Friday, August 19, 2011

Ahmed Mohamed Kipande wa Kilwa Jazz Band

Kilwa Jazz Band

   
Ahmad Kipande

Ahmed Mohamed Kipande ni kati ya wanamuziki ambao wameacha jina kubwa kutokana na mchango wake katika maendeleo ya muziki wa Tanzania.
Kipande alizaliwa Kilwa Kivinje  mwaka 1937, alianza shule 1946 huko huko Kilwa Kivinje na baada ya darasa la nne akahamia Dar es Salaam ambako aliendelea shule ambayo baadae iliitwa Uhuru Boys mpaka alipomaliza darasa la nane.
Alipoanza kazi alianzisha kundi la muziki lililokuwa likitumia vyombo vya asili , baadae akaanzisha bendi rasmi ya muziki aliyoiita Home Boys. Ujuzi wa muziki wa Kipande ulianza kujulikana rasmi 1955 wakati alipoweza kushika nafasi ya pili katika mashindano ya kupiga gitaa yaliyofanyika mtaa wa Kichwele, mbele ya viongozi wa Kikoloni. Kipande alipata zawadi ya shilingi 15 kwa kuwa wa pili. Mwaka 1958 aliachana na bendi ya Home Boys na kuanzisha Kilwa jazz Band akiwa na wanamuziki watano tu. Kipande alikuwa hodari kwa gitaa la solo na hata kumudu vizuri gitaa la Hawaian na pia alikuwa mpuliza saksafoni mahili sana. Alikaa miaka mingi Kilwa na kupiga nyimbo ambazo hadi leo bado watu wanazipenda. Napenda nipate lau nafasi, Nachekacheka Kilwa leo, Play your Part na nyingi nyingine, kutokuelewana fulani kukamfanya ahame na kuanzisha African Quellado, bendi nzuri ambayo haikudumu muda mrefu, alijaribu kufufua tena Kilwa Jazz iliyokuwa imekufa lakini haikudumu muda mrefu.Hakurudi tena kwenye muziki mpaka mauti yalipomkuta. Shahiri zuri sana lilitungwa na mtunzi Saidi M Nyoka(Udogo si hoja) katika kumuelezea Ahmad Kipande.

Amezikwa Jumanne,jeneza tukalibeba,
Aprili mbili nne, mwaka themanini na saba,
Ikabidi tujazane, kinamama kinababa,
Kwa Maguruwe sa nane,tutele kwenye msiba,
Machozi tele matone, simanzi imetukaba,
Kiasi tusijuane, uzishini kwa nasaba,
Kalale pema panene, Kipande kwaheri baba

Alikuwa maarufu, Kipande na bendi yake
Nchi hii kaisifu,katika utunzi wake,
Leo tena katawafu,Yarabi pema muweke,
Muweke paangalifu, kila jaza imfike,
Anukishie harufu, njema kaburini pake,
Umsamehe machafu,Yarabi kando uyaweke,
Yaweke mema matufu, Kipande afaridhike,
Faraja ya ukunjufu, Roho yake ifufuke,
Mjaze mema Latifu, humo kaburini mwake.

Alikuwa mwimbaji, mzuri wan chi hi,
Kadhalika mtungaji, hodari wa wasanii,
Kisha mpulizji, wa zumari kwa bidii,
Bidii ya mwanambuji, sasa hatumsikii,
Bwana Mungu mfariji,Pepo njema ya utu,
Aishi katika mji,wa amani na jamii,
Jamii ya watendaji, mazuri ya utwalii,
Nasi nyuma wafataji, njia ndo hii hii,
Kimezimika kipaji, kupotea jii jii

Alikuwa kiongozi, wa bendi mwenye akili,
Kaongoza Kilwa jazi,kwa nyimbo za maadili,
Kwa amri ya Mwenyezi, kaufisha wake mwili,
Mwili wake hatuwezi, kuuona kwa dalili,
Mawazo yake azizi, hayafutiki kwa kweli,
Molla umpe makazi,mazuri penye kivuli,
Kivuli chenye mbawazi,kisichopenya miali,
Mwondoshee mabazazi,na adui wakatili,
Afate maelekezi , ua wewe Bwana Jalali.

Kipande alifariki 23 April 1987 nyumbani kwake Tandika Maguruwe na kuzikwa hukohuko, baada ya kuugua kwa muda wa miaka 10 akiwa amepooza upande wa kulia wa mwili wake.

No comments:

Post a Comment