Sunday, March 9, 2014

URAFIKI JAZZ BAND 2

Urafiki Jazz Band
Bendi ya Urafiki ikiwa katika hali yake ya uchanga mwaka 1970 ilipata ajali ya gari, wakati kundi zima likitoka katika onyesho huko Chang’ombe, gari lao aina ya Volkswagon Kombi liligonga mti maeneo kona ya Kigogo na Msimbazi Mission.
Baadhi ya wanamuziki waliumia sana na gari lao, likawa halifai kabisa.
Wapigaji walioumia walikuwa ni Hamisi Mashala – Drummer Boy - alivunjika mguu, Mohamed Bakari Churchil aliumia kichwani na kushonwa nyuzi kadhaa, na pia Ayoub Iddi Dhahabu na Maarifa Ramadhani walipata maumivu makali kwa ndani mwilini.

Bendi ilisimamisha maonyesho yake kwa muda hadi  wanamuziki wake walipopata nafuu na kuanza maonyesho tena. Hali ya ajali ile ilileta fikra mbaya kwa wanamuziki hao na wapenzi wao na ilionekana kana kwamba kulikuwa na mkono wa mtu katika ajali ile.  Juma Mrisho ‘Ngulimba’ alitunga wimbo ‘Nimekosa Nini Jama’, wimbo ulioelezea kadhia hiyo. Katika kipindi hiki dhana ya ushirikina ilitawala sana katika bendi mbalimbali. Vifo vya wanamuziki mara nyingi vilihusishwa na upinzani katika bendi. 
Kufikia miaka ya ‘80’ kati bendi ya Urafiki ikawa inasua sua kutokana na uchakavu wa vyombo na Menejimenti iliyokuwepo wakati huo haikuwa tayari kutoa pesa kununulia vyombo vipya. Bendi ya Urafiki ilifikia tamati katika miaka ya ‘80’ kati kati na bendi hiyo ikatoweka katika anga za muziki na kubaki historia.

No comments:

Post a Comment