Wednesday, December 4, 2013

MOKOLO NA KOKUFA ULITUNGWA NA NANI?



Kuna kitendawili kikubwa cha nani alitunga wimbo wa Mokolo Nakokufa  kuna wanosema ni wimbo uliotungwa na  Wendo Kolosay maarufu kama Papa Wendo na aliuimba mwaka 1966  kwenye msiba wa Paul Mwanga kule Kongo Brazzaville, na aliyempigia gitaa alikuwa HonorĂ© Liengo. Rochereau  alikuweko siku hiyo na akamkaribisha Mzee Wendo auimbe wimbo huo na African Fiesta National. Kwa kuwa Wendo alikuwa na matatizo ya fedha wakati huo akakubali haraka, na Rochereau akamuahidi Wendo kuwa atampa haki zake zote za utunzi, hatimae Rochereau akaurekodi wimbo huo kwa jina lake na arrangement yake, hili ni jambo ambalo hujitokeza mara nyingi katika bendi za Afrika ambapo kiongozi huweka jina lake katika tungo zilizorekodiwa. Wendo aliendelea kuweko katika kundi la Africana Fiesta National kwa miaka miwili mpaka pale lilipotokea kasheshe Brussels Ubelgiji  baada ya bendi kuwa huko kwa mualiko wa ubalozi wa Kongo na bendi kutapeliwa malipo ya safari hiyo, Rochereau akawaacha wanamuziki wengine huko wasijue la kufanya moja wapo alikuwa Mzee Wendo, na ndipo Wendo akaiacha bendi hiyo na  akajiunga na mwanamuziki mwingine maarufu Dewayon.Mpaka mwaka 1990 alipokuwa akiulizwa ni utunzi wake gani alioupenda kuliko wote, Mzee Wendo daima alikuwa akisema Mokolo  Nakokufa.
Sam Mangwana alikuwa mmoja ya wanamuziki waliokuweko African Fiesta National wakati Wendo alipokuja kujiunga na kundi hilo, nae alipourekodi wimbo huu tena aliandika mtunzi ni Wendo kolosay.  Unaweza kuusikiliza wimbo huu version ya Sam Mangwana na maelezo ya ziada kupitia link hii http://www.rdctube.com/mokolo-nakokufa-minha-angola-sam-mangwana/

Huyu Wendo Kolosoy ni nani?

Antoine Wendo Kolosoy (alizaliwa tarehe 25 Aprili mwaka 1925 na kufariki July 28 mwaka 2008).  Wendo alizaliwa wilaya ya Mai-Ndombe magharibi ya Kongo. Alipofikisha umri wa miaka saba baba yake alifariki na muda mfupi baadae mama yake ambaye nae alikuwa muimbaji akafariki pia, hivyo Wendo akapelekwa kuishi katika kituo cha watoto yatima kilichokuwa kikiendeshwa na Society of the Missionaries of Africa. Akiwa na umri wa miaka 11 akaanza kupiga gitaa, lakini alipofikisha umri wa miaka 12/13 akafukuzwa katika kituo hicho kutokana na kutunga nyimbo ambazo hazikuwapendeza wafadhili wake akaanza kupiga muziki wa kuburudisha wasafiri katika pantoni  zilizokuwa zikifanya kazi katika Mto Kongo.  Pamoja na kuwa alibatizwa kwa jina la Antoine Kalosoyi, alipewa jina la Wendo kutokana na jina la mmoja wa watawala wa Uingereza aliyeitwa Duke of Windsor, hilo Windsor lilianza kubadilika na kuwa Wendo Sor na hatimae Wendo peke yake kubakia. Na katika utu uzima wake alikuja kuitwa Papa Wendo. Kwenye mwaka 1941 alianza kupiga muziki katika jiji la Leopordville (Kinshasa) akiwa na bendi yake ya Victoria Bakolo Miziki na wakati huo akakutana mmoja ya wale ndugu wawili wa Kigiriki walioanzisha record label ya kwanza Kongo, Nicolas Jeronimidis na kukubaliana kutoa nyimbo zake chini ya label ya Ngoma. Mwaka 1948 akiwa na mpiga gitaa Henri Bowane walifyatua kibao ambacho kiliweza kupata umaarufu hata nje ya Kongo, kibao hicho  kiliitwa Marie-Louise, kibao hiki kilipendwa sana katika nchi za Afrika Magharibi. Wendo aliendelea kuimba nyimbo nyingi kwa lugha mbalimbali ikiwemo Kiswahili.  Kwa kipindi kirefu sana Wendo alipotea katika ulimwengu wa  muziki japo kwa muda alikuweko African Fiesta National akiwa na Tabu Ley na Sam Mangwana. 

Baada ya Laurent Kabila na baadae mwanae Joseph Kabila kushika madaraka Kongo walimsaidia  mzee huyu kuanza kurekodi tena na kuanza kufanya maonyesho. Nilibahatika kukutana nae Ivory Coast mwaka 1998 wakati wa tamasha la MASA Cultural Festival akiwa na kundi lake alilokuwa bado akiliita Victoria Bakolo Miziki. Onyesho lake la mwisho alilifanya mwaka 2004 na hatimae kufariki 2008.






3 comments:

  1. Mwanamuziki wa mkongwe wa Kongo Mzee Mose Fan Fan aliposti maneno haya kwenye Facebook kuhusu hili alisema... Wimbo "mokolo na ko kufa" ulitungwa na Faugus Izeyidi yeye alikuwa mi solo guitarist katika bendi pia mdongo wake Roger Izeyidi, Rochereau alitengeza na kufania arregement pia ka yimba katika record na concert.

    ReplyDelete
  2. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  3. Kuna maelezo mengine kama haya kuhusu wimbo huo......kutoka http://www.mbokamosika.com/article-c-est-sam-mangwana-qui-fut-a-l-origine-de-mokolo-na-kokufa-selon-jessy-d-120913963.html....

    Thus the guistariste can create an instrumental tone that can give inspiration to the singer
    compose a song , a song composed can also give an inspiration to
    particular rhythm . Now back to the song " MOKOLO NAKOKUFA ."

    To me, this song has gone through some steps, and multiple entries before reaching its fin.Officiellement speaking , the story begins with Faugus through others, to finish with Tabu Ley.

    ReplyDelete