Thursday, June 29, 2017

HATIMAE MWANAMUZIKI MKONGWE BROTHER ZENNO AZIKWA

MWANAMUZIKI  na mchambuzi wa muziki wa charanga maarufu kwa jina la Brother Zeno hatimae amezikwa na makaburi jirani na alipokuwa akiishi kule Mbagala Kibondemaji. Zerno ambaye alikuwa muimbaji mzuri atakumbukwa kwa kuwa mmoja wa waanzilishi wa bendi ya Dar es Salaam Jazz B, bendi iliyokuwa ikiongozwa na Patrick Balisidya, ambayo ilianza kufanikiwa kwa kasina kuanza kuwa tishio kwa Dar es Salaam Jazz Band A, chini ya Michael Enoch, bendi ikavunjwa na wanamuziki wengine wakaingizwa Dar Jazz A, lakini Patrick akakasirika na kutokomea , baadae akaja kuanzisha Afro 70 na kufanya mambo makubwa. Baadae Brother Zeno alijiunga na Shirika la Bima ya Taifa, na baada ya kujiunga kampuni hiyo ndie aliyetoa msukumo wa kuanzishwa kwa bendi katika shirika hilo, Bima Jazz Band na hivyo pia kupewa kazi ya kutafuta wanamuziki wa kujiunga na bendi hiyo na yeye mwenyewe kuwa kati ya wanamuziki waanzilishi wa kundi hilo lililokuja kujizolea umaarufu mkubwa. Kati ya wanamuziki wa kwanza katika bendi hiyo waliobaki hai sasa ni wawili tu baada ya kifo cha Zeno. 







Binti pekee wa marehemu akiwa na mumewe wakiweka shada la maua







Baadhi ya wanamuziki waliohudhuria mazishi ya Brother Zeno


Aliyekaa ni Abdallah Mbosanga mmoja ya wanamuziki wawili waliobaki hai wa bendi ya Bima Jazz band ya kwanza. Mwingine ni Duncan Ndumbalo

Tuesday, June 27, 2017

BROTHER ZENNO AFARIKI DUNIA

RIP Brother Zerno
Hakika siku za karibuni zimekuwa ngumu kwa wapenzi wa muziki wa zamani, mfululizo wa misiba na wanamuziki kuugua kumekuwa ni habari karibu kila siku. Mchambuzi mahiri wa muziki wa Charanga Zerno Andrew Lucas, aliyefahamika zaidi kwa jina Brother Zeno, amefariki dunia asubuhi leo katika hospitali ya Temeke,  Brother Zeno  aliyekuwa akishirikiana na 'Mzee wa Macharanga' Charles Hillary enzi hizo Radio One, alikuwa na ufahamu mkubwa wa muziki wa kutoka Cuba na hivyo kuwa mpenzi mkubwa wa watu waliopenda muziki huo. Brother Zeno amesumbuliwa karibu mwaka mzima na tatizo la moyo na katika siku zake za chache mwisho alikuwa akipumua kwa msaada wa mashine, alitegemewa angepata nafuu na kuhamishiwa Muhimbili kwa matibabu zaidi lakini Mungu amekuwa na mipango mingine.
Msiba wa Mzee utakuwa nyumbani kwake Mbagala Kibonde Maji na mazishi yatakuwa kesho 28/6/2017 saa kumi hukohuko Mbagala

Friday, June 23, 2017

SHAABAN DEDE ANAUMWA AMELAZWA MWAISELA NO 5

Mwanamuziki mkongwe Shaaban Dede 'Kamchape' amelazwa leo katika hospitali ya Muhimbili wadi ya Mwaisela No 5. Wapenzi wa muziki tumkumbuke katika swala zetu.

