Sunday, December 11, 2022

BURIANI TSHALA MUANA

 

MAREHEMU TSHALA MUANA

Jana Jumapili tarehe 10 Disemba 2022, Claude Mashala, mwenza na producer wa Tshala Muana alitushtua wapenzi wa muimbaji mkongwe Tshala Muana kwa kuandika kwenye ukurasa wake wa Facebook maneno yafutayo, “Alfajiri ya leo, Bwana mwema ameamua kuchukua Mama wa Taifa. Mungu atukuzwe kwa nyakati zote njema alizotupitisha  hapa duniani. Kwaheri Mamu wangu,”  kwa maneno haya tukafahamu kuwa mwanamuziki Tshala Muana hatunae tena. Tshala Muana ametuacha akiwa na umri wa miaka 64.

Lisabeth Tshala Muana Muidikay, anayejulikana pia kama Tshala Muana,  na sifa zaidi ya 'Malkia wa Mutuashi' alizaliwa tarehe 13 Machi 1958 huko Lubumbashi. Alikuwa mtoto wa pili katika familia iliyokuwa na watoto kumi. Mama yake, Alphonsine Bambiwa Tumba alikuwa mjane mwaka wa 1964 baada ya mumewe Muidikay Amadeus aliyekuwa mwanajeshi,  kuuawa na wafuasi wa marehemu Patrice Lumumba.

Elise alianza kuimba toka alipokuwa mdogo, alikuwa muimbaji kwenye kwaya ya  kanisa la kambi ya jeshi ya Kibembe. Mnamo 1967, miaka mitatu baada ya kifo cha baba yake, mama yake alihama na watoto hadi Kananga, Lisabeth akahamia Kinshasa mwanzoni mwa miaka ya 70. Mwaka 1976 akajiunga katika kikundi cha muimbaji M'Pongo Love akiwa kama mcheza show, baadae akahamia kundi la Minzoto Wella Wella na hatimae akajiunga na Les Tigresses d'Abeti Masikini, kundi la muimbaji nguli wa kike Abet Masikini.

