Sunday, April 15, 2012

Abbu Omar Profesa Omar Junior


Ganda la album ya 3 ya Abbu Omar
Abbu Omar Njenga, mwanamuziki ambaye ndiye ambaye amenipa historia nzima hii ya Simba wa Nyika, alijiunga rasmi na Simba wa Nyika 1981, mwaka ambao aliingia Nairobi kupitia Mombasa akitokea UDA Jazz. Nia yake ya awali ya kwenda Kenya ilikuwa ni kutafuta elimu zaidi baada ya kuwa amemaliza Songea Boys high School, aliona kwenda Kenya angeweza kupata chuo ambacho kingeweza kumpa elimu ambayo ingemnyooshea maisha. Bahati mbaya alikuta ada zilikuwa juu kuliko uwezo wake, hivyo akalazimika kutafuta kibarua ili aweze kuishi. Kazi ambayo ilikuwa rahisi zaidi kupata ni kazi ya muziki kwani alikuwa na kipaji cha kupiga muziki na alikuwa mwanamuziki wa UDA Jazz 'Wana Bayankata'. Alimwendea mwanamuziki Charles Ray Kasembe wa Les Volcano ili ajiunge na bendi hiyo. Huyu Charles Kasembe ndiye aliyekuwa mpiga rhythm gitaa wa Mbaraka Mwinyshehe wa muda mrefu(nyimbo kama Wajomba Wamechacha) aliacha Super Volcano kabla ya kifo cha Mbaraka na Mbaraka akampata mpiga rhythm mwingine aliyeitwa Stanley Mtambo aliyedumu mpaka kifo cha Mbaraka.
Kutokana na kuwa mpiga gitaa maarufu wa Super Volcano Charles Kasembe aliona ni heri kuanzisha bendi  aliyoiita Les Volcano.  Abbu hakupata nafasi Les Volcano maana ilikuwa imeshajaa wanamuziki. Kasembe alimshauri Abbu awaone Wilson na George Peter ambao wakati huo walikuwa katika jitihada za kufufua tena Simba wa Nyika. Charles mwenyewe alimpeleka Abbu mpaka Bombax Club  iliyoko Ngong Road, ambapo ndipo Simba wa Nyika walikuwa wanajiandaa kupiga. Abbu alipandishwa jukwaani siku hiyohiyo na kukabidhiwa gitaa la rhythm, upigaji wake ukampa kazi siku hiyo hiyo.  Kwa hiyo pia Abbu akashiriki katika album ya kwanza ya awamu hiyo ambapo album hiyo ilikuwa na nyimbo kama Barua ya Mapenzi, Mama Nirudie,  na palikuweko album nyingine na ikafuata album ya tatu iliyokuwa na ule wimbo maarufu wa Shilingi  Yaua, Abbu alikaa Simba wa Nyika mpaka 1987 ambapo aliacha bendi, lakini aliendelea kuwa na uhusiano na bendi hiyo na kuendelea kushiriki katika recording mbalimbali za bendi hiyo  hadi ya mwisho 1992 kabla ya kifo cha George Peter. Abbu Omar ambaye kwa upigaji wake wa rhythm ulimfanya arith heshima ya Professsor Jnr ikikumbukwa kuwa Professor Omar mkubwa alikuwa ndiye yule aliyeanzisha Les Wanyika. Kwa sasa Abbu Omar yuko Japan ambako ana piga muziki mara nyingine kwa kushirikiana na Fresh Jumbe na Lister Elia

7 comments:

  1. Wakongwe wa mziki hawa,tunashukuru sana kwa kutupa kumbukumbu hizi adimu

    ReplyDelete
  2. wanamuziki wa zamani walau tunapata historia zao nzuri pamoja na kwamba mimi si kizazi cga muziki huo lakini napenda kuusikiliza kutokana na historia na mameno yake mazuri. sasa, sijui hawa dot.com tutasimilia nini wajukuu zetu? HEBU WANAMUZIKI WA SASA MMBADILIKE.

    ReplyDelete
  3. wanamuziki wa zamani walau tunapata historia zao nzuri pamoja na kwamba mimi si kizazi cga muziki huo lakini napenda kuusikiliza kutokana na historia na mameno yake mazuri. sasa, sijui hawa dot.com tutasimilia nini wajukuu zetu? HEBU WANAMUZIKI WA SASA MMBADILIKE.

    ReplyDelete
  4. JFK naomba nikuulize kwenye wimbo wa christina JKT kimulimuli umeshiriki kuimba? nahisi kama nasikia sauti yako humu?

    ReplyDelete
  5. J.K,ASANTE KWA HISTORIA HII NZURI NA YA KUELEWEKA,NAONA HAPA KUNA WAKONGWE MAARUFU WAMESHIRIKI KATIKA ALBAM HII,KM.FRESH JUMBE,TWAHIRI MOHAMED,ABDALLAH GAMA,RAMA ATHMANI NA GEORGE KESSY,NAKUMBUKA HUYU GEORGE KESSY NDIYO ALIKUWA MMOJA KATI YA WAANZILISHI WA MLIMANI PARK ORCH WAKATI IKIWA CHINI YA TTCC,KABLA YA KUCHUKULIWA NA DDC.

    ReplyDelete
  6. Wakuu,

    Nadhani hakuna nyimbo ambayo kinanda cha George Kessy akiwa Mlimani Park kinaposikika zaidi kama katika ile nyimbo ya Barua Toka kwa Mama!

    Mdau Sokomoko Damu, Helsinki, Finland.

    ReplyDelete