Monday, June 5, 2017

MWANAMUZIKI HALILA TONGOLANGA AFARIKI DUNIA

HALILA TONGOLANGA, mwanamuziki wa siku nyingi ambaye alikuwa amelazwa katika hospitali ya Muhimbili amefariki dunia usiku wa kuamkia leo. Halila alikuwa amesafirishwa kutokea Ndanda kuja Muhimbili akihisiwa kuwa na matatizo ya figo. Licha ya kuwa alifika Muhimbili juzi Ijumaa usiku, lakini alikuwa hakufanyiwa vipimo vyovyote vikubwa mpaka umauti unamkuta. Jana Jumapili ililazimika kuanza kufanya jitihada za kupata daktari ambaye angemshughulikia kwa karibu zaidi, na daktari alipatikana ambaye aliahidi angeanza kufwatilia swala lake leo asubuhi lakini mapenzi ya Mungu yalikuwa tofauti. Juzi nilipomuona alinambia kuwa ana mengi anataka kunambia, lakini moja aliloweza kunambia pale ni kuwa yeye anajihisi ana kansa, 'Nilimuuliza anajuaje hilo, kwa vile hajapimwa hakuwa na jibu"
Wengi tutamkumbuka Tongolanga kwa wimbo wake wa Kimakonde aliouimba kwa mara ya kwanza akiwa na Les Mwenge 'Kila Munu Ave Na Kwao"
 Mwili wa marehemu unategemewa kusafirishwa leo saa tano kuelekea kwao Newala. Habari zaidi  zitawafikia kupia hapa
Mungu amlaze Pema peponi Halila Tongolanga


Saturday, June 3, 2017

TONGOLANGA ANASUBIRI VIPIMO

Katibu Mtendaji wa BASATA mwenye kitenge akiwa na Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi, walipomtembelea Tongolanga asubuhi ya leo.
Halila Tongolanga kwa kweli anaumwa. Kwa maelezo ya mdogo wake, ni mwezi wa tatu sasa anaingia na kutoka hospitali mbalimbali. Mpaka jana alikuwa katika hospitali ya Ndanda, na kwa msaada wa Mbunge wa Tandahimba aliweza kupatiwa Ambulance na kufikishwa Muhimbili ambako amelazwa Kibasila No 10. Mpaka jioni ya leo alikuwa anasubiri vipimo.
Tongolanga ndie mtunzi na mwimbaji wa wimbo maarufu wa 'Kilamunu ave na kwao' aliouimba kwanza akiwa Les Mwenge bendi iliyo mali ya JWTZ.

Friday, April 28, 2017

SI KWELI KUWA HARRISON SATCHMO SIWALE ALIFIA GEREZANI,


Mar. Harrison Siwale-Satchmo

......................  SIKILIZA HAPA GUITAR LA MZEE SIWALE...................
 
Tarehe 8 September 2013, niliandika katika blog hii habari niliyoipa kichwa cha habari, Harrison Siwale aliishia wapi? Ni habari ya kusikitisha.

Niliandika hivi-----Nimetoka kuongea na Mzee mmoja ambaye nilimuomba anitafutie habari za Harrison Siwale  aka ‘Satchmo’, ambaye alikuwa mpiga rhythm mahiri na maarufu sana katika miaka ya sabini, Harrison alikuwa na staili ya pekee ya upigaji wa gitaa wa kudokoa nyuzi na kupata aina ya pekee ya mlio wa gitaa. Kati ya nyimbo ambazo upigaji huu unasikika ni katika nyimbo za Jamhuri Jazz Band kama vile Mganga 1  na 2, Blandina na kadhalika. Pamoja na bendi nyingine Harisson aliwahi kupigia Atomic na Jamhuri Jazz Band zote za Tanga, na kisha kuvuka mpaka na kuwa na makazi Mombasa kwa muda mrefu ambako aliendelea na muziki. Kwa kadri ya maelezo niliyopewa leo na huyu Mzee niliyemuomba anitafutie habari ili nijue yu wapi huyu mwanamuziki siku hizi? Haya ndio aliyonambia.



