Mwishoni mwa mwaka 1981 ndipo Issa juma alipoamua kujitoa Les Wanyika. Sauti yake ilikwishakuwa maarufu kutokana na nyimbo alizoimba akiwa bendi hiyo. Maproducer kutoka kampuni mbalimbali za kurekodi mjini Nairobi waliposikia hilo wakaanza kumfuata ili arekodi katika studio zao. Kampuni iliyoweza kumpata ilikuwa na kampuni ya Meghs iliyokuwa mali ya mhindi mmoja aliyejulikana kwa jina la Babuu. Katika kampuni hiyo alirekodi nyimbo kadhaa zilizokuja pata umaarufu. Kimsingi inaoneka mwanzoni Issa hakuwa na wazo la kuanzisha bendi, mpaka alipolazimika kutafuta jina la bendi ya kuzibeba nyimbo hizo alizorekodi, ndipo kwa mara ya kwanza jina la Super Wanyika lilipozaliwa. Nyimbo zilizotolewa kwa jina la bendi hii zilikuwa kama Anita, Unataka nikupendeje, Jennifer na kadhalika. Wanamuziki walioshiriki katika kazi hizi za mwanzo walikuwa Mohamed Tika, Shoushou Batenga, na Michael Beche waimbaji, huyu Mzee Shoushou alikuwa Mkongo ambaye aliwahi kupitia bendi ya safari Trippers. Mzee Maneno Shaaban alipiga drums, Issa Khalfani Bendera, kwenye solo, Stanley Mtambo gitaa la rhythm, George Madrago gitaa la bezi, Said Makelele na Mambi Iddi wakiwa kwenye trumpet. Nyimbo zilipotoka zilianza kuvuma na kulazimisha bendi ianze kufanya maonyesho. Wanamuziki wakakubaliana na Babuu ambae pamoja na kuwa na studio pia alikuwa na vyombo vya muziki, hivyo akawakodisha vyombo hivyo kwa mkataba maalumu. Super Wanyika ilidumu kwa zaidi ya muda wa miaka mitatu. Baadhi ya wanamuziki waliokuwemo katika kundi hilo ni Mzee Mohamed Tungwa akipiga solo, Abdalah Kimeza kwenye Saxaphone, Jumanne Kilongola kwenye trumpet, Joseph Tito akipiga gitaa la rhythm, Shwaib Ole monduli muimbaji, na wengineo. Lakini bendi hatimae ilikuja kufa kwa makosa yaleyale ya uongozi mbovu. Issa Juma akaanza kusahau kuwapa wanamuziki wenzie haki stahili.
Sauti yake iliendelea kuwa muhimu katika anga la muziki, hivyo akaanza kuingia mikataba tofauti na ule aliyokuwa nao Meghs. Akaingia mkataba na kampuni ya AIT, halafu akaingia mkataba na producer mashuhuri Nairobi wakati huo Bwana Joe Mwangi wa Matunda Production. Sasa kazi ambazo zilifanywa katika mikataba hiyo mipya alitambulisha kuwa zimerekodiwa na bendi aliyoitambulisha kama Wanyika Stars, baadhi ya nyimbo ambazo zilirekodiwa kwa jina hilo ni kama Sigalame,Mpita njia,Bomanga, Mony na kadhalika. Kutokana na wanamuziki hawa walioshiriki kazi hizi, baadhi wakaunda kundi la Sigalame System ambalo halikudumu sana, wengine wakaunda kundi la Orchestra Vinavina, pamoja na kuwa na muziki mzuri hawa Vinavina hawakuwa na bahati ya kupendwa hivyo wakaondoka Nairobi na kuhamia Morogoro Tanzania, wengi wa wanamuziki wa bendi hii asili yao ilikuwa Morogoro,baadae bendi hii ilikuja kuitwa Les Cubano. Les Cubano ilikuwa na wanamuziki kama Michael Beche, Niko Zengekala, Shwaib Ole Monduli, Banza Tax wakiwa ni waimbaji, Mohamed Tungwa na Issa Bendera wapiga solo,Fred Mwalasha rhythm gitaa, George Madrago gitaa la bezi, Mzee Maneno Shaaban akipiga drums, Said Makelele, Mambi Idd, Jumanne Kilongola wapiga trumpet, Kibwana Magati alikuwa anapiga drum na bezi, Abdalaah kimeza na Comson Mkamwa walikuwa wapuliza sax.......itaendeleaaa
No comments:
Post a Comment