Monday, November 5, 2012

MANENO UVURUGE MPIGA GITAA MAHIRI


Maneno Uvuruge ni moja ya wanamuziki waliotoka katika familia ya wanamuziki ya ukoo wa Uvuruge. Kaka zake Jumanne, Stamili, na Huluka ni kati ya wapiga magitaa walioheshimika sana katika jamii ya wanamuziki wa bendi Tanzania.
Jumanne Uvuruge ambae alikuwa mkubwa wa akina Uvuruge wote, ndie aliyetunga kibao maarufu cha Georgina, kilichopigwa na Safari Trippers na kuimbwa na Marijani Rajabu. Siku zake za mwisho za maisha Jumanne alikuwa anajishughulisha na kupata riziki yake kwa kuzunguka katika mabaa mbalimbali na gitaa na kupiga maombi mbalimbali ya wanywaji, na kisha kuhama na kuelekea baa nyingine. Hayakuwa maisha rahisi.
Maneno Uvuruge hana kumbukumbu ya jinsi gani Jumanne alijifunza gitaa, lakini anajuwa kuwa Stamili alifundishwa na Jumanne. Anakumbuka zaidi jinsi Huluka alivyojifunza kwani ndie alikuwa kaka yake waliefuatana kuzaliwa. Huluka alijifunza gitaa kwa kuanza kuchonga gitaa lake mwenyewe, akiiba mishipi ya kuvulia ya baba yake na ndio zikawa nyuzi za gitaa lake, siku babake alipogundua wizi huo alivunja vunja gitaa na kumkataza asiguse mishipi yake tena, lakini akamwelekeza inakonunuliwa, Huluka alitafuta pesa na kwenda kununua mishipi na kuendelea na gitaa lake la kopo. Wakati huo Huluka alikuwa anasoma, naye Maneno akaanza hamu ya kutaka kujua kupiga gitaa akawa anaiba gitaa hilo la kaka yake kila alipoenda shule, ilikuwa ni ugomvi kila alipokata nyuzi kwani alikuwa bado anajifunza. Jumanne na Stamili wakaanza rasmi kumfundisha gitaa Huluka nae akalijua vizuri sana. Si muda mrefu baadae nae akaanza rasmi kumfundisha mdogo wake. Maneno anasema wimbo wa kwanza kakake kumfundisha ni ile rhythm ya wimbo Novelle Geneation wa Orchestra Lipualipua, wimbo huu ulikuwa ni kipimo muhimu kwa wapiga rythm wengi enzi hizo. Mwanamuziki muimbaji marehemu Freddy Benjamin ndie aliyemshauri kujiunga na bendi. Alimkaribisha UDA Jazz ambako alikuwa akiimbia na pamoja na kuweza kupiga gitaa alifanyiwa mizengwe na mpiga rhythm aliyekuweko na ambae pia alikuwa katibu wa bendi. Baadae Freddy huyohuyo alimuombea kazi Super Rainbow iliyokuwa na makao yake makuu pale Sunlight Bar Mwananyamala B. Na hapo akakutana na wanamuziki kama Hatibu Iteytey aliyekuwa bingwa wa kupiga saxaphone, Nuzi Ndoli muimbaji, Rocky, Mzee Bebe, wakati huu Eddy Sheggy alikuwa bado hawajajiunga na bendi hii. Hatimae si muda mrefu Eddy Sheggy na Emma Mkello walijiunga na Super Rainbow, hawa hukumbukwa sana na wapenzi wa muziki kutokana na ule wimbo wa Milima Ya Kwetu, pia nae Banza Tax baadae akajiunga kipindi hiki. Na kule Mabibo bendi ya Mambo Bado ilipata msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo wanamuziki wake Juma Choka mpiga drums, Lodji Mselewa na Nana Njige pia wakajiunga na kundi na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana Assossa