Thursday, July 12, 2012

Orchestra Mambo Bando- Bomoa Tutajenga kesho


Andre Milongo

Kazembe wa Kazembe

William Maselenge

Sadi Mnala
Orchestra Mambo Bado ilikuwa bendi ambayo pamoja na kuwa haikukaa kwa muda mrefu katika anga za muziki, ilikuwa ni bendi ambayo ilikuwa ndogo kulingasha na nyingine zilizokuweko wakati huo lakini iliweza kujiwekea nafasi katika masongamamno wa bendi uliokuweko wakati huo. Bendi hii ilianza mwaka 1981, ikiwa chini ya 'Mtoto Mzuri' Tchimanga Assossa ikajulikana sana kwa ajili na mtindo wake ulioitwa Bomoa Tutajenga kesho. Bendi ilianza mazoezi katika ukumbi uliokuwa ukiitwa Lango la Chuma, Mabibo, ulikuwa ukumbi mpya na bendi ilikuwa mpya, wakati ukumbi ukifanyiwa ukarabati, bendi nayo ilikuwa ikifanya mazoezi makali ili kuweko na uzinduzi wa bendi na ukumbi kwa siku moja. Wanamuziki waliokuweko  mwanzoni walikuwa ni  Sadi Mnala Drums (kwa sasa yuko Msondo), William Maselenge rythm guitar(marehemu), Mzee Andre Milongo(?), Bass na Second Solo, Kazembe wa Kazembe(marehemu) Solo guitar. Pamoja nao walikuweko John Kitime(Njenje),gitaa na kuimba, Jenipher Ndesile (?),muimbaji ambaye sauti yake ilijulikana kutokana na wimbo ‘Bomoa Tutajenga Kesho, George Mzee(Marehemu), muimbaji, Likisi Matola(Moonlight Band)Mpiga Bass na Kinanda,Lucas Faustin(Police Brass Band) muimbaji na Huluka Uvuruge(Msondo) Solo, rhythm na second solo, baadae Athumani Cholilo(Marehemu) muimbaji na Banza Tax(Marehemu)muimbaji, Selemani Nyanga(Uholanzi) drums na bass, Nana Njige(Marehemu) Muimbaji. Bendi ilizunguka miji mingi nchini kama ilivyokuwa kawaida ya bendi miaka hiyo, wakati mwimbaji wa Makassy Masiya Radi kwa kukanyagwa na daladala la Simba Mtoto bendi ilikuwa Mpanda. Wakati Mheshimiwa Sokoine anapata ajali iliyomtoa uhai wake, bendi ilikuwa ikijitayarisha kufanya onyesho Shinyanga. Na bendi ilikuwa Shinyanga wakati amri ya kusimamisha shughuli zote za kupiga muziki kwa mwezi ilipotolewa, jambo lililoleta mateso makubwa kwa wanamuziki hadi walipoweza kurudi Dar es salaam.Mambo bado ilikuwa bendi iliyokuwa ikipiga mtindo wa harakaharaka kufuatia nyao za Lipualipua kutokana na Kiongozi wa Bendi Tchimanga Assossa kuwa na historia ya bendi hiyo. Hili lilifanya bendi iwe tofauti kwani mtindo wa pole pole wa Kamanyola bila jasho  ndio uliokuwa umetawala wakati huo.
Wimbo 'Bomoa Tutajenga Kesho' uliwahi kupigwa marufuku na Umoja wa Vijana wa Mkoa wa Dar es Salaam, jambo ambalo mpaka leo halina maelezo ya kueleweka.

2 comments:

  1. Balozi, hii bendi ilikufaje?

    ReplyDelete
  2. santw mkuu JFK, hizi ni history nadra tunazipata!

    ReplyDelete