Tuesday, August 14, 2012

Mjue Anania Ngoliga sehemu ya 2


Anania Ngoliga Chalankhanya
Baada ya mtiti wa bendi nzima kuhama Ram Choc StarsAnania akarudi tena Legho Stars ikiwa inaongozwa na Joseph Mulenga,  kwenye gitaa la solo wakiweko Joseph Mulenga na John  Maida, rhythm Christopher Chiwaligo, kwenye Bass Adolf Mpoloto, waimbaji walikuwa Ana Mwaole, Banza Tax, Salim Shaaban na Anania Ngoliga. Baada ya muda si mrefu Anania akaacha tena  bendi na kuhamia kwenye bendi iliyokuwa mbioni kuanzishwa na bwana mmoja waliyemtambua kwa jina la Mponzi aliyekuwa ameanzisha bendi iliyokuwa inaitwa Ngoza Makayota Band, hapo hakukaa sana kwani kulikuweko tu na ahadi ya vyombo kununuliwa kukawa na mazoezi tu bila dansi na vyombo havikutokea. Yeye na  wanamuziki wenzake wakaondoka tena kundi zima na kwenda Iringa na huko wakajiunga na bendi iliyokuwa inaendeshwa na kanisa Katoliki la Mshindo iliyokuwa inaitwa VICO Stars (Vijana Catholic Stars). Hawakukaa muda mrefu katika bendi hii kwani ilikuwa na masharti magumu na pia haikuwa na fedha za kuwalipa kwani hata maonyesho yake yalikuwa machache sana ambayo karibu yote yalifanywa vijijini, hivyo wakalazimika kuhamia Dodoma ambako waliambiwa kuna bendi inayotaka kujipanga upya. Wakati huu walikuwa tayari wanasafiri  na kuhama kama kundi lililokuwa na wanamuziki watano, wakaenda Dodoma na kujiunga na Materu Stars, bahati mbaya hata katika kundi hili hawakupata nafasi ya kufanya onyesho lolote kutokana na tatizo la kukosekana kwa vyombo.Kwa bahati sana siku moja wakatembelewa na  Kasaloo Kyanga aliyewaambia wanahitajika  Iringa kwani kuna bendi ilikuwa inatakiwa kuanzishwa, wakarudi Iringa na kuanzisha Living Light Band , band ambayo ilianza kupiga katika hoteli ya Living Light iliyokuwepo eneo la Wilolesi, wakati huu ilikuwa mwaka 1993 mwishoni. kutokana na ubora wa kazi zake, Bendi ikapata mkataba Dodoma Hotel, tatizo lilikuwa mwenye bendi akatoa amri kuwa wanamuziki wapige muziki bila kulipwa chochote hadi pale atakaporudisha fedha alizonunulia vyombo. Hili lilikuwa gumu ukikumbuka kuwa hakukuweko na makubaliano yoyote kati ya wanamuziki na mwenye mali katika mkakati wa kununua vyombo. Ikalazimu wanamuziki waondoke kwenye bendi hii kwa ugomvi mkubwa. Kundi hili likapata taarifa kuwa kuna shirika lilioitwaTACOSODE lilikuwa na vyombo vya muziki, hivyo kundi hili lilijiunga na na kutengeneza bendi ya TACOSODE mwaka 1995, Anania aliweza kuendeleza bendi hii mpaka mwaka 2002 ambapo vyombo vilichakaa mpaka havikuweza kutumika tena. Baada ya hapo alijiunga na Tango Stars ambapo wakawa na bendi nzuri ambayo iliendelea vizuri wanamuziki wakiwa wanapata mishara , ghafla mwenye bendi akaamua kushusha mishahara kukawa hakuna jinsi ila kuhama ambapo Anania akahamia Karafuu band ya Zanzibar, na kisha kuhamia Kalunde Band ambako ndiko yuko mpaka sasa.

2 comments:

  1. VICO Stars ni Vijana Consolota Stars na sio Catholic kama ulivyosema!

    ReplyDelete
  2. Nakubaliana na wewe Vico Starsilikuwa VIjana Consolata Stars

    ReplyDelete