aliweza kuifufua tena Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari bendi ilikuwa iko katika hali mbaya kwani Assossa aliacha tena akiwa katika harakati ya kuunda bendi mpya na hivyo Orchestra Mambo Bado ikafa rasmi. Juma Choka akamtaarifu Maneno kuwa Urafiki Jazz kuna nafasi ya kazi na hapo akenda na kusailiwa na Ngulimba wa Ngulimba, Marehemu Mzee Juma Mrisho, Urafiki nayo ilikuwa katika siku zake za mwisho lakini bado yule mpiga solo mahiri Michael Vicent alikuweko. Kipindi hiki pia Urafiki Jazz iliwapata wanamuziki kama  Mohamed Gota gota na Hussein Jumbe. Maneno Uvuruge sasa alianza kufahamika kwa wanamuziki wengine kuwa ana uwezo mkubwa na bendi zikaanza kumsaka, na kuanzia hapo amekuwa hatafuti kazi bali anatafutwa. Bendi ya kwanza kumchukua ilikuwa ni Maquis, alichukuliwa ili awe mpiga gitaa la rhythm, aliwakuta wapiga rhythm wawili, huko, Mbwana Cox na Omari Makuka, nae akawa mwanamuziki wa kutegemewa wa Maquis, wakati huo wapiga solo wa bendi hiyo walikuwa ni Nguza Viking, na Mzee Lubaba.
Kama kawaida ya wanamuziki, mwanamuziki Belly Kankonde akakutana na Marehemu Mzee Mwendapole na kuamua kuipa uhai bendi ya Afrisongoma. Kankonde akawashawishi wanamuziki wenzie wanne wa Maquis, Maneno Uvuruge (guitar), Kiniki Kieto(mwimbaji), Comson Mkomwa(saxophone) na Keppy Kiombile(bass) wakahamia Afrisongoma. Maneno hakukaa muda mrefu katika bendi hiyo,kwani Nguza alimfuata yeye na Comson na kuwarudisha Maquis, na kwa kuwa walikuwa wamekwishapokea fedha za Mzee Mwendapole kesi ilifika polisi na ikalazimu Maquis warudishe fedha hiyo. Lovy Longomba alijiunga na Maquis nae hakukaa muda mrefu Mwendapole akamshawishi akaunde upya kundi la Afrisongoma ambalo katika awamu ya kwanza liliishia kurekodi mara moja na kutokuwa na maendeleo. Lovy pia tena akamuondoa Maneno na kuhamia nae Afrisongoma.
Wakati huo Mosesengo Fan Fan yule mpiga gitaa mahiri aliyetoka kwa Franco na kupigia Matimila na Makassy alikuwa amehamia Uingereza na akawa amemtaka Kiniki Kieto awashawishi Maneno Uvuruge, Keppy Kiombile, na Vivi Kapaya wamfuate,lakini mpango huo uliishia kwa Kiniki na Vivi kuendelea na Fanfan wakati Maneno na Keppy wakahamia Afrisongoma wakiwa na Lovy. Wanamuziki kadhaa walihamia Afriso wakati huo wakiwemo Kalamazoo mpiga saxaphone, na Mzee Mponda mpiga gitaa mahiri, ambae baada ya kutoka Msondo alikuwa kapita Sikinde na akatua Afrisongoma. Na hapo ndipo msondo wakamchukua Maneno kwa mara ya kwanza. Alikaa kwa muda na rafiki zake akina Benno Vila Anthony wakaweza kumshawishi ahamie Sikinde. Baada ya muda si mrefu Nguza akamfuata ili kumshawishi ajiunge na Orchestra Sambulumaa. Ilikuwa ni ushawishi wa Skassy Kasambula na Emmanuel Mpangala aliyekuwa mkurugenzi wa bendi ndio ulioweza kumfanya Maneno ahamie Sambulumaa.

1 comment:

  1. Historia kubwa sana ya Muziki wetu Tanzania,shukrani sana!!

    ReplyDelete