Saturday, October 2, 2010

Kuzaliwa kwa Bana OK

Baada ya kifo cha Franco, Lutumba Simaro ndie alie liongoza kundi zima la TPOK Jazz kwa miaka minne. Ilionekana kuwa ili warithi wa Franco waendelee kufaidi matunda ya kundi hilo, wazo lilitolewa kuwa Simaro abakie na wanamuziki wote na familia iendeshe utawala mwingine wote, na warithi wawe wanapata asilimia 40 ya mapato yote, ambapo dada yake Franco ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa familia angeyasimamia shughuli hizo. Dada wa Franco, baada ya kushauriana na nduguze aliamua kuwa familia ipewe asilimia 30,na isijihusishe kabisa na mambo ya bendi. Baada ya makubaliano haya bendi ilianza kazi na safari yake ya nje ya kwanza ilikuwa Tanzania na Kenya. Hali ilikuwa ngumu baada ya kifo cha Franco, lakini mambo polepole yalianza kuwa mazuri. Ghafla magazeti yakaanza kuwa na barua za wasomaji zikimlaani Simaro kuwa anaendesha bendi kama mali yake peke yake na kutokutoa msaada wa maana kwa watoto wa Franco. Hatimae akaandikiwa barua rasmi kuwa arudishe vyombo vyote vya muziki nyumbani kwa Franco.Hiyo ilikuwa mwishoni mwa mwaka 1993. Wakati huo huo mwanasheria wa familia ya Luambo alienda kwenye TV na kutangaza kuwa Simaro si kiongozi tena wa bendi.
Ilikuwa ni pigo kwa Simaro ambaye alijiunga na OK Jazz tangu 1961, na kupitia kwake wanamuziki kama Femi Joss, Kwammy, Isaac Musekiwa, Defao, Albino Colombo waliweza kuwika katika OK Jazz, na wote walikuwa wameondoka akabaki mwenyewe na sasa alikuwa akifukuzwa kupitia TV.
Katika onyesho lake la mwisho aliwaomba watu wa TV ya RTNC kuhudhuria,na kwa kutumia nafasi hiyo nae akatangaza kuwa yeye si mwanamuziki wa TP OK Jazz tena, ilikuwa ni tangazo la kusikitisha lililoleta simanzi kwa wengi. Na ndio ukawa mwanzo wa Bana OK, wanamuziki walikutana walikutana katika ukumbi wa Bar ya Zenith na kuamua kuanzisha bendi chini ya Rais wa Lutumba Simaro. Ilikuwa tarehe 4 January 1994. (Habari na picha kutoka www.afropop.org kwa ruksa ya Banning Eyre)

No comments:

Post a Comment