Sunday, August 5, 2012

Mjue Anania Ngoliga



Anania Ngoliga anasema hajui alikojifunza kalimba alijikuta tu analijua. Kazaliwa kakuta baba yake na baba zake wadogo wote wakipiga chombo hicho. Hata dada zake watoto wa baba yake mdogo walikua mabingwa wa kupiga kalimba. Anakumbuka wakati akiwa mdogo yeye na ndugu zake walikuwa wakishindana ni nani bingwa wa kupiga chombo hicho. Pamoja na kuzaliwa akiwa ana ona vizuri, lakini akiwa na umri mdogo wa miaka mitano hivi akaanza kupoteza uwezo wa kuona, hivyo alianza shule katika shule ya Wasioona Buigiri. Mwalimu Abel Mbata aliyekuwa anafundisha hapo Buigiri ndie aliyemshawishi babu yake Anania ili aweze kujiunga na shule hiyo, baba yake akafanya mipango yote na Anania akajiunga na shule. Katika shule ya Buigiri, kulikuweko na magitaa na piano na vyombo vingine vya kisasa, hivyo Anania akajifunza hata kupiga vyombo hivyo. Kufikia darasa la nne tayari alikuwa kiongozi wa Kwaya ya shule yake. Aliendelea na shule mpaka alipomaliza darasa la saba mwaka 1976, alipomaliza shule alirudi kwao Mpwapwa.
John Kitime na Anania Ngoliga
Bela Flek, Anania Ngoliga, John Kitime
Anania Ngoliga
Alipofika Mpwapwa akajiunga na kwaya ya kanisa Kuu la Anglican Mpwapwa, ambapo hata hapo baada ya muda mfupi akawa mwalimu wa kwaya hiyo. Mwaka 1987 akasindikizana na rafiki yake kuja Dar es Salaam kuja kumsalimia dada yake aliyekuwa kaolewa. Alifikia kwa dada yake maeneo ya Msasani, kwa bahati nzuri sana jirani na alipofikia kukawa na jamaa aliyekuwa na gitaa, hivyo akawa analipiga mara kwa mara jambo ambalo likamfanya shemeji yake amuulize kwanini asijiunge na mojawapo ya bendi? Bahati nzuri huyo jamaa mwenye gitaa alikuwa anawafahamu baadhi ya wanamuziki wa bendi iliyojulikana kama Jambo Stars, iliyokuwa mali ya Dr Vulata, ikiwa na makao makuu Komakoma Mwananyamala. Hivyo Anania akaenda kuonana na wanamuziki wa bendi hiyo na kujitambulisha kama muimbaji, mwenyewe anasema alilazimika afiche kuwa anajua gitaa baada ya kusikia wapigaji wa magitaa waliokuweko katika bendi hiyo wakati ule, ambao walikuwa wazuri sana. Jambos aliwakuta Kazembe wa Kazembe, Cobra wa Bilumba ambao kweli walikuwa wapigaji wazuri wa magitaa, pia alimkuta Omari Gendaeka katika bezi na pia mpigaji mwingine Cheo Ali. Kwa hiyo baada ya majaribio akaonekana anafaa, hivyo akawa mmoja wa wanamuziki katika bendi ya Jambos. Aliendelea kupiga katika bendi hiyo mpaka siku moja ambapo mwanamuziki Lovy Longomba alipita kuangalia mazoezi yao, Lovy muda uleule akaamua kumchukua katika bendi yake ya Afriso Ngoma, hivyo basi akamwendea shemeji yake Anania na kumwomba amshawishi  Anania ajiunge na Afriso Ngoma, bendi iliyokuwa mali ya Mwendapole, na Lovy akiwa kiongozi wa bendi.
Kitime, Casey Dreisen, Anania
Anania mwenyewe anasema aliona kama ni ndoto, kwani si muda mrefu alikuwa katoka Mpwapwa na alikuwa hajawahi kupigia bendi yoyote, na kuja kuombwa na mwanamuziki kama Lovy kujiunga na bendi yake ilikuwa kama ndoto. Alienda kuripoti Afriso, bahati mbaya siku alipofika huko ilikuwa ndio siku Lovy anasafiri, kwa hiyo licha ya Lovy kuacha maagizo kwa wanamuziki wenzake kuwa wampokee Anania, na kwa uhakika zaidi wamfanyie interview. Hakuna mtu aliyeshughulika nae, Anania anasema anadhani jamaa walimdharau maana alikuwa bado hata viatu hajanunua alikuwa bado na viatu vya matairi alivyotoka navyo Mpwapwa na pia kwa kuwa alikuwa haoni, hawakumtilia maanani. Lovy aliporudi baada ya wiki mbili akakuta hata interview hajafanyiwa kwa hiyo akamuomba aimbe, nae akaimba vizuri nyimbo za Afriso, na kupata kazi mara moja, wakati waimbaji wa awali wawili Kasavubu na Anderson Supa wakapoteza kazi. Baadhi ya wanamuziki waliouweko wakati huo walikuwa John Maida, Robert Tumaini Mabrish, Mjusi Shemboza, Kasongo Kalembwe, Peter Kazadi wakiwa kwenye vyombo, Ramadhani Kinguti, Tofi Mvambe, Lovy na mwenyewe Anania kwenye uimbaji. Katika bendi hii walirekodi nyimbo nyingi ikiwemo Elly wangu na kusafiri  karibu wilaya zote nchini.
  Kutoka hapo akahamia Legho Stars wakati bendi inaanza kwa mara ya kwanza, waimbaji walikuwa yeye Anania, Shibanda Sonny, Marcelino Vitalis na Lucy Emea, kwenye vyombo Stamili Uvuruge, Chris Chiwaligo, George Mtully na Hemed Mganga. Baada ya Stamili Uvuruge na Shibanda Sonny kuondoka, ndipo akaja Tchimanga Assossa akiwa na na Jemsia Msuya, John Maeda na Shaaban Manyanya na kuanza awamu ya pili ya Legho Stars. Anania hakukaa sana akaiacha bendi hii kwa mara ya kwanza  na kujiunga na kundi la Ram Choc Stars liliyokuwa linaongozwa na Bi. Rukia Mtama, bendi hii iliikuwa na  waimbaji Banza Tax, Salim Shaaban, Adiel Makula, Chris Chiwaligo, Ado Mpoloto, Geofrey Charahani, kwenye rhythm Yahaya Mkango, bendi ilipata mkataba huko Iringa katika Iringa hotel, lakini wanamuziki wakawa hawalipwi kwa hiyo wanamuziki wakaondoka wote kwa pamoja siku ya mwaka mpya 1991….inaendelea

No comments:

Post a Comment