Showing posts with label biography. Show all posts
Showing posts with label biography. Show all posts

Friday, August 19, 2022

IJUE HISTORIA FUPI YA DEKULA KAHANGA VUMBI


Dekula Kahanga Vumbi
 Kwa wapenzi wa muziki wa dansi Tanzania, jina la mpiga gitaa Dekula Kahanga Vumbi si geni, wengi hasa humfahamu kama mwanamuziki wa Maquis Original, na wanakumbuka mlio wa gitaa lake katika wimbo wa Ngalula, hasa pale ambapo Assossa anamhamasisha aongeze utamu kwa kutaja jina' Vumbi Vumbi'.
Lakini Je, mkali huyu alianzia wapi?
Kwanza kabisa  baba yake hakupenda kabisa apige gitaa,  lakini bahati nzuri alikulia kwa bibi yake katika mji wa Uvira, mkoa wa Kivu, Jamhuri ya Kongo. Kwa bibi kama walivyo wabibi wengi, alikuwa na uhuru zaidi na akaanza kwa kutengeneza magitaa yake, ambayo yalikuwa yakivunjwa kila baba yake alipokuwa akija kuwatembelea.

Jirani na alipokuwa akiishi kulikuweko na bar inaitwa Sikiya sosi ambapo palikuweko  na bendi ikiitwa Gramick Jazz, bendi iliyopitiwa na wanamuziki wengi ambao baadae walikuja Tanzania akiwemo Dr Remmy ngala. Vumbi alikuwa akisikiliza muziki ukipigwa ndani ya  hiyo bar na yeye akawa anafuatisha kwenye gitaa la kutengeza mwenyewe la nyuzi tatu, hatimae bibi yake akamnunulia gitaa dogo la nyuzi nne ambalo alikuwa anaenda nalo mpaka shule, ambapo mwalimu wake siku nyingine alikuwa akimwita awatumbuize wanafunzi wenzie.
Siku moja alikutana na jamaa aliyekuwa akipiga katika bendi iliyokuwa ikimilikiwa na mapadri, Dekula akawa anamnunulia sigara huyu jamaa nae akaanza kumfundisha chords mbalimbali za kupiga gitaa. Wanamuziki wengi wa zamani walipitia hatua hii ya kuwanunulia wakongwe sigara ili wafundishwe kupiga chombo. Mwanafunzi Dekula  aliendelea vizuri hatimae akajiunga na bendi hiyo ya mapadri iliyoitwa Kyalalo Band akiwa mpiga rhythm. Wanamuziki wa Kyalalo hawakuruhusiwa kujiunga na bendi zilizo kuwa zinapiga muziki kwenye bar, wala bendi yenyewe  haikuruhusiwa kwenda kupiga kwenye bar, kulikuweko na ukumbi mkubwa wa kanisa na hapo ndipo walipofanya mazoezi na maonyesho.  Hatimae Dekula aliiacha bendi hiyo ya mapadri na kujiunga na bendi Bavy National tena kama mpiga gitaa la rhythm.

 

Bavy National  Orchestre, kutoka kulia mstari wa nyuma ni Dekula (Rythm),Packot(Solo na Kiongozi),Maboko(Besi),
Merry-Djo (Drums).
Kutoka kulia mstari wa mbele,Waimbaji ni Djo-Mali,Issa Nundu na Simplice Mofeza.
Mwaka wa 1983  katika "Sikia Sosi Bar" Mjini  Uvira Mkoani Kivu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Alipoingia Bavy National akakutana na mwimbaji Issa Nundu ambae alikuwa anafanya kazi hospitali, lakini jioni anajiunga na bendi, baada ya muda Kyanga Songa ambaye alikuwa Bwana Shamba nae alijiunga nao. Kyanga Songa  na Kasaloo Kyanga walipokuwa TANCUT Almasi Orchestra  Iringa, walinunua baiskeli na wakawa wanajiita Mabwana Shamba na baiskeli zao.
Katika kipindi hicho wakazi wa Kongo ya Mashariki, ambako kunazungumzwa Kiswahili, walikuwa wakisikiliza na kuzijua bendi nyingi kutoka Afrika ya Mashariki, bendi kama Tabora Jazz, Mangelepa, Simba wa Nyika, Mlimani Park zilisikilizwa sana maeneo hayo, na nyimbo kama Kassim ilikuwa moja ya nyimbo maarufu wakati huo na hivyo ikawa ndoto ya Vumbi na wenzie kuwa lazima siku moja waende huko unakotoka muziki mtamu huo ili nao waweze kushiriki. Katika kipindi hicho Kyanga Songa na Issa Nundu waliondoka  kwenye bendi yao ya Bavi National na kuelekea Tanzania, bendi ikatetereka sana, lakini kuondoka kwa hao wenzie kukamuongeza sana hamu Dekula ya kuja  Afrika Mashariki.
Siku moja mtu mmoja aliyeitwa Alida Shanga akamfwata Dekula na kumwambia kuwa ametumwa na Mzee John Luanda aliyekuwa anamiliki Chamwino Jazz Band, kuja kutafuta wanamuziki toka Kongo. Bila kusita Dekula na wenzie kadhaa wakafanya mipango na kuondoka Kongo kwenda Dar es Salaam Kujiunga na Chamwino Jazz band. Baada ya kushuka kwenye treni, kituo chao cha kwanza kilikuwa Tandale jijini Dar es Salaam, bila kuchelewa, siku waliofika na ndio siku wakaanza mazoezi.
Wakiwa bado vijana, yeye na wenzie watatu walikuja wakiwa na staili ya  kuimba na kucheza steji show ambayo wakati huo marehemu Julius Nyaisanga aliita sarakasi, si hivyo tu na pia wao ndio kilikuwa kikundi cha kwanza kuanza kurap katikati ya nyimbo. Waimbaji wakiwa ni   Sisko Lunanga, Fanfan Bwami, na mwenzao mmoja Baposta Kilosho ambae hatimae alirudi Kongo. 

Recording ya kwanza ilimuacha Julius Nyaisanga akishangaa vituko vya vijana hawa. Katika bendi ya Chamwino wakati huo wapiga magitaa walikuwa Vumbi Dekula, Kazembe wa Kazembe (huyu alikuwa Msukuma ambaye aliishi kwa muda Kongo na alikuwa mpiga gitaa hodari sana), na Mzee Albert huyu kwa sasa  yupo Manzese amepumzika. Baadae walimchukua Muhidin ambae alikuwa mpiga bezi wa Dr Remmy.
Siku moja walienda kuomba kupiga na Maquis Original, kwa ile staili ambayo wanamuziki huiita lift au kijiko,  wakati huo zaidi walikuwa wakipiga nyimbo za kopi kama Mario, Maze na kadhalika, hivyo wakazipiga hizo na watu wakafurahi sana na kuwatuza  fedha nyingi, wakachanganyikiwa maana bendi yao ya Chamwino ilikuwa haina mshahara na si mara moja walitembea kwa miguu kutoka Buguruni hadi Tandale kwa kukosa hata nauli.  Wakati huo kwa kuwa walikuwa wadogo kwa umri na hata umbo, marehemu Ndala Kasheba alikuwa akiwaita ‘Vimario’, hata hivyo upigaji wao ulikuwa mzuri sana.
Nguza aliwashauri wawe wanakuja kupiga kabla Maquis hawajaanza kupiga. Hivyo wakaamua kuiacha Chamwino, na wakawa wanasindikizana na Maquis, hili lilimuudhi John Luanda aliyewaleta nchini. Siku moja wakiwa Silent Inn, maafisa wa Uhamiaji walikuja kuwachukua wakalazwa Central Police na kisha kupelekwa gereza la Keko. Wakiwa huko walimwandikia barua Mzee Luanda kumuhakikishia kuwa watarudi Chamwino, basi wakaachiwa na kurudi na kuisuka upya Chamwino Jazz Band.
Lakini hawakukaa muda mrefu Mzee Makassy akaja kuwaomba waingie katika bendi yake, wenzake waimbaji  wakaenda  yeye akabaki Chamwino, lakini muda si mrefu Nguza akamwambia aandike barua ajiunge na Maquis. Nae akafanya hivyo na ndio kujiunga rasmi na Maquis kama mpiga gitaa la second solo. Aliwakuta wanamuziki kama Maneno Uvuruge, Omari Makuka, Keppy kiombile, Ilunga Lubaba, William Maselenge na wanamuziki wengine wengi wazuri.  Aliendelea kupiga second solo hadi siku moja bendi ilikuwa inapiga maeneo ya Ukonga, kwa kawaida Mzee Lubaba alikuwa anapiga kuanzia saa tatu mpaka saa sita, na  kisha Nguza Viking akiingia na kuendelea .

Maquis wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma,  wa pili toka kulia na shati jeusi Vumbi, wapili toka kushoto na suruali nyeusi Issa Nundu

Siku hiyo Nguza hakuonekana, Vumbi  akaweza kupiga nyimbo zote za Nguza, na kesho yake  akaambiwa afike ofisini akasainishwa rasmi mkataba wa kuwa mwanamuziki wa Maquis.  Baada ya muda mfupi Nguza akaacha bendi. Muda mfupi baada ya hapo walirekodi ule wimbo maarufu wa Makumbele, solo ya wimbo huu ilikuwa awali ikipigwa na Mzee Lubaba, lakini afya ya mzee Lubaba ilianza kuzorota nae akawa anawafundisha nyimbo zake wanamuziki wengine, wimbo wa Makumbele alifundishwa  Omari Makuka na akawa anaupiga katika maonyesho mbalimbali, lakini wakati wa kutaka kurekodi kamati ya uongozi ya Maquis iliamua Vumbi aufanyie mazoezi  na aurekodi. Kurekodiwa kwa album ya Makumbele ilitokana na safari ndefu ya bendi ambayo ilichukua miezi mitatu katika mikoa ya Ziwa, hivyo bendi iliporudi Dar  ilikuta sifa ya bendi imepungua, hivyo walirekodi album ya Makumbele iliyokuwa na nyimbo kama Tipwatipwa, Ngalula na Makumbele, sifa ya bendi ikarudi juu tena kwa mara nyingine. Na ni wakati huo ambapo bendi ilihamia katika ukumbi wa Lang’ata Kinondoni. Vumbi aliendelea kupiga katika bedi hii mpaka alipoamua kuhamia Sweden ambako yuko mpaka leo akiendelea kupiga muziki.