Thursday, August 4, 2011

Andy Swebe na kunzishwa kwa Kilimanjaro Connection na African Stars


Kilimanjaro Connection awamu ya pili

Sunshine Band wakiwa Muscat
Adam Kinguti, kaka wa Ramadhan Kinguti maarufu kama Kinguti System, alirudi Dar es salaam na vyombo vipya vya muziki baada ya kutoka kutumikia katika ubalozi mmoja wapo wa  nje. Na hivyo wana muziki kadhaa wakaamu kuhama MK Group, wana Ngulupa na kwenda kuanzisha Bicco Stars. Mkutano wa kwanza wa wanamuziki wa MK wa kupanga kuhamia Bicco uliwahusisha Sidy Morris, Asia Darwesh, Andy Swebe, Mafumu Bilali , Joseph Mulenga, Green Simtowe na Deus Mgunda, lakini wengine walibadili mawazo na kubakia MK. Hapakuweko na sababu maalumu ya kuhama Ngulupa zaidi ya uamuzi wa kudhani Bicco kungekuwa kuzuri zaidi. Bicco ilikusanya wanamuziki kama  Asia Darwesh, Fresh Jumbe, Ramadhan Zahoro Bangwe, Aimala Mbutu, Ray Thomas, Seif Lengwe, Shomari Fabrice, Nyota Abdallah, Bob Ludala, Athumani Cholilo na pia Yahaya omari, kati ya kazi za kukumbukwa za bendi hii ilikuwa ni kufanya mradi wa nyimbo za Mzee Mwinamila, Bicco Stars walirekodi na Mzee Mwinamila.  Asia alipata vyombo vyake na  akaanzisha Zanzibar sound, Mafumu na Sidy, wakaondoka na  bendi hiyo na kuhamia Arusha. Andy alibaki na Bicco Stars lakini wakati wa safari moja ya kuzuru mikoa wito ukamjia kuwa kuna kazi imepatikana Japan chini ya uongozi wa Kanku Kelly, hivyo alilazimika kuhama bendi na kujiunga na wenzie katika Zanzibar Sound huko Arusha na kuanza mazoezi ya kazi ya Japan. Hapo ndipo Kilimanjaro Connection ilipozaliwa, ilikuwa ni bendi ya watu sita akiwemo Kanku Kelly(Trumpet), Asia Darwesh(Keyboards na kuimba), Buruhani Adinani(Guitar), Mafumu Bilali(Saxophone), Shomary Fabrice(Drums), na Andy Swebe(Bass), bendi ilikaa Japan miezi sita na baada ya hapo ikaenda Malasia, lakini Asia alijitoa katika bendi hii na kurudia bendi yake ya Zanzibar Sound. Hivyo katika safari ya Malasia bendi ilimuongeza ikiwa na Delfe Mulunga na Maneno Uvuruge. Andy na Mafumu wakiwa kulekule Malasia waliamua kuacha kikundi na waliporudi Dar es salaam walijiunga tena na Asia na kuendelea kupiga Bahari Beach Hotel, lakini muda si mrefu Zanzibar Sound ikapata kazi Bahrain, hivyo Andy na Mafumu wakabaki na kujiunga na  Bob Gadi, Shaft, Palmena Mahalu na wanamuziki wengine na kurudi tena kwa  Mkurugenzi wa MK Group Baraka Msilwa na kuanzisha bendi ya African Stars na kuendelea na mkataba Bahari Beach Hotel kwa miaka mitano, wakipiga mtindo wa Kipetapeta.
Mafumu Bombenga akawa amepata vyombo na wanamuziki wote wa kundi hili kasoro Bob Gadi wakahama bendi na kuanzisha kundi jingine na kuliita African Stars, jina hili lilileta ugomvi na uongozi wa bendi iliyopita, hivyo ikalazimika kubadili jina na kujiita African Beat Band, baadhi ya wanamuziki waliokuwemo walikuwa Amigolas, Mafumu Bilali, Andy Swebe na Buruhani Adinani bendi ikahamia Arusha na kukaa huko mwaka mzima. Karibu Bendi hii nzima tena ikahama na ikarudi tena chini ya Baraka Msilwa na kuanzisha kundi la African Revolution wakiwa na mtindo wa Chumvichumvi.  Bendi ilianza kazi Arusha ikaongeza wanamuziki kama  Deo Mwanambilimbi, Yuda, Baraka Rajab, Oscar Haule, Cadet Bongoman, Deo Mwamba, na Petit Makambo. Delfin Mulunga akamwita Andy wakaenda Muscat kwa mkataba wa miezi sita, kule ikaundwa bendi ya Estetica Musica. Baada ya kurudi nchini Andy akawa hana bendi akipiga katika recording nyimbo kama  Siwema, Siri yangu za JD, nyimbo mbalimbali za Cosmas Chidumule na wanamuziki wengine wengi. Baada ya hapo wakiwa na Maneno Uvuruge wakaanzisha bendi ya kupiga muziki wa jazz tupu na hivyo kuanzisha bendi inaitwa Almasi Band, bendi ilianza kupendwa sana. Kundi zima likapata mkataba wa kwenda Muscat kufungua Seeb International Hotel, band iliporudi Dar ikakuta vyombo vimeuzwa ukawa mwisho wa Almasi Band. Kwa sasa Andy alieanza na bass la nyuzi nne, akahamia bezi la nyuzi 5, anajifunza bezi la nyuzi 6.

No comments:

Post a Comment