'Baada ya kufa kwa yale makundi ya Simba wa Nyika na Les Wanyika, Harrison Siwale alianza kupiga muziki wa Injili katika eneo la Kilifi. Akawemo katika kundi lililokuwa likifanya maonyesho yake katika miji mingi ikiwemo Mombasa na Nairobi. Umahiri wake wa kazi ukamfanya mwenye vyombo vya hilo kundi alilokuwemo Harrison kumuamini sana na kumuachia awe kiongozi wa kundi hilo na kuwa huru kuzunguka sehemu mbalimbali. Inasemekana Harrison akapata tamaa ya kuingia mitini na vyombo vile, hivyo ghafla akapotea. Taarifa zikamfikia mwenye vyombo kuwa vyombo vyake viko njiani kuvushwa kungia Tanzania kupitia mji wa Lungalunga. Mwenye vyombo akaweka mtego hapo na Harrison akakamatwa hapo akiwa na vyombo hivyo, kesi ilifika mahakamani na akahukumiwa kifungo cha miaka mitatu'. Baada ya hapa kuna hadithi mbili, moja ikisema alifia gerezani Shimo la Tewa, na nyingine ikisema alifariki baada ya kumaliza kifungo chake.

Je, nini hasa kilitokea? Najaribu kuwasiliana na watu mbalimbali kupata hadithi zaidi kuhusu mwanamuziki huyu.

HATIMAE (2017 APRIL).... Kwa bahati sana nimeweza kuanza kuwasiliana na mtoto wa Harrison Satchmo Siwale, ambae tuliweza kukutana kupitia facebook. Kijana huyu ambaye jina lake ni Salehe Siwale aliweza kunambia kuwa baba yake alimuoa mama yao na walizaliwa vijana wawili yeye na kaka yake.

Na niliweza kupata taarifa za ziada baada ya kuniunganisha na mama yake ambaye ndie alikuwa mke wa Mzee Siwale nikaweza kuongea nae mubashara kupitia video call ya whatsapp. Kwanza kabisa mama huyo ansema kuwa katika kipindi alichoishi na Mzee Siwale hakuwahi kufungwa wala kuzungumzia kuwa aliwahi kufungwa. Na Mzee Siwale alifariki katika Kitongoji cha Rongai  huko Nakuru na kuzikwa tarehe 31/3/2013. Ukiangalia kuwa taarifa ya awali niliyopewa ilikuwa katika miezi michache baada ya kifo chake, niwazi si kweli kuwa alifia Gerezani na kama angekuwa aliwahi kufungwa hakika mkewe angekuwa anajua.

