Polygram ndio ilikuwa kampuni kubwa huko Kenya, yenye mitambo ya kufyatua santuri katika miaka ya 70, kampuni hii ambayo ilikuja baadae kuuzwa kwa kampuni ya Tamasha ndio iliyokuwa ya kwanza kufyatua nyimbo za Simba wa Nyika, kwa watakaokumbuka nyimbo za Arusha Jazz zilikuwa katika lebo ya Phillips, Polygram ilikuwa ni tawi la Phillips Kenya wakati huo. Kulikuweko pia, wakati huohuo kampuni kama Chandarana iliyokuwa Kericho hii ilikuwa na lebo ya Ngoma, na Sabasaba, ambapo bendi kama Tabora Jazz, Safari Trippers, Cuban Marimba zilifyatua santuri zao kwa lebo ya Sabasaba. Orchestra Fauvette ikiwa na akina Kasheba na King Kiki wakiwa vijana wakati huo walifyatua pia kwa lebo ya kampuni hiyo.
Baada ya Simba wa Nyika kuingia kurekodi nyimbo zao za kwanza na Polygram huko Nairobi waliamua kuhamia jiji hilo, ambapo walianza na show klabu yao ya kwanza ikiwa Shade Club iliyokuwa katika eneo la Parklands. Baada ya album yao ya kwanza kutoka hadharani, ambayo iliitwa ‘Jiburudisheni na Simba wa Nyika’ iliyokuwa na nyimbo kama Njoo Kijana Tushirikiane, I Love You Madina, Mama Sofia, Naepuka Mama umaarufu wa bendi ulipaa juu katika nchi zote za Afrika Mashariki. Huu wimbo Njoo Kijana Tushirikiane ulitaja majina ya wanamuziki wote wa Simba wa Nyika wakati ule. Ikawa bendi hii kila ikiingia studio iliteremsha vibao murua, Papara Zako Nimezizoea,Nafikiria nitakujibu,Mombasa na kadhalika zilivuma katika anga la Afrika Mashariki.
Ikumbukwe kuwa katika kipindi hiki mlipuko wa bendi kali kutoka Kongo ndio ulikuwa katika kiwango cha juu sana, Lipua lipua, Belabela, Orchestra Veve, Orchestra Sosoliso na bendi zingine nyingi kali, zilikuwa zikitoa vibao vipya kila wiki, kamwe haikuzima umaarufu wa Simba wa Nyika. Wakati huo kuna ya chombo kilichokuwa na umuhimu wa pekee nacho kilikuwa gitaa la rhythm, huko Kongo bendi kama Lipualipua ilikuwa na mpigaji rhythm maarufu Vata Mombasa ambaye alileta utamu mpya katika nyimbo za Lipualipua, katika Simba wa Nyika kulikuweko na Profesa Omari. Jina lake kamili lilikuwa Omari Shaaban. Katika nyimbo kadhaa na hata kwenye maonyesho ya Simba wa Nyika kibwagizo cha ‘Cheza na Profesa Omari’ kilisikika mara kwa mara, huku kutajwa tajwa kulifanya Profesa ajulikane sana kiasi cha kwamba siku ambayo hakuja kwenye muziki, wapenzi walilalamika na hata kuondoka kwenye muziki. Pamoja na kujulikana huku Profesa alikuwa mtu mtaratibu na mnyenyekevu ambaye alikuwa rahisi kuishi nae, na aliyekuwa anaipenda kazi yake. Simba wa Nyika iliendelea kuwa maarufu lakini kama wasemavyo Waswahili ngoma ikivuma sana hupasuka ndivyo ilivyokuwa kwa Simba wa Nyika. Umaarufu wa bendi hii katika miji ya Kisumu, Mombasa, Nakuru, Kakamega na miji mingine ya Kenya ulisababisha akina mama wenye fedha zao, maSugarMumy, kuivamia bendi na kushindana kuwachukua na kuwalea wanamuziki. Mama mmoja tajiri akamshika kiongozi wa bendi Wilson Peter, na pamoja na mengine akamnunulia gitaa la gharama aina ya Gibson la thamani ya dola 2500, na pia akampa gari aina ya Celester na kumuhamisha kutoka gari lake pijo 504, wakati huo Celester zilikuwa gari za matajiri tu, hapo Wilson akaanza kubadilika, kwa kutokuja kazini bila sababu, kuwafokea wanamuziki wenzake, kukaanza kutokea malalamiko toka kwa wanamuziki wenzie hasa pale yule Sugarmummy alipoanza kushiriki katika maamuzi ya bendi yakiwemo kuingilia mikataba ya bendi. Hapo ndipo wanamuziki wote waliamua kuondoka Simba wa Nyika na kuanzisha Les Wanyika ilikua November 1978.
Walioanzisha Les Wanyika walikuwa wanamuziki walewale wa Simba wa Nyika, walioyoongezeka ni John Ngereza , aliyekuja kupiga solo kuchukua nafasi ya Wilson Peter, Issa Juma, ambaye kwa kweli alikuwa ndiyo kwanza kajiunga na Simba wa Nyika akakuta kuhama huku. Wengine waliokuwemo katika bendi hii mpya walikuwa ni Profesa Omari (rhythm), Tom Malanga (Bass), Joseph Just(Tumba), Rashid Juma(Drums),Mohamed Tika(Vocals), Phoney Mkwanyule na Sijali Zua(Trumpets) hawa walikuwa wanamuziki toka Morogoro mazao ya mwalimu maarufu wa muziki Father Canuti, na pia walipitia Super Volcano. Recording ya kwanza kabisa ya bendi hii ndiyo iliyotoa album iliyokuwa na nyimbo kama Sina Makosa, Paulina, Pamela, Nisaidie baba na kadhalika. Waimbaji walikuwa Issa juma, Mohamed Tika na John Ngereza, saxaphone ilipigwa na Mkongo mmoja aliyejulikana kwa jina la Kayumba, yeye hakukaa sana bendi hii. Kitu kimoja ni kuwa katika kuhama huku hata George Peter nae alikuwa ahamie bendi mpya lakini wanamuziki kwa hasira hawakutaka tena mtu kutoka familia ya Wilson, kwani George hakuwa na ubaya wowote na wenzie.
Wimbo maarufu wa Sina Makosa ulitungwa na Profesa Omari japo yeye hakuwa mwimbaji lakini alijua kupanga vizuri magitaa na akautunga wimbo huu kutokana na hadithi iliyomtokea kweli………..itaendelea
Safi sana kaka Kitime...hii habari nilikuwa naisubiri sana kuhusu haya makundi mawili kama unakumbuka siku moja nilikutumia email kuulizia historia ya hizi bendi mbili....NAISUBIRI KWA HAME SEHEMU YA PILI YA HADITHI HII!...well done
ReplyDeleteMimi ni mgeni katika blog hii ila nimegungua kuwa kutokuijua kwangu mapema nimekosa mengi, hiyo story imenivutia sana kwa kweli na imenilazimu kuusikiliza tena huo wimbo kwabi kupata kisa chenyewe kumeongeza burudani nakumbuka nilisikia hapo awali kisa cha ile nyimbo ya Pamela kweli nilifurahi sana, kuanzia sasa sitakuwa nakosa kuingia humu.
ReplyDeleteMike
kaka naomba kujua wilson peter, george peter na william peter ni wenyeji wa mkoa gani??
ReplyDeleteUkisoma humu historia ya Simba wa Nyika utaelewa hilo swali kuwa Baba yao alitokea Burundi George na William walizaliwa Tanga
ReplyDelete