuwa
ametoka Nzega akaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka Magharibi ya Tanganyika
wakati huo, na kwa kuwa nchi ilikuwa imegawanywa katika majimbo, yakiweko
majimbo kama Northern Province, Southern Highlands Province, Western Province
na kwa vile Nhende alitoka Western province akaanzisha bendi na kuiita Western
Jazz Band 1959. Akanunua vyombo aina ya Grampian toka duka la Souza Junior duka
la vyombo vya muziki lililokuwepo mtaa wa Mkwepu. Aliweza kupata fedha baada ya
kuuza ng’ombe kadhaa wa mamake. Wakati huo katika bendi za aina yake, ilikuwa ni
Dar es Salaam Jazz Band peke yake iliokuwa na gitaa ya umeme, na hivyo Nhende
akawa na kazi ya kutafuta mpigaji kwa ajili ya bendi yake. Ambapo alimfuata
mpiga gitaa la umeme wa kwanza Haus Dibonde (Msukuma), aliyekuwa anapigia Dar
es Salaam Jazz Band iliyokuwa
chini ya Mzee Muba, baada ya hapo akawapata wanamuziki wengine kutoka Ulanga
Jazz Band, wakati huo pia chombo
cha banjo kilikuwa muhimu hivyo akamtafuta mpiga banjo toka Cuban Marimba tawi
la Dar es Salaam. Cuban Marimba wakati huo ilikuwa na tawi Dar Es Salaam tawi lililokuwa
chini ya Mzee Mwaipungu. Mwaka mmoja baadae Nhende alipata transfer ya kikazi
na kwenda Morogoro, hivyo huku nyuma alilazimika kuongeza wasanii ili
kuimarisha bendi wakati hayupo. Akampata David Makwaya mwimbaji, na Ally
Rashid(huyu ameacha muziki karibuni akiwa Msondo) mpiga Saxaphone toka
Zanzibar. Bahati mbaya yule mpiga gitaa Haus akapata kichaa katika mazingira
yaliyohusishwa na ushirikina kutokana na ushindani wa bendi uliokuwepo. Hivyo
basi walifuatwa wanamuziki watatu toka Tabora Jazz, wanamuziki hao walikuwa
wametoka pamoja katika bendi iliyokuwa na makazi Mwanza ikiitwa Kimbo Twist
Band na wakahamia Tabora Jazz, na kutoka hapo wakachukuliwa na Western Jazz,
ukiangalia habari ambayo imeandikwa katika blog hii iliyohusu Dodoma Jazz,
unapata mtiririko wa wanamuziki hawa waliotoka Tabora Jazz, mmoja wao Rashid
Hanzuruni alitua kwa muda Dodoma. Pamoja na Rashid Hanzuruni pia
walisindikizana na Kassim Mponda na Omary Kayanda. Baada ya kazi nzuri sana
aliyoifanya katika anga za muziki, Hanzuruni nae akarukwa na akili katika
mazingira yale ya yule mpiga solo wa kwanza akalazimika kurudishwa Tabora
ambako alikaa mpaka mauti yake. Wema Abdallah akachukua nafasi ya mpiga solo
katika bendi ya Western. Pamoja na kuwa mpigaji mzuri sana wa solo, tatizo la
kinidhamu lilifanya Wema aondolewe Western, na mpigaji mwingine mzuri sana
Shamba Abdallah akachukua nafasi, solo la Shamba linasikika kwenye nyimbo kama
Rosa na Vigerege.
Ukumbi wa nyumbani la Western Jazz ulikuwa
Alexander Hall, ukumbi ambao hatimae ulikuja kuwa ukumbi wa DDC Kariakoo.
Western Jazz walinunua drums zao za kwanza baada ya Kilwa Jazz kununua drums na
kuzipitisha zikiwa juu ya gari lao kwenye ukumbi wa Western Jazz. Western
walijibu mapigo kwa kwenda kununua seti ya drum toka kwa bendi moja ya Wagoa iliyoitwa De Mello Brothers.
Western Jazz Band
walirekodi santuri kadhaa chini ya mkataba waliyousaini na lebo ya Phillips ya
Kenya, na kwa miaka mngi bendi hii ilikuwa maaruf sana Afrika ya Mashariki
nzima. Hatimae Western na mtindo wao wa Saboso walitoweka katika anga za muziki
miaka ya mwisho ya sabini. Kati ya nyimbo zao nyingi ni hizi hapa; Rosa,
Vigelegele, Jela ya Mapenzi, Helena no 1 na 2.

No comments:
Post a Comment