Hatimae mwanamuziki Kabeya Badu (1945-2013)amezikwa katika makaburi ya
Kinondoni mchana wa leo kwenye muda wa saa kumi na nusu.
Kaburi la Freddy Ndala Kasheba |
Katika mlolongo wa taratibu za mazishi haya King Kiki
aliombwa kutoa maelezo machache kuhusu marehemu na katika maelezo mafupi
aliweza kuleta maelezo ambayo yaliwatoa machozi watu wengi. King Kiki alieleza
kuwa yeye, marehemu Ndala kasheba na sasa marehemu Kabeya wametoka mji mmoja huko
Kongo unaoitwa Likasi. Kila mmoja katika ujana wake alikuwa akiendelea na
shughuli zake za kimuziki japo walifahamiana. Kabeya hatimae alijiunga katika
kundi maarufu la muziki wakati huo la Baba Gaston. Katika mizunguko yao ya
maisha wakajikuta wako pamoja katika kundi Safari Nkoy ambalo tayari King Kiki na Kasheba walikuwa
wakilipigia, awali kundi hili lilikuwa liiitwa Orchestra Fauvette na lina historia ndefu hapa Tanzania. Mwaka 1974
Kiki alaliacha kundi hili na kuelekea Tanzania, ambako alifanya mambo mengi kimuziki katika bendi ya Maquis. Mwaka 1978 akiwa Orchestra Maquis, aliweza kuushawishi
uongozi wa Maquis wakati ule kuwa kuna wanamuziki wangeweza kuongeza sana nguvu kwenye bendi
hiyo kwa upande wa uimbaji, na ndipo Kabeya Badu, Kalala
Mbwebwe na Chatanda Ngalula walipofuatwa Congo na kuja kujiunga na Maquis. Kiki
alipohamia Orchestra safari Sound alihama na Kabeya na Kalala na kwenda
kuanzisha Masantula Ngoma ya Mpwita. Kabeya alihamia tena Maquis na kisha
kwenda Tancut Almasi ambako alikaa kwa miaka kadhaa kisha kurudi Maquis kwa
muda na kuhamia Zaita Muzika wakawa tena wote na Kasheba. Kundi hilo hatimae ikawa Wazee Sugu na Kabeya kadumu na kundi hilo mpaka mwisho wa uhai wake. Hapa ndipo King Kiki alionyesha
masikitiko yake pale alipowaambia watu kuwa wenzie wote hao sasa ni marehemu.
Kalala Mbwebwe alifia Iringa miaka kadhaa iliyopita.
Jambo la kushangaza ni kuwa bila kupanga kaburi la Kabeya
Badi liko jirani kabisa na kaburi la Freddy Ndala Kasheba.
No comments:
Post a Comment