Saturday, October 2, 2010

UPINZANI......

Leo hii kuna neno maarufu limetokana kwa wasanii wa Kimarikani-BIF. Si kwamba ni utamaduni mgeni, ila utekelezaji wake ndo umekuwa tofauti siku hizi, na kwetu hapa kumekuweko na utamaduni wa ushindani ambao kwa kuchochewa mara nyingine na vyombo vya habari ukageuka upinzani. Katika kipindi fulani cha miaka ya sitini muziki wa jiji la Dar katika nyanja ya Band za rumba ulitawaliwa na bendi mbili, Dar es Salaam Jazz- Majini wa Bahari na mtindo wao wa Mundo, na upande wa pili Kilwa Jazz. Ulikuwa mpambano mkali uliofikia hata wapenzi wa bendi hizi mbili kutandikana makonde. Bendi zilitungiana nyimbo za mafumbo moja maarufu ulikuwa ule wimbo wa Dar Es Salaam Jazz Mali ya mwenzio siyo mali yako, ukiwadhihaki kilwa Jazz kutokana na eneo la Klabu yao kuwa na utata wa kodi. Morogoro kulikuwa na miamba wawili, Morogoro Jazz na Cuban Marimba, ushindani wao uliweza kuwasha moto wa upenzi Afrika ya Mashariki nzima, watu walikuwa wanajitahidi kuwepo Morogoro siku za wikiendi, Morogoro Jazz wakiwa na mtindo wao waSululu, Cuban Marimba na mtindo wa Ambianse. Nao pia walitunga nyimbo zenye vijembe nyingi zilizowatia kiwewe wapenzi wao, Cuban walikuja na mtindo wao Subisubi, wakijisifu kuwa wao ni Jini Subiani linanyonya. Tanga kulikuwepo na vijana wa Barabara ya 4 Atomic Jazz wana Kiweke , wakipambana na Jamhuri Jazz Band na mitindo yao mingi kama vile Dondola na Toyota. Ushindani huu uliendelea katika bendi mbalimbali, kama vile Juwata na Sikinde. Kuna ushindani mwingine ulikuwa zaidi wa kufikirika kama ilivyokuwa inadhaniwa na wengi kati ya Vijana Jazz na Washirika Stars, kiasi cha kwamba kuna wakati ule wimbo wa Nimekusamehe lakini sintokusahau ulitafsiriwa kuwa ulikuwa umetungwa na Hamza Kalala kwa ajili ya kumtaarifu Hemed Maneti, japokuwa si Maneti wala Hamza ambae niliongea nae kuhusu wimbo huo karibuni aliyesema kuwa aliutunga kwa ajili hiyo. Kwa wapenzi wa muziki enzi za uhai wa Maquis Du Zaire, na Orchestra Safari Sound wanakumbuka ushindani mkubwa ulio kuwepo kati ya hizi bendi mbili ambazo kuna wakati huo zote zilikuwa zikiwa na makao makuu jirani, Maquis wakiwa Ubungo na OSS Kimara. Maquis walipoasisi mtindo wao wa Ogelea piga mbizi, OSS wakaja na Chunusi, wakiwa na maana ukiogelea kiboko yako Chunusi. Katika mtiririko wote huu wa ushindani mara chache sana ulifikia wanamuziki binafsi wakashikana mashati kwa sababu za ushindani. Na ushindani ulikuwa wa maana kwa kuwa kweli bendi zilipiga muziki tofauti, Jamhuri na Atomic zote za Tanga lakini kila moja ilikuwa na muziki tofauti, na vivyo hivyo Moro Jazz na Cubano, au Tabora Jazz na Nyanyembe Jazz. Kila Jumanne asubuhi, Radio Tanzania ilikuwa na kipindi kilichorusha nyimbo zilizorekodiwa katika studio yake,Misakato. Ilikuwa si ajabu kukuta wanamuziki wa bendi yenye ushindani ukisikiliza nyimbo mpya za washindani wao. Na hata kutoa sifa pale ambapo zinastahili, na kutokea hapo watu wanajipanga kutengeza kazi bora kuliko hiyo. Nakumbuka Tancut Almasi ilikuwa Morogoro wakati Vijana Jazz wakirushwa nyimbo zao za Ngapulila, Adza kwa mara ya kwanza katika kipindi cha misakato, ilikuwa uhimu kusikiliza kazi yao kwani wakati huo Shaaban Wanted ndio alikuwa kahama Tancut na kujiunga na Vijana, na mfumo wa vyombo wa Vijana ulikuwa sawa na Tancut na Washirika pia yaani Solo gitaa, Rythm Gitaa, Second solo, Keyboards, bass, na vyombo vya upulizaji. Hii haikuleta upinzani bali iliongeza ushindani, hapo tulikaa chini na hata kurekibisha baadhi ya nyimbo tulizoziona ziko chini ya kiwango cha vijana, matokeo yake ndio ile album, yenye nyimbo kama Helena Mtoto wa Arusha, Masikitiko na kadhalika

No comments:

Post a Comment