Thursday, May 5, 2011

ALLY MAKUNGURU


Nimesikiliza sana leo wimbo Mjomba wa Orchestra Safari Sound -Ndekule. Gitaa la rhythm katika wimbo huo lilipigwa na Ally makunguru, nikamkumbuka sana marehemu rafiki yangu huyu.Tulikutana na Ally makunguru kwa mara ya kwanza 1975. Wakati huo nikiwa mwalimu lakini nikiwa Iringa na kibendi chetu kidogo kilichojulikana kwa jina la Chikwalachikwala, huyu bwana alikuja kwangu na kunambia  anataka kujiunga na bendi yetu. Nilipomuuliza kama amewahi kupigia bendi nyingine akanambia ametoka Masasi ambako alikuwa anapigia  Kochoko Jazz band, sijaweza kumkuta mtu aliyewahi kuisikia bendi hiyo mpaka leo.
Makunguru alilipenda sana gitaa, nilikuwa nikimuacha nyumbani asubuhi akifanya mazoezi ya gitaa ninapokwenda darasani, na kumkuta  anaendelea na mazoezi ninaporudi kutoka kazini. Alikuwa hali mchana anafanya mazoezi tu. Na akawa mpigaji wetu muhimu katika rhythm maana aliweza kupiga rhythm zilizokuwa zinatamba wakati huo, kama ya wimbo, Cheza kimbunga ya JKT, Tambola na mokili wa Johnny Bokelo na nyimbo kadhaa za Lipua lipua na Orchestra Kiam. Siku bendi ya JKY Kimbunga ilipokuja Iringa tukaona fahari kumtambulisha mpigaji anaeweza kupiga nyimbo zao, hilo lilikuwa kosa, maana JKT waliondoka nae mara moja na kwenda nae Dar es Salaam na kuanza kuishi maisha ya muziki ya Dar. Alofanya kazi nzuri sana na hivyo kuweza kuwa na uwezo wa kuhama bendi atakapo. Makunguru aliweza kupigia Tanzania Stars, Mlimani Park, OSS Ndekule, MK Group na hatimae kuhamia Kenya ambako alishiriki kupiga wimbo ule maarufu Nchi ya kitu kidogo, na huonekana katika video clip ya wimbo huo

No comments:

Post a Comment