TheDynamites..Salim wa kwanza kushoto |
Salim wa pili kushoto, Paul Muhuto wa tatu toka kushoto. Seaview Hotel |
Salim Willis ni mmoja wa wanamuziki waliowahi kupigia bendi
ya Afro70, alianza kupata hamu ya kuwa mwanamuziki baada ya kuwa mpenzi mkubwa
wa filamu za Elvis Presley, mwanamuziki mahiri wa muziki wa rock'n'roll aliyetawala anga za muziki wa
dunia kwa muda mrefu, na hata baada ya kifo chake santuri zake bado zinauza kwa
wingi zaidi ya wanamuziki wengi walio hai
mpaka leo. Moto huu wa kutaka kuwa mwanamuziki ulimfanya aanze
kuhudhuria maonyesho ya bendi ya Wagoa iliyotengenezwa na wanafunzi wenzie
wakati akisoma shule ya St Xavier(Kibasila). Hapo akawa kila bendi ikipiga yeye
alianza kupiga marakasi, pamoja na ugomvi mwingi aliozua wakati akipiga chombo
hicho kutoka kwa wanamuziki wa bendi hiyo aling’ang’ania na hatimae akawa
mahiri kiasi cha kutakiwa kutokosa wakati wa maonyesho ya bendi hiyo ambayo yote yalifanyika
pale shuleni. Kutoka shule ya St Xavier akahamia St Joseph ambako huko akakutana wapenzi wa muziki
wenzie na kuanzisha kundi la Dynamites akiwa mpiga drums. Kundi lake la
Dynamites lilikuwa na wanamuziki
wafuatao; Abdallah Boja, Bashir Farahani, Mohamed Manyika, Salha,
na yeye Salim katika drums. Kwa
kadri ya mfumo uliokuwa wakati ule kulikuwa na vikundi vingi vikiwa na majina
lakini havikuwa na vyombo, kwa hiyo vijana wa vikundi hivi walifanya mazoezi
kwa kutumia magitaa baridi na hatimae kuzunguka kufuata bendi kubwa na kupata
nafasi ya kutumia vyombo vya umeme pale bendi hizi zinapokuwa katika mapumziko.
Kulikuwa na kawaida ya bendi kupumzika nusu saa katika kila onyesho. Hivyo
Salim alikuwa katika kikundi cha
Dynamites na kuzunguka kwenye mabendi kutafuta nafasi ya kuachiwa kupiga vyombo vya moto.
Alipohamia St Joseph ndipo wakati huohuo alipoanza
kufuatilia bendi ya Sparks ambayo ilikuwa ikipiga Gateways, na yeye kwa kuwa
alikuwa akiishi Gerezani aliweza kusikia muziki wa bendi hiyo na kuanza kuhakikisha
hakosi kwenye maonyesho ya bendi hiyo. Nako huko akakimbilia chombo chake cha
maracas, hapa wakamtambua kuwa anaweza japo alikuwa mfupi sana akawa anawekewa
kiti cha chuma awe anaonekana. Hapa akakutana na Paul Mhuto na urafiki wao
wakaanzisha kundi la Gypsies. Huu ukoo wa akina Mhuto walikuwa wanamuziki
wazuri wote wakijua kupiga kwa umahiri vyombo mbalimbali, na
Salim nae akaanza kuwa na hamu ya kujifunza gitaa hasa kwa ajili ya kuupenda
sana wimbo maarufu wa Besame mucho. Akafikia mpaka akaweza kupiga wimbo huo kwa
kidole kimoja, bila hasa hata kujua ni chord gani hupigwa wimbo huo, lakini hii
ilikuwa hatua kubwa katika kuonyesha nia ya kuweza kupiga wimbo huo. Mmoja wa
wanamuziki wa Sparks akampa kitabu cha kujifunzia chords za gitaa, akampa pia
na gitaa aende nalo nyumbani akajifunze. Wakati huo huo akawa anajiendeleza katika drums chini ya mwalimu wake George Muhuto, ambaye alikuwa akimuelekeza
beats fulani na kumpa homework kuwa lazima ajue hizo beat kufikia kesho yake.
Na kwa juhudi zake mwenyewe za kuanza kufuatisha mapigo ya santuri za vikundi
mbalimbali kama The Famous Flames ya James Brown akawa mpigaji mahiri. Akawa
anaruhusiwa kupiga nyimbo za polepole na kuruhusiwa kuwa kwenye jukwaa mapema
kwani ilikuwa lazima arudi kwao kabla ya saa nne. Wakati wote huo alikuwa akitoroka
tu nyumbani kwao kwa kupitia tundu alilolitengeneza kwa kufumua vigae vya
nyumba yao ambayo ilikuwa moja ya kota za relwe. Baba yake alipogundua akamtuma
mfanya kazi wao mmoja amfuatilie ajue anaishia wapi , mfanya kazi akarudi na
jibu kuwa jamaa anaishia kwenye muziki na anapiga sana. Baba yake hakuchukia
ila alimwambia awe anagonga
anapitia mlangoni. Muda si mrefu baada ya hapo bendi ya Sparks ikafa
ikazaliwa The Comets. Hapo ndipo likaanzishwa pia kundi la Gypsiys ambalo alikuweko
yeye Salim Willis, Paul Muhuto, Charles Sabuni, Omari Sykes na Abraham Sykes na
Mzanda. Kwa vile kundi lilikuwa halina vyombo, wakawa hawana mahala pa
kufanyia mazoezi basi wakaamua kuwafuata Afro70 ambao wakati huu walikuwa
wakipiga Princes Bar..........
Nini siri ya kifo cha mwanamuziki Gobby? Kitime umeuliza swali la msingi sana ambalo hujalijibu.
ReplyDelete