Katika nyimbo zote za Tancut Almasi, husikika vyombo vya
upulizaji vya trumpet na saxophone. Tancut ilikuwa na mfumo wa kuwa na trumpet
mbili, alto saxophone moja na tenor saxophone moja. Katika nyimbo zake za kwanza kwanza
kulikuwa na wapigaji wawili Abdul Mngatwa na Mafumu Bilali Bombenga, Mafumu
aliyekuwa anapiga alto saxophone aliacha bendi na Akuliake Salehe, maarufu kama King Maluu alijiunga na
kushirikiana na Abdul. Hivyo katika nyimbo zote za Tancut Mzee Mngatwa
alikuweko akipiga tenor saxophone. Leo niwaletee historia fupi ya Mzee huyu.
Abdul Mngatwa alizaliwa mwaka 1952 katika kijiji cha
Kolang’a Misima wilaya ya Handeni. Alianza lower primary school mwaka 1960 na
baadae akafaulu kuingia upper primary school na hatimae kumaliza darasa la 7
mwaka 1966. Akiwa Handeni siku moja aliingia katika dansi lililokuwa likipigwa
na bendi ya JKT Kimbunga, ambapo
alimuona mpiga tumba anaemkumbuka kwa jina la Juma, ambaye alijifananisha nae
na kujiona kuwa na yeye anaweza kujiunga na Jeshi hilo, hivyo basi ilipofika
1969 akajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kambi ya Mgulani, Dar es Salaam. Akiwa
jeshini akajiunga na darasa la muziki ambapo mafunzo yalikuwa ni kusoma na
kuandika muziki ambapo alifaulu vizuri sana, na akiwa na wenzie 26
walichaguliwa kwenda kambi ya Makutopora kuanzisha Brass band ya kambi hiyo.
Walipofika huko walikaa miezi 6 wakishiriki katika kilimo cha zabibu maana
kambi hiyo haikuwa na chombo chochote cha muziki, hili wakaliona ni tatizo kubwa, hivyo kundi zima wakaamua kutoroka
na kurudi Mgulani, ambapo walipokelewa vizuri baada ya kutoa malalamiko yao. Malalamiko
yalisikilizwa na safari hii walipewa vyombo kila mtu na chombo chake. Ikumbukwe kuwa mpaka wakati huu hawa jamaa walikuwa wakijua kusoma na kuandika
muziki lakini walikuwa hawajui kupiga vyombo, hivyo wakaanza mara moja kila
mmoja kujifunza chombo alichokabidhiwa, Mzee Mngatwa alianza kujifunza
saxophone. Kati ya vyombo walivyopewa kulikuweko na magitaa, hivyo
waliporudishwa tena Makutopora walianzisha Brass band na ‘Jazz’ band. Abdul
Mngatwa aliteuliwa kuwa kiongozi wa kundi hili. Alilitumikia jeshi kama
mwanamuziki mpiga saxophone hadi mwaka 1981. Mwaka 1982 alikwenda kujiunga na
Asilia Jazz Band ya Dar es Salaam, hii ilikuwa bendi ya Wizara ya Utamaduni,
ambayo ilikuwa inatumia vyombo ambavyo vilikuwa na utata wa umiliki kwani Patrick Balisidya
mpaka umauti wake alikuwa anadai alidhurumiwa vyombo hivyo na Wizara hiyo, kwani alikuwa
akieleza kuwa alipewa vyombo hivyo na Mzee Sarakikya baada ya kushiriki
‘Maonyesho ya mtu mweusi’ yaliyofanyika Lagos, Wizara nayo ilisisitiza kuwa vyombo hivyo ni mali ya serikali kwani vilinunuliwa na Wizara hiyo.
Abdul Mngatwa watatu toka kulia mstari wa mbele. |
Mngatwa aliiitumikia Asilia Jazz mpaka Wizara yenyewe
ilipoamua kuifunga bendi
hiyo. Mwaka 1985 alijiunga na UDA
Jazz Band wana Bayankata, alikaa hapa kwa mwaka mmoja na kufuatwa na viongozi
wa Tancut Almasi Orchestra na kujiunga na bendi hiyo hadi nayo iliposambaratika
1993. Mzee Mngatwa ameshiriki nyimbo zote zilizowahi kurekodiwa na Tancut, ila
pia aliwahi kurekodi na bendi ndogo ya Materu Stars ya Dodoma katika album yao
ya Chabure, wakati akiwa bado Tancut Almasi Orchestra. Kwa sasa Mzee Mngatwa
yuko Iringa akifanya shughuli ya askari mlinzi katika Msikiti ulioko maeneo ya
Lugalo Iringa mjini.
No comments:
Post a Comment