Saturday, November 30, 2013

HABARI ZILIZOTUFIKIA.......TABU LEY ROCHEREAU HATUNAE TENA


Akiwa na Mavatiku, mwenye gitaa


Msikilize hapa akiimba kuhusu siku ya kifo chake.....MOKOLO NA KOKUFA
Tabu Ley Rochereau alizaliwa  tarehe 13 Novemba, mwaka 1940. Tabu Ley alizaliwa jimbo la Bandundu katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo. Mwaka 1954 alipokuwa na umri wa miaka 14 tu alitunga wimbo wake wa kwanza Bessama Muchacha ambao alirekodi na African Jazz, bendi ya Joseph Kabasele (Baba wa muziki wa Kongo). Alipomaliza tu shule akajiunga na bendi hiyo kama mwanamuziki na kushiriki kuimba wimbo wa Indepence Cha Cha,(wimbo uliotungwa na Joseph Kabasele 'Grand Kalle') wakati wa sherehe za kupata uhuru kwa Kongo 1960. Akapata umaarufu mkubwa kuanzia hapo, na akakaa kwenye bendi hii mpaka mwaka 1963, ambapo yeye na Dr. Nico walipoanzisha kundi lao la African Fiesta. 1965 wawili hawa walitengana na Tabu Ley akaanzisha African Fiesta National, kundi ambalo pia lilijulikana kama African Fiesta Flash. Kundi hili lilikuja kuwa kati ya makundi bora yaliyowahi kufanikiwa kimuziki katika Afrika nzima, nyimbo kama Afrika Mokili Mobimba iliweza kuuza zaidi ya santuri milioni moja mwaka 1970. Bendi hiyo pia ilitoa wanamuziki waliokuja kutikisa ulimwengu wa muziki wa Afrika  kama vile Papa Wemba na Sam Mangwana.

Mwaka 1970 Tabu Ley alianzisha bendi aliyoiita Orchestra Afrisa International, jina hilo liliunganisha Africa na Editions Isa iliyokuwa record label yake, akapata jina Afrisa. Alirekodi nyimbo kama Sorozo, Kaful maya Aon aon na kujiweka katika kundi moja na TP OK Jazz kuwa kati ya bendi mbili bora Africa. Mwaka 1980 alimgundua mcheza show Mbilia Bel na kumfanya muimbaji na hivyo kukuza zaidi jina la bendi kwa vibao kama Nadina, Nakei Nairobi na kadhalika, na pia kumfanya Mbilia Bel kuwa mwanamke wa kwanza kupata umaarufu katika muziki wa soukus wa Kongo. Tabu Ley na Mbilia walikuja kuoana na kupata mtoto mmoja.

Mwaka 1988 Tabu Ley akampata mwanadada mwingine Faya Tess  na Mbilia akaacha bendi na kuanza kujitegemea. Baada ya hapo umaarufu wa bendi hizi ulianza kupungua baada ya wapenzi kuanza kupendelea zaidi soukus lililokuwa likipigwa na vijana ambalo lilikuwa likipigwa kwa mwendo kasi zaidi.

Tabu Ley alianza kutengeneza muziki kutafuta soko la kimataifa zaidi, na kupata umaarufu kwa album kama Muzina, Exi Ley na Babeti Soukus, mwaka 1996 alifanya kazi nzuri katika album ya Gombo Salsa aliyoifanya na kundi lile maarufu la Africando. Kwa muda mfupi Tabu Ley aliishi Marekani lakini akarudi Kongo mara baada ya kuangushwa kwa Mobutu Sese Seko 1997. Na akapata nafasi katika baraza la mawaziri la Laurent Kabila. Baada ya kifo cha Laurent Kabila,  Tabu Ley  alijiunga katika serikali ya mpito iliyoundwa na Joseph kabila. Novemba 2005 Tabu Ley aliteuliwa cheo cha Vice- Governor wa mambo ya utawala, siasa na ustawi wa jamii wa jiji la Kinshasa.

Habari zilizotufikia punde ni kuwa Tabu Ley ameaga dunia muda mfupi uliopita katika hospitali ya Mama Yemo kutokana na ugonjwa wa moyo , Mama Yemo ni hospitali kubwa mjini Kinshasa ambayo iliyopewa jina hilo lililokuwa jina la mama yake Mobutu Sese Seko. HABARI MPYA ZINASEMA TABU LEY AMEFIA UBELGIJI AMBAKO ALIKUWEKO KIPINDI KIREFU KUTOKANA NA HALI YAKE KUTOKUWA NZURI!!!!!!!!
Mungu amlaze pema Tabu Ley, aliyetupa raha maisha yetu yote kwa sauti yake tamu.
SOMA ZAIDI HAPA


No comments:

Post a Comment