Mungu Amlaze Pema Mchungaji Harrison ‘Satchmo’ Siwale








Saturday, April 22, 2017

KIFO CHA SOKOINE KILIIKUTA ORCHESTRA MAMBO BADO IKO SHINYANGA


Mwaka 1984 nilikuwa mwanamuziki wa bendi ya Orchestra Mambo Bado, bendi iliyokuwa inaongozwa na Tchimanga Kalala Assossa. Bendi ilikuwa ni moja ya bendi zilizokuwa pendwa wakati huo, mtindo wa bendi ulikuwa unajulikana kama Bomoa. Neno hili lilitokana na wimbo wa Bomoa Tutajenga Kesho, wimbo ambao  baadae kwa sababu ambazo mpaka leo sizijui, ulikuja kupigwa marufuku na Umoja wa Vijana wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati ule, usisike kwenye radio ya Taifa, redio ambao ilikuwa pekee wakati huo. Orchestra Mambo Bado ilikuwa na watu ishirini hivi, Tchimanga Assossa kiongozi na mwimbaji. George Mzee muimbaji, Lucas Faustin muimbaji, Jenipher Ndesile muimbaji, Banza Tax muimbaji, Athumani Cholilo muimbaji, John Kitime muimbaji, Likisi Matola mpiga gitaa la bezi, Andre Milongo akipiga gitaa la second solo, Huluka Uvuruge na Kazembe wa Kazembe wapiga gitaa la solo, William Maselenge akiwa kwenye gitaa la rhythm. Kulikuweko na wacheza show wanne, mafundi mitambo watatu na mweka hazina mmoja na meneja wa bendi. Masikani ya bendi yalikuwa katika ukumbi wa Lango la Chuma, Mabibo Dar es Salaam
Tarehe 12 April 1984, kundi zima lilitua katika mji wa Shinyanga baada ya kuwasili hapo kwa treni kutokea Dar es Salaam. Kwa taratibu za miaka hiyo, pamoja na ratiba ya ziara ya bendi kutangazwa kwenye gazeti la Uhuru, meneja wa bendi alikuwa akilazimika kutangulia mji ambao dansi litapigwa kuwahi kufanya mikataba na kumbi  ambazo dansi lingepigwa na pia kufuatilia vibali mbalimbali vya kuruhusu onyesho kufanyika. Mawasiliano yalikuwa magumu na urasimu ulikuwa mkubwa. Haikuwa kazi rahisi maana miaka hiyo ili bendi isafiri ililazimika kupata  kibali cha Afisa Utamaduni wa Mkoa ambao ni masikani ya bendi kuruhusu bendi kutoka nje ya Mkoa na kisha kibali hicho kupelekwa kwa Ofisa Utamaduni wa Mkoa ambao bendi inakwenda, nae baada ya kuruhusu bendi kuingia mkoani kwake, unaomba kibali cha Afisa Utamaduni wa Wilaya unakotaka kupiga muziki ili nae akuruhusu kufanya onyesho kwenye wilaya yake. Baada ya hapo meneja hutafuta na mtu ambaye ana spika ya mkononi, megaphone kuikodisha na kisha kutafuta mtu wa kutangaza onyesho. Ili kubana matumizi kuna mara nyingine wanamuziki wenyewe ililazimika wapite mtaani na spika hiyo kujitangaza. Kulikuwa na mji kama Mpanda wakati huo, ambapo mtangazaji hakuwa na megaphone, mtu maalumu alipita mtaa kwa mtaa akiwa na ngoma ambao aliipiga watu wakikusanyika basi anatangaza ujio wa bendi katika mji wao.
Tarehe 12 April 1984, Orchestra Mambo Bado iliwasili Shinyanga kwa treni ikitokea Dar es Salaam, kuanza ziara ya Kanda ya Ziwa. Wanamuziki tulionyeshwa vyumba vya kulala, mambo yalionekana kuwa yatakuwa mazuri kwa siku ile, matangazo yalikuwa yamebandikwa kwenye nguzo za umeme sehemu mbalimbali za mji, na hali ya kuonyesha kuwa watu walikuwa na taarifa ya ujio wetu ilikuwa dhahiri. Ilikuwa ni muda wa saa kumi hivi ilipotangazwa kuwa nchi imepata msiba mkubwa sana. Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine amefariki katika ajali ya gari jirani na Morogoro. Kwanza ilikuwa ni mshtuko, halafu akili ilipotulia tulijua kuwa na sisi kama bendi tunaingia kwenye tatizo kubwa sana, tulikuwa na nauli ya kuja tu mpaka Shinyanga, na fedha ya kula ya siku moja tulikuwa tunategemea kupiga dansi ili kuweza kulipa malazi ya siku hiyo na kupata fedha ya kula na kuendelea na safari kesho yake, tukitegemea mapato mengine makubwa katika maonyesho ya Mwanza wikiendi iliyokuwa inafuata. Hayo yote tulijua sasa yameharibika, tulirudisha vyumba vyote mara moja na kubaki na viwili tu kimoja kikiwa cha wasichana waliokuwa kwenye bendi, wengine wote ikalazimu tuhamishie mizigo yetu chumba kingine. Baadae tulikaa na Afisa Utamaduni kutafakari kama dansi lingeweza kulia siku ile, na kama halitalia nini hatima ya watu hawa 20 wageni kutoka Dar es Salaam? Kama kiasi cha saa moja jioni, Afisa Utamaduni akaruhusu tupige dansi ili tuweze kupata nauli ya kurudi Dar es Salaam, kwani ilijulikana wazi kitaanza kipindi cha maombolezo ambacho hakuna mtu alijua kitaisha lini,  hivyo hakukuwa na sababu ya kuendelea na safari kutoka hapo. Vipindi vya maombolezo huwa ni vipindi ambavyo pamoja na mambo mengine shughuli za muziki husimamishwa. Kwa wanamuziki na wale wanaotegemea shughuli za muziki na familia zao, kipindi hiki huwa kigumu sana. Lakini kinaleta ukakasi