Sunday, December 18, 2022

ABOU SEMHANDO ALIFARIKI SIKU MBILI BAADA YA KUONGOZA MSAFARA WA KUMZIKA DR REMMY

MarehemuAbou Semhando.

Ilikuwa ni mida ya saa tisa usiku, alfajiri ya Jumamosi 18 December 2010, nilipopigiwa simu na mwanamuziki mkongwe Luiza Nyoni, alikuwa analia akanambia kumetokea ajali na Abou Semhando aliyekuwa kwenye pikipiki amegongwa na gari na amefariki, ajali ile ilikuwa imetokea maeneo ya Mbezi Tanki bovu. Niliamka na kuelekea eneo la ajali na hakika taarifa ile ilikuwa ni ya ukweli. Nilikuta pikipiki ya Abou imepakiwa katika gari la polisi na gari iliyomgonga ikiwa kwenye mtaro. Abou ambaye kati bendi alizopigia ni pamoja na Sola TV, Vijana Jazz, Diamond Sound na Super Matimila kweli alikuwa amefariki..
Katika ajali hiyo gari aina ya benzi ilimgonga nyuma akiwa katika pikipiki yake wakati akitoka kupiga mziki maeneo ya Africana. Kwa maelezo ya wanamuziki wenzake Abou alipiga drums nyimbo ya pili toka mwisho na baada ya hapo kuamua kuelekea nyumbani ambapo ndipo alipokutana na ajali hiyo. Jambo la kusikisha pia ni kuwa Abou aakiwa na pikipiki yake ndiye aliyeongoza msafara wa mazishi ya Dr. Remmy Ongala siku mbili tu kabla kifo chake.
Gari lililohusika katika ajali

Pikipiki ya Abou

Gari lililohusika katika  ajali hiyo

Abou Semhando wa kwanza kulia akiwa na miwani kwenye shughuli ya kuaga mwili wa marehemu Remmy Ongala siku mbili kabla ya kifo chake. 

Ratiba ya  Mazishi ya mwanamuziki na na meneja wa Bendi ya African Stars-Twanga Pepeta  Marehemu Abou Ally Semhando “BABA DIANA”

         Jumamosi 18/12/2010-ndugu na jamaa kukusanyika nyumbani kwa marehemu, Mwananyamala Kisiwani(Ngilangwa) kwa ajili ya kutoa pole na kuwafariji wafiwa.
         Jumapili 19/12/2010-Saa 11 Swala ya alfajiri katika msikiti wa Muhimbili, baada ya swala waombolezaji kuingia katika magari na kuelekea kijiji cha Kibanda, Muheza tayari kwa mazishi.
         Mara baada ya chakula cha mchana mwili kupelekwa msikiti wa Muheza nabaada ya swala mwili kupelekwa makaburini kwa maziko.
         Waombolezaji watarejea Dar es Salaam baada ya maziko.
1.19/12/2010 ni siku aliyokuwa amuoze binti yake wa kwanza
2. Alikuwa ameuandikia uongozi wa Bendi kuwa umpe likizo ya mwezi kwani alitaka asiweko katika jukwaa kwa kipindi. Ni mara ya kwanza yeye kuandika barua ya kuomba likizo
3. Katika simu yake ringtone aliyoiweka ni ya wimbo wa Njohole Jazz Band- bendi hii wanamuziki wake karibu wote walikufa pamoja katika ajali mbaya ya gari.

Waliosimama..Remmy Ongala, Abuu Semhando,Kasaloo Kyanga, Fan Fan wote wamekwisha fariki.

Abou Semhando alikuwa mpiga drum wa Remmy Ongala enzi za Super Matimila na mtindo wao wa Talakaka. 1981. 
Mara baada ya mazishi ya Dokta Remmy, Abou Semhando na Cosmas Chidumule walikuwa wakitaniana, kuwa nani atakaefuata baada ya kifo cha mwenzao,
Abou Semhando : Utafuata wewe ukawe unamsaidia kuimba.
Cosmas Chidumule: Mi sitaki utaenda wewe  mpiga drum wake.
Siku mbili baadae Mungu akapitisha uamuzi wake.

MUNGU WASAMEHE MAPUNGUFU YAO NA KUWALAZA PEMA 
AMEN

1 comment:

  1. Sehemu inayosikitisha zaidi ni hiyo ya utani wa Cosmas Chidumule na Abou Semhando. Sijui baada ya kusikia kifo baada ya utani wao Cosmas alijisikiaje.

    ReplyDelete