Sunday, July 22, 2012

Zamani kulikuweko na Bif?


Leo hii kuna neno maarufu limetokana kwa wasanii wa Kimarikani-BIF. Si kwamba ni utamaduni mgeni, ila utekelezaji wake ndio umekuwa tofauti siku hizi, siku hizi kumekuweko na utamaduni wa kuchochewa mara nyingine na vyombo vya habari ili kuuza magazeti au kukipa kipindi watizamaji au wasikilizaji, na kisha ukageuka upinzani mkali wenye uadui kati ya wasanii wawili. Miaka yote kumekuweko na upinzani katika sanaa, lakini mara nyingi ulikuwa ni wa aina ya kuleta ubora katika sanaa. Katika kipindi fulani cha miaka ya sitini muziki wa jiji la Dar katika nyanja ya Band za rumba ulitawaliwa na bendi mbili, Dar es Salaam Jazz- Majini wa Bahari na mtindo wao wa Mundo, na upande wa pili Kilwa Jazz. Ulikuwa mpambano mkali uliofikia hata wapenzi wa bendi hizi mbili kutandikana makonde wakikutana barabarani. Bendi zilitungiana nyimbo za mafumbo moja maarufu ulikuwa ule wimbo wa Dar Es Salaam Jazz Mali ya mwenzio siyo mali yako, ukiwadhihaki kilwa Jazz kutokana na eneo la Klabu yao kuwa na utata wa kodi. Morogoro kulikuwa na miamba wawili, Morogoro Jazz na Cuban Marimba, ushindani wao uliweza kuwasha moto wa upenzi Afrika ya Mashariki nzima, watu walikuwa wanajitahidi kuwepo Morogoro siku za wikiendi ili tu kuhudhuria bendi ambayo waliipenda kati ya hizi mbili, Morogoro Jazz wakiwa na mtindo wao wa Sululu, Cuban Marimba na mtindo wa Ambianse. Nao pia walitunga nyimbo zenye vijembe nyingi zilizowatia kiwewe wapenzi wao, Cuban walikuja na mtindo wao Subisubi, wakijisifu kuwa wao ni Jini Subiani linanyonya. Tanga kulikuwepo na vijana wa Barabara ya 4 Atomic Jazz wana Kiweke, wakipambana na Jamhuri Jazz Band na mitindo yao mingi kama vile Dondola na Toyota. Ushindani huu uliendelea katika bendi mbalimbali, kama vile Juwata na Sikinde. Kuna ushindani mwingine ulikuwa zaidi ni wa kufikirika kama ilivyokuwa inadhaniwa na wengi kati ya Vijana Jazz na Washirika Stars, kiasi cha kwamba kuna wakati ule wimbo wa Nimekusamehe lakini sintokusahau ulitafsiriwa kuwa ulikuwa umetungwa na Hamza Kalala kwa ajili ya kumkashifu Hemed Maneti, japokuwa mtunzi wa wimbo huu Hamza Kalala ambae niliongea nae kuhusu wimbo huo karibuni alikataa kuwa aliutunga kwa ajili hiyo.
Kwa wapenzi wa muziki enzi za uhai wa Maquis Du Zaire, na Orchestra Safari Sound wanakumbuka ushindani mkubwa ulio kuwepo kati ya hizi bendi mbili ambazo kuna wakati huo zote zilikuwa zikiwa na makao makuu jirani, Maquis wakiwa Ubungo na OSS Kimara. Maquis walipoasisi mtindo wao wa Ogelea piga mbizi, OSS wakaja na Chunusi, wakiwa na maana ukiogelea kiboko yako Chunusi. Katika mtiririko wote huu wa ushindani mara chache sana ulifikia wanamuziki binafsi wakashikana mashati kwa sababu za ushindani. Na ushindani ulikuwa wa maana kwa kuwa kweli bendi zilipiga muziki tofauti, Jamhuri na Atomic zote zilikuwa bendi za Tanga lakini kila moja ilikuwa na muziki tofauti, na vivyo hivyo Moro Jazz na Cuban Marimba Band, au Tabora Jazz na Nyanyembe Jazz na Kiko Kids, ambazo zote masikani yake yalikuwa Tabora. Enzi hizo kila Jumanne asubuhi, Radio Tanzania ilikuwa na kipindi kilichorusha nyimbo zilizorekodiwa katika studio yake kipindi kiliitwa Misakato. Ilikuwa si ajabu kukuta wanamuziki wa bendi yenye ushindani ukisikiliza nyimbo mpya za washindani wao. Hata wanabendi wengine waliona ni muhimu kusikiliza kipindi hicho ili kujifunza mapya kutoka kwa wenzao, na hata kutoa sifa pale ambapo zinastahili, na mara nyingi baada ya hapo bendi zilijipanga kufanya kitu bora kuliko kilichotolewa na wenzao. Nakumbuka wakti fulani bendi Tancut Almasi ilikuwa Morogoro wakati Vijana Jazz wakirushwa nyimbo zao mpya za Ngapulila, Adza kwa mara ya kwanza katika kipindi cha misakato, ilikuwa muhimu kusikiliza kazi yao kwani wakati huo Shaaban Wanted ndio kwanza alikuwa kahama Tancut na kujiunga na Vijana Jazz, na mfumo wa vyombo wa Vijana ulikuwa sawa na Tancut na Washirika pia yaani Solo gitaa, Rythm Gitaa, Second solo, Keyboards, bass, na vyombo vya upulizaji. Hii haikuleta upinzani bali iliongeza ushindani, na Tancut waliweza kuboresha album yao iliyofuata iliyokuwa na nyimbo kama Helena Mtoto wa Arusha, Masikitiko na kadhalika.

