Monday, May 14, 2012

Mjue Issa Juma aliyeimba Sina Makosa


Issa Juma Singano alikuwa muimbaji, wengi inakuwa rahisi kumfahamu nikisema  yule muimbaji aliyeimba wimbo wa Sina Makosa. Issa alizaliwa Tanga, alianza muziki akiwa na umri wa miaka 15.Alianza muziki huko kwao Tanga na moja ya vikundi vingi vilivyokuwepo Tanga wakati ule, na akweza kwenda hadi Uganda ambako alikaa mpaka 1970 alipoingia Dar es Salaam na akajiunga na Police Jazz ya Dar es Salaam, miezi sita baadae akahamishiwa Police Jazz ya Tanga. Uwezo wake wa kuimba ukavuka mpaka hadi Kenya na kusikika na producer maarufu A.P. Chandarana, huyu akamuita Issa Juma Kericho. April 1971 Issa akahamia Kericho na kujiunga na Kericho Jazz Band, bendi haikudumu muda mrefu ikasambaratika na Chandarana akamuajiri Issa kama recording assistant kwenye studio yake maarufu ya Chandarana. Issa aliishi sana hapa hata kuanza familia yake hapa. Alijaribu kurekodi nyimbo zake kadhaa lakini hazikupata umaarufu. Mwaka 1977 akaamua kuhamia Nairobi. Alipofika Nairobi akajiunga na Orchestra Kumbakumba ambayo ilikuwa na mchanganyiko wa wanamuziki wa Tanzania na Kenya, mmojawapo akiwa mwanamuziki maarufu muimbaji wa Jamuhuri Jazz band Yusuph Mhando. Mwishoni mwa mwaka 1978 Issa Juma akajiunga na Simba wa Nyika. Kama ilivyohadithia katika makala zilizopita Issa alifika Simba wa Nyika akaikuta katika mgogoro mkubwa ambapo wanamuziki wengi walikuwa wakijiandaa kuanzisha Les Wanyika. Nae akawa mwanamuziki muanzilishi wa Les Wanyika. Na hapa ndipo sauti yake ilikuja kujulikana sana katika ile album iliyokuwa na nyimbo kama Sina Makosa, Pamela, Paulina na kadhalika. Aliacha Les Wanyika June 1981 na kwenda kujiunga na Super Wanyika. Mwaka 1988 alipata ugonjwa wa kupooza na akafariki mwishoni mwa mwaka 1990. MUNGU AMLAZE PEMA PEPONI.

2 comments:

  1. Wakuu,

    Ni jana tu nilipoitia mkononi CD yake ya Issa Jumaa & the Wanyika Stars - World Defeates the Grandfathers na Zanzibara 6. Niliisikiliza kijuu juu kwa sababu nilikuwa nazipitia pia CD za kina Petit Payees, Black Bazaar, Dj Arafat na Nigeria Gold Vol. 3 na DVD ya Africa Dance 9 ambazo nimezipokea jana hiyo hiyo toka kwa supplier wangu halafu nilikuwa na mchecheto wa kutazama mpira Portugal - Czech. Jumamosi na Jumapili niko free kwa hiyo nitaisikiliza CD ya Issa Juma and the Wanyika Stars kwa umakini zaidi.

    Kitu kimoja Mama Mtoto aliniambia wakati CD ya Issa Juma ikiwa inapiga "..Baba, almost all the songs sound the same.. It is like you are in Chinese restaurant you don't what music ended and which one has started!.."

    Mdau, Sokomoko Damu, Helsinki, Finland.

    ReplyDelete