TBC Radio Pugu Road Dar es Salaam |
Utangazaji kabla ya Uhuru |
Mwaka 1951 afisa mmoja wa BBC alipendekeza kuanzishwa kwa redio katika koloni la Uingereza la Tanganyika, ili kupata ujuzi wa kutengeneza vipindi kwa ajili ya wenyeji wa nchi hii. Serikali ya Uingereza ikatoa kiasi cha dola 30000 na Dar es Salaam Broadcasting Station ikazaliwa. Redio ilianza na kutangaza kipindi kimoja cha Kiswahili kwa wiki, hii ikapanda kwa kipindi hicho kurudiwa mara mbili kwa wiki. Kutokana na uhafifu wa mitambo, ilikuwa vigumu kusikia matangazo hayo hata nje ya Dar es salaam tu. Taratibu vipindi vikaongezwa na mitambo ikaboreshwa na hatimae jina likabadilishwa na radio hiyo kuitwa Tanganyika Broadcasting Service. Kufikia 1954 pamoja na mapungufu mengi ya vifaa, radio ilikuwa na wataalamu wote wenyeji, lakini ilikuja kuwa na mafanikio ambayo yalikuwa kama kwa nchi nyingine nyingi zilizokuwa ni koloni za Uingereza.
Mwaka 1961 bila kumwaga damu Tanganyika ikapata Uhuru chini ya uongozi wa Mwalimu J ulius Nyerere na chama chake cha TANU. Serikali mpya ikaona redio ni kiungo muhimu cha kuunganisha wananchi na mipango ya serikali yao, lakini chombo hicho kilikuwa bado ni chombo binafsi hivyo mara nyingine kutokuwa na msimamo sawa na serikali. Mwaka 1964, Tanganyika ikaungana na Zanzibar, pamoja na Muungano huu kwa sababu ambazo ngumu kuelewa serikali ya Tanzania bara iliamua kutokuingiza teknolojia ya TV wakati Zanzibar iliamua kufanya hivyo na 1970 Zanzibar ikawa kati ya nchi za kwanza Afrika kuwa na TV ya rangi.
Kueleweka na kuenea kwa siasa ya ujamaa kulitegemea sana radio, mwaka 1965 serikali ya Tanzania ilitiaifisha TBC
na pia kuibadili jina na ikaitwa RTD Radio Tanzania Dar es Salaam, na shirika hili likawekwa chini ya Wizara ya Habari na redio ikawa chombo cha kuelimisha sera mipango na taratibu mbalimbali za serikali.
Jambo moja kubwa na baya ambalo wakoloni hasa wa Kiingereza walilifanya ni kujitahidi sana kufuta utamaduni wa nchi walizotawala na kuingiza utamaduni wao, na wananchi wengi waliopata elimu wakati huo na hata wale wanaoppata elimu sasa, elimu iliyo katika mfumo wa elimu ya wakati huo huona kujivua utamaduni wao na kuonekana mzungu zaidi ndio kilele cha mafanikio katika elimu. Hilo ndilo lililomfanya Mwalimu Nyerere atamke wakati wa kuunda Wizara ya Utamaduni na Vijana kuwa’….katika dhambi kubwa ambazo ukoloni ulifanya ni kutufanya tuamini kuwa hatujawahi kuwa na utamaduni wetu….’ Radio ikawa chombo kimoja kilichoweza kuunganisha watu wa nchi hii ambao walitokana na makabila zaidi ya 120 kuweza kutumia lugha ya Kiswahili na hatimaye kuifanya kuwa lugha ya Taifa. Nchi nyingine nyingi za Kiafrika ziliona suluhisho la kupata lugha ya Taifa ilikuwa ni kuchukua lugha ya wakoloni waliowatawala. Na mpaka leo tuna nchi nyingi za Kiafrika ambazo lugha zao za Taifa ni Kireno, Kifaransa au Kiingereza. Tanzania iliweza kuwa tofauti kwa hili, Mwalimu Nyerere aliona kurithi lugha ya wakoloni ilikuwa ni dalili nyingine ya mafanikio ya wakoloni ya kufuta utamaduni wa wananchi. Lakini tukumbuke kuwa wakati wa kupata Uhuru nchi nzima kulikuwa na watu wachache sana wenye radio, inasekemekana wakati tunapata uhuru kulikuweko na redio zisizozidi 100,000 nchi nzima, na nyingi zilikuwa Dar es salaam kwa vile hata TBC yenyewe haikuweza kusiskika mbali. Hata kufikia mwishoni mwa miaka ya 60 ni chini ya asilimia 30 ya wananchi walikuwa na uwezo wa kusikiliza RTD kila siku, ndipo serikali ikasambaza redio mashuleni na hata vijiji vingi vilipewa redio na kukawepo mahala pa kusikilizia redio, japo redio ilijikita zaidi katika vipindi vya ‘kuhamasisha maendeleo’ na hotuba mbalimbali za viongozi wakitoa maagizo mbalimbali.
Kiwanda cha kutengeza redio za bei rahisi kikaanzishwa Dar es Salaam. Tukapata redio maarufu kama National Panasonic 177, iliyopewa jina ‘redio ya mkulima’.
Ili redio isikilizwe lazima iwe na vipindi vya burudani,muziki ni sehemu muhimu ya burudani katika vyombo vya utangazaji, katika kile kilichoonekana kinaweza kukuza muziki wa Tanzania, ilifikia Bunge la Tanzania wakati huo likafikia mapaka kujadili kupiga marufuku muziki kutoka nje. Hili halikutimia japo redio ilielekezwa kuwa katika vipindi vyake vya muziki , ule wa kutoka nje usizidi asilimia 30 ya muziki wote utakaopigwa na kituo hicho. Ili kuweza kujaza asilimia 70 hiyo RTD ilifanya kazi kubwa ya kurekodi muziki wa aina mbalimbali kutoka hapa nchini, na hili limeifanya mpaka leo RTD sasa TBC, kuwa wameweza kuwa na maktaba kubwa sana ya muziki wa Tanzania wenye historia ya nchi yetu na watu wake na siasa zake na ndoto na mafanikio yake.
Shukurani sana kwa makala hii fupi lakini yenye mafunzo makubwa kuhusu hazina na historia ya nchi yetu Tanganyika. watu wangeelewa hiyo beti ya mwisho ya makala hii basi hata leo hii kungekuwa na hadhari kuhusu muziki wa nje na wa nyumbani ungepewa nafasi inayostahili. Pamoja sana mkubwa.
ReplyDeleteAsante kwa elumu yako..🙏
ReplyDelete