Monday, September 26, 2011

Maisha ya Frank Humplick

Franz Yosef Humplick ndilo jina alilopewa Frank Humplick baada ya kuzaliwa katika shamba la baba yake, ambaye alikuwa mhandisi wa Kiswisi ambaye alishiriki katika ujenzi wa reli ya Tanga hadi Arusha. Tarehe 3 April 1927 ndo siku Frank alipozaliwa. Mama yake alikuwa Mchaga. Frank pia alizaliwa na dada zake wawili Thecla clara na Maria Regina ambao hatimae alifanya nao kazi nyingi za muziki wao wakiwa waimbaji, yeye akitunga, akiimba na kupiga gitaa.
Frank alianza rasmi kazi ya muziki kwa kurekodi  1950. Akiwa Katika bustani iliyokuweko katika ghorofa la KNCU, alirekodi nyimbo ambazo zilirekodiwa na kampuni ya Galatone kutoka Afrika ya Kusini.
Peter Colmore  ambaye aliweza kugundua vipaji vya wanamuziki wengi kama Edward Masengo, Mathias Mulamba, Esther John  kupitia Kampuni yake ya High Fidelity Productions, alianza kazi ya kupromote kazi za Frank na dada zake. Akitumia label yake ya His Masters Voice Blue Label aliweza kuanza kusambaza kazi za  ndugu hawa na kwa miaka kumi sauti ya Frank Humplick na dada zake ilitawala anga za Afrika ya Mashariki. Wimbo wa Harusi ambao ulirekodiwa katika miaka ya 50, uliitwa wimbo wa Taifa wa Harusi wa Afrika ya Mahsariki, wimbo huu ulikuja kurudiwa tena na bendi ya Afro70, chini ya Patrick Balisidya na pia The Mushrooms wakaurekodi tena na kuupa umaarufu mpya na hata wao kujipatia umaarufu japo haukumpa chochote Frank wala ndugu zake.
Frank na dada zake waliimba nyimbo kadhaa za Kichaga, kuna habari inasema Chief Thomas Marealle alimwomba Frank atunge nyimbo za Kichaga kwani wakati huo akina George Sibanda toka Rhodesia ya Kusini(Zimbabwe), Manhattan Brothers(Afrika ya Kusini) waliimba kwa lugha zao za Kishona na Kizulu. Frank alitimiza kazi hiyo kwa kutunga nyimbo kama Wasoro na Kiwaro.
Kati ya nyimbo ambazo zinastahili ziwekwe katika kumbukumbu ya Taifa hili ni wimbo Yes No. Wimbo huu uliotugwa wakati wa mapambano ya kutafuta Uhuru, ilikuwa na mafumbo mengi na  ulitumika kabla ya kila mkutano wa TANU na kutumiwa sana na wanasiasa wa wakati huo kiasi cha Gavana Sir Edward Twining alitoa amri usipigwe tena Sauti ya Dar es Salaam na msako wa nyumba kwa nyumba ulifanyika kutafuta nakala za wimbo. Frank Humplick anasatahili akumbukwe zaidi na Taifa la Tanzania.

No comments:

Post a Comment