Friday, April 6, 2012

Wimbo wa Sina Makosa, ni hadithi ya kweli


Kwanza kabla ya kuendelea na historia hii ya Simba wa Nyika na matawi yake lazima nitoe shukrani za dhati kwa mwanamuziki Abou  Omari Njenga, ambaye bila yeye historia hii tusingeipata. Abou ambaye kwa sasa anaishi na kupiga muziki Japan, pia alipitia na kupiga katika makundi haya ameweza kukusanya karibu yote ninayoyaandika humu. Kwa kuwa naye pia likuwa mmoja wa wanamuziki wa makundi haya tutasikia habari zake katika maendeleo ya simulizi hii. Aksante sana Abou.
Wimbo wa ‘Sina makosa’ kwa kweli ulikuwa kama wimbo wa Taifa wa Afrika Mashariki, kila ulipoenda uliusikia na mpaka leo bendi nyingi zinaendelea kuupiga wimbo huu mzuri. Wimbo huu ulitungwa na Profesa Omari Shaabani ambaye ndiye aliyekuwa mpiga gitaa la rhythm na Kiongozi wa Les Wanyika.  Muimbaji kiongozi katika wimbo huu alikuwa Issa Juma, waliokuwa wakijibu walikuwa John Ngereza ambaye pia alikuwa akipiga solo na Mohamed Tika. Huyu John Ngereza, ambaye alitokea Amboni Jazz Band ya huko Tanga, aliendelea kuimba na kuwa muimbaji mzuri na anasikika vizuri katika nyimbo kama Afro, Amigo na Nimaru.  Issa Juma sauti yake iliongoza nyimbo kama vile Pamela, Paulina, Kasuku na Usia wa Baba. 
Profesa Omari Shaaban mtunzi wa 'Sina Makosa'
  Wimbo wa  ‘Sina makosa’ ulitokana na kisa cha kweli. Kuna dada ambaye ni mzaliwa Kisumu aliyekulia Nairobi ndie chanzo cha hadithi ya wimbo huu, dada huyu aliyekuwa akifanya kazi Kenya Extelecoms kiwa na wadhifa mzuri hivyo maisha yake kuwa mazuri alikuwa mpenzi mkubwa wa Les Wanyika hapo ndipo akakutana na Profesa Omari na kuwa na urafiki wa siri kwani alikuwa pia na mapenzi na bwana mwingine aliyekuwa akifanya Special Branch ya usalama wa Kenya, huyu bwana alikua na familia yake pia. Siku moja Profesa na huyu dada wakiwa wamekaa katika Coffe Shop kwenye jengo la Kenya Cinema wakipata kinywaji ndipo huyu bwana wa Special Branch alipowakuta hapo na kuanzisha vurugu kubwa na kumpiga sana Profesa aliyeokolewa na wapenzi wa muziki waliomfahamu. Huyu mtu wa Special Branch nae alikuwa mpenzi mkubwa wa Les Wanyika, na baada ya kutoa adhabu hiyo alimwonya Profesa kuwa akiwakuta pamoja tena angemuuwa. Baada ya hapo jamaa alimuacha huyo bibi lakini binti aliendelea kuhudhuria maonyesho ya Les Wanyika hata wimbo huo ulipotungwa na kuwa maarufu..Hasira za nini bwanaa, wewe unawake nyumbani nami nina wangu nyumbani chuki ya nini kati yangu mimi na wewe, nasema Sina makosaa bwanaa……………….inaendelea

No comments:

Post a Comment