Mzee Iddi Nhende ndiye aliyepata wazo la kuanzisha bendi
maarufu ya Western Jazz. Iddi Nhende alianza muziki akiwa bado mdogo katika
bendi ya shule alipokuwa Primary huko Nzega, mwaka 1944 alijiunga na Tabora
Boys Secondary na hapa akajiunga na Brass Band ya shule ambapo alikuwa mpigaji
wa Cornet. Alimaliza shule na kuja Dar es Salaam kujiunga na Chuo cha Afya,
Sewa Haji Medical Training Center. Baada ya kumaliza mafunzo akaajiriwa Bohari
ya madawa na kisha mwaka 1957 alihamishiwa Muhimbili. Upenzi wake wa muziki
ulimfanya mwaka huohuo ajiunge na Rufiji Jazz Band kama mpiga trumpet, bendi
hii wakati huo ilikuwa ikifanya maonyesho yake Minazini Community Centre
iliyokuwa eneo linaloitwa siku hizi Mchikichini na pia walikuwa wakipiga muziki
katika ukumbi wa Arnatougro.
Kutokana na miji kuwa ndio ilikuwa inaanza, watu wengi
kutoka maeneo mbalimbali walihamia mijini na kujaribu kutafuta wenzao waliotoka
sehemu moja na kuwa na vikundi vya kusaidiana au kuwaunganisha, watu wa sehemu
mbalimbali walianzisha bendi wakazipa majina ya wanakotoka, hivyo waanzilishi
wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga
jazz na kadhalika. Hivyo Iddi Nhende aliyekuwa ametoka Nzega akaamua kuanzisha
bendi ya watu kutoka Magharibi, kwa kuwa nchi ilikuwa imegawanywa katika
majimbo, yakiweko majimbo kama Northern Province, Southern Highlands Province,
Western Province na kwa vile Nhende alitoka Western province akaanzisha Western
Jazz Band 1959. Akanunua vyombo aina ya Grampian toka duka la Souza Junior duka
la vyombo vya muziki lililokuwepo mtaa wa Mkwepu. Aliweza kupata fedha baada ya
kuuza ng’ombe kadhaa wa mamake. Wakati huo katika bendi za aina yake ni Dar es
Salaam Jazz Band peke yake waliokuwa na magitaa ya umeme, hivyo Nhende akawa na
kazi ya kuwatafuta wapigaji ambapo alimfuata mpiga gitaa la umeme wa kwanza
Haus Dibonde(Msukuma), aliyekuwa anapigia Dar es Salaam Jazz Band(hii ilikuwa
chini ya Mzee Muba), baada ya hapo akawapata wanamuziki wengine kutoka Ulanga
Jazz Band, wakati huo chombo cha banjo kilikuwa muhimu hivyo akamtafuta mpiga
banjo toka Cuban Marimba tawi la Dar es Salaam. Cuban Marimba wakati huo
ilikuwa na tawi Dar Es Salaam lililokuwa chini ya Mzee Mwaipungu. Mwaka mmoja
baadae alipata transfer ya kwenda Morogoro, hivyo huku nyuma alilazimika kuongeza
wasanii ili kuimarisha bendi wakati hayupo. Akampata David Makwaya mwimbaji, na
Ally Rashid(huyu ameacha muziki karibuni akiwa Msondo), mpiga Saxaphone toka
Zanzibar. Bahati mbaya yule mpiga gitaa Haus akapata kichaa katika mazingira
yaliyohusishwa na ushirikina kutokana na ushindani wa bendi uliokuwepo. Hivyo
basi walifuatwa wanamuziki watatu toka Tabora Jazz, wanamuziki hao walikuwa
wametoka pamoja katika bendi iliyokuwa na makazi Mwanza ikiitwa Kimbo Twist
Band na wakahamia Tabora Jazz, na kutoka hapo wakachukuliwa na Western Jazz.
Wanamuziki hao walikuwa
Rashid Hanzuruni, Kassim Mponda na Omary Kayanda. Baada ya
kazi nzuri sana, Hanzuruni Nae akarukwa na akili katika mazingira yale ya yule
mpiga solo wa kwanza akalazimika kurudishwa Tabora ambako alikaa mpaka mauti
yake. Wema Abdallah akachukua nafasi ya mpiga solo katika bendi ya Western.
Tatizo la kinidhamu lilifanya Wema aondolewe Western, na mpigaji mwingine mzuri
sana Shamba Abbdallah akachukua nafasi, solo la huyu bwana linasikika kwenye
nyimbo ka Rosa na kadhalika.
Hall la nyumbani la Western Jazz lilikuwa Alexander Hall,
ambalo lilikuja kuwa hall la DDC Kariakoo. Western walinunua drums baada ya
Kilwa Jazz kununua drums na kuzipitisha kwao kuwaringia. Walinunua toka kwa
bendi moja ya Wagoa iliyoitwa De Mello Brothers. Western walirekodi santuri
kadhaa chini ya mkataba waliyousaini na lebo ya Phillips ya Kenya. Hatimae
Western na mtindo wao wa Saboso walitoweka katika anga za muziki miaka ya
mwisho ya sabini. Kati ya nyimbo zao nyingi ni hizi hapa; Rosa, Vigelegele,
Jela ya Mapenzi, Helena no 1 na 2.
No comments:
Post a Comment