5 comments:

  1. muziki wa wakati huo ulikuwa ni shule tosha ya maisha pia ukiachia burudani. watu kama akina kitine na wengine kila kukicha tunasikilizia kusikia wanaleta kitu kipya angalau siku moja tupate burudani kama za wakati huo. mheshimiwa kitime uko wapi ndugu tunahitaji kuona mchango wako katika muziki wewe ni muhimu sana

    ReplyDelete
  2. kaka kitime mimi ni fan wako sana napenda sana kutembelea hii blog yako ubarikiwe na kazi yako nzuri naomba kama hutajali utuweke ule wimbo wa talakatalaka mpakani yanitoa jasho na ule wimbo mwingine wa kila munu ave na kwao asnte sana na ubarikiwe sana

    ReplyDelete
  3. sijui zamani lakini BIF nyingi za sasa hivi ni kwa ajili ya kugombea market share tu

    ReplyDelete
  4. This is a master piece. Hebu ktk nyakati zijazo uzungumzie ama uwazungumzie wataalamu ama wahandisi wa sauti kwa maana ya sound engineers kwa sasa. wale wanaokuwa na bendi na wale waliokuwa studio za nyakati zile kama RTD . Walikuwa watu kama Chrispin Lugongo na James Muhilu. Ni upi mchango yao ktk kuinua kiwango cha ubora wa muziki na mashairi yake. Naitwa Louie

    ReplyDelete
  5. @ Anoymous July July 23, 2012 11:14 AM.

    Umenena!! tunapozungumzia muziki wetu wa kitanzania halisi na recordings pale Radio Tanzania Dar-es-salaam (RTD) enzi hizo huwezi kuwasahau sound engineer Chrispin Lugongo na James Muhilu. Hawa wali-play great role kufanya muziki uwe mzuri kama tunavyousikia. Si tu wali0master recording lakini pia waliweza kutoa ushauri mambo yalivyokuwa yakienda sivyo, inasemeka wimbo ulikuwa unaweza ukarekodiwa vizuri lakini wakati wa kumalizia kukafanyika kosa kidogo basi wimbo wote ulifutwa na kuanza upya.

    Pia tusimsahau Bwana Julius Nyaisanga ambaye ni mdau namba mbili kuutangaza muziki wa kitanzania kupitia kipindi cha kutambulisha nyimbo mpya enzi zile kipindi cha "MISAKATO" ambacho nakumbuka kilikuwa kinarusha Ijumaa Usiku saa nne hadi saa tano na kurudiwa siku ya Jumamosi Asubuhi -around saa nne pia had saa tano. Kikifungiwa na klabu Raha Leo Show

    Kisondella - (Mafinga-Iringa)

    ReplyDelete