Monday, October 11, 2010

Matangazo ya Magazeti


Matangazo ya bendi za muziki zamani yalikuwa na vituko vyake katika upangaji na pia maelezo yake. Magazeti maarufu kwa matangazo yalikuwa ni Uhuru ambalo lilikuwa gazeti la kila siku na magazeti ya kila wiki kama Mzalendo, Mfanyakazi, Heko na kadhalika. Pichani  ni matangazo ya Bendi ya OSS wakati huo wakiwa na mtindo wa Masantula Ngoma ya Mpwita, kama  tangazo linavyoonyesha kikosi hicho kilikuwa na Ngalula na Frida wakiwa kwenye kucheza show, Mottoo mpiga tumba, King Kiki kwenye uimbaji, Otrishi mpiga rhythm, Kalala Mbwebwe na Kabeya Badu waimbaji, Hatibu Iteytey katika kupuliza saxophone. Pembeni kuna tangazo la Kyauri Voice wakiwa na mtindo wa Katakata mwendo wa jongoo, wanamuziki wakiwemo Mbwana Cocks kwenye gitaa, na Belela Kabaa kwenye bezi. Vijana Jazz watoto wa nyumbani, hapa tunawaona Hassan Shaw kwenye kinanda. Hili jina ‘Watoto wa nyumbani’ lilikuja kutokana na kuweko na ushindani mkubwa kati ya bendi za kikongo wakati huo na zile zenye wanamuziki waKitanzania watupu, kama unakumbuka Vijana Jazz walitunga hata wimbo kuwananga wenzao waliokuwa wakijichubua na kusuka nywele ……oo ni mwanaume gani anapaka wanja, naomba ujirekebishe, ohh ni mwanaume gani anasuka nywele, naomba ujirekebishe, oo ni mwanaume gani ana paka Ambi…... UDA Jazz na mtindo wa Bayankata , enzi za John Kijiko kwenye  solo, Chipembele(Bob Chipe) kwenye drums, Forty kwenye rhythm. Na Juwata Jazz wakikuletea Msondo ngoma Magoma Kitakita.

1 comment:

  1. Nakumbuka miaka hii nilikuwa bado sijafikia umri wa kwenda muziki, lakini nilipenda sana kusoma matangazo ya bendi mbali mbali katika magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Mfanyakazi. Wanamuziki wa enzi hizo na waliofuata baadae walikuwa na majina ya jukwaani ambayo aidha wao wenyewe au mashabiki wao waliyatumia kuonyesha umahiri wao katika muziki. Nakumbuka wanamuziki kama Kida Waziri ‘Stone Lady’, ‘Field Marshal’ Nguza Viking, ‘Supreme’ Ndala Kasheba, ‘Mkurugenzi wa Solo’ Batii Osenga (huyu pia alikuwa akijulikana kama Popolipo), ‘Dokta’ Said Mabera, Waziri Ali ‘Kissinger’, ‘Dokta’ Remmy Ongala, ‘El Nassir’ Skassy Kasambula, Jerry Nashon ‘Dudumizi’, dekula Kahanga ‘Vumbi’, Mulenga Kalonji ‘Vata’, Ilunga Banza ‘Mchafu’, Nduka Musingu ‘Malik Star’, Shaka Mswamili ‘SM’, ‘Bedui wa Solo’ Patrick Kamaley, ‘Jabali la Muziki’ Marijan Rajab, Athumani Momba ‘Sauti ya Chuma’, Adam Bakari ‘Sauti ya Zege’, Shaaban Athumani ‘Luxury’, Kinyamagoha ‘Expedito’ na wengineo wengi.

    ReplyDelete