Mnamo 1978, aliondoka kwenda Afrika Magharibi, safari yake ilianzia Jamhuri ya Afrika ya Kati na kupitia Nigeria na Togo na hatimae kutua Ivory Coast. Wakati huu huu ambapo Sam Mangwana na kundi lake la African All Stars waliweka makazi yao mjini Abidjan na kuingiza upenzi wa muziki wa Kongo katika eneo hilo la Afrika. Msanii na mtayarishaji wa Ivory Coast Jimmy Hyacinthe aligundua kipaji chake cha Tshala Muana kama muimbaji na mtunzi wa mitindo ya kucheza, akamjumuisha katika bendi yake, kwa pamoja wakaenda Paris mnamo 1982  na Lisabeth ambaye sasa akaanza kujulikana kwa jina la Tsala Muana akarekodi nyimbo zake za kwanza mbili katika santuri. Mmoja wa Kifaransa ulioitwa ‘Amina' na wa pili ulikuwa ‘Tshebele’ uliokuwa katika lugha yake ya Kikasai na ulikuwa wa mtindo wa mutwashi uliotokana na ngoma ya waBaluba kabila lake Tshala Muana. Kutokana na umahiri wake umaarufu wake ulikua haraka nchini Ivory Coast na nchi jirani.
Mnamo 1984 alirudi Paris  na kuishi huko kwa muda mrefu, kipindi ambacho Paris ilikuwa kitovu cha muziki wa Kiafrika kimataifa. Akiwa huko akisaidiana na mpiga besi, mpangaji wa muziki  na mtayarishaji Aladji Touré wa Cameroon, alirekodi albamu kadhaa  kama  'Kami', 'Mbanda Matière' na 'M'Pokolo'  chini ya lebo ya Safari Ambiance, nan i wakati huohuo akaanza kufanya kazi na mpiga gitaa mahiri wa Kongo Rigo Bamundele Star. Tshala aliandika nyimbo zake nyingi yeye mwenyewe na tofauti na wasanii wengine wengi wa Kongo, hakuishia tu na rumba ya Kongo inayoimbwa kwa lugha ya Kilingala na kwa mtindo wa  soukous tu, aliongeza vionjo vyake vingi kutoka kwa ngoma ya kwao ya Mutwashi. Katika albamu zake na katika maonyesho yake, alitoa nafasi kubwa kwa nyimbo katika mahadhi ya mutuashi, zilizoimbwa kwa lugha yake ya mama Tshiluba. Kwa kiasi kikubwa ni kutokana na Tshala Muana, mtyindo wa Mutwashi umejulikana zaidi duniani. Baada ya Abidjan na Paris, mwaka 1986, alirudi Kinshasa ili kujitambulisha tena "nyumbani". Japokuwa maonyesho yake yalipokelewa vizuri, muda si mrefu ilidhihirika kuwa uchumi duni wa nchi yake ulimfanya  kushindwa kujipatia riziki nchini Kongo. Alirudi Paris kuendelea na kazi yake kutoka huko. Alifanya hivi kwa kutoa albamu mpya kwa utaratibu wa album moja  kila mwaka na kisha kuzuru Ulaya na Afrika. Pamoja na Mbilia Bel, alikua mmoja wa 'Wanawake Wanaoongoza' wa muziki wa Kongo mwishoni mwa miaka ya 1980. Lebo ya kiMarekani ya Shanachie pia ilitoa mkusanyo wa nyimbo zake kwenye CD mwaka wa 1991, nyimbo nyingi kwenye albamu hiyo zilikuwa katika  mdundo wa mutuashi. Katika miaka ya 90, Tshala Muana aliendelea kujiendeleza kimuziki. Katika miaka hiyo aliandika nyimbo kadhaa ambazo alifanikiwa sana kuvuka Mutuashi na pia kupiga katika mtindo wa  Salsa. Matokeo ya haya yanaweza kusikika kwenye baadhi ya nyimbo za CD 'Mutuashi', iliyotolewa na lebo ya British Sterns mwaka wa 1996. Mnamo 1998, alishiriki pia kwenye albamu ya tatu kutoka mfululizo wa 'Sans Papiers', iliyotolewa na Ibrahim Sylla. Katika albamu hii, iliyoandaliwa na Lokassa Ya Mbongo, waimbaji wengine katika album hiyo walikuwa Mbilia Bel, M'Pongo Love, Oumou Sangare na Nahawa Doumbia, waimbaji wanawake wakali sana Afrika.
Mwaka wa 1997 Laurent Désiré Kabila alipochukua utawala kutoka kwa Mobutu Sese Seko kama Rais wa Kongo,  Tshala Muana alianza kujihusisha na siasa za Kongo. Mnamo 1999 alikua mjumbe wa kitaifa katika Bunge la Mpito la Bunge la Katiba na Sheria. Hii ilifuatiwa na miaka mitatu ambayo hakuna albamu yake moja iliyotolewa. Kwa bahati nzuri, baada ya hapo alianza pale alipoishia mwaka 2002 na albamu ya 'Dinanga', ambayo ina maana ya 'Mapenzi'. Albamu iyake ya 21 iliyoitwa 'Malu', ilishinda tuzo ya msanii bora wa kike katika tuzo za Kora 2003. Albamu ya 'Malu' iliuza zaidi ya nakala 500,000. Mnamo 2006, alitoa albamu mbili yenye jina 'Mamu Nationale' ambayo inamaanisha 'Mama wa Taifa', likawa pia jina lake jipya. Katika miaka iliyofuata, aliendelea kutoa albamu mara kwa mara. Mnamo 2018, kwa mfano, alitoa albamu 'Don de Dieu' pamoja na Mbilia Bel. Baada ya karibu miaka 45, mnamo 2020 ilionekana kana kwamba kazi yake ya muziki ilikuwa imekamilika. Baada ya kulazwa hospitalini kwa dharura mnamo Juni 2020, ripoti zilienea kwamba 'Malkia wa Mutuashi' alikuwa amefariki. Muda mfupi baadaye, hata hivyo, alitoa taarifa akisema kwamba bado yuko hai na yuko mzima. Kwamba yeye bado yuko katikati ya maisha ya muziki na kisiasa ilithibitishwa miezi michache baadaye mnamo Novemba wakati alitoa wimbo 'Aliyekosa shukurani'. Maneno ya wimbo huo yalimuudhi Rais Tshikseki hadi Tshala. Huyo ndie Tshala Muana ambaye alfajiri ya Jumapili 10 mwezi wa 12  mwaka 2022, ametuacha duniani , Mungu amlaze pema, mwendo ameumaliza.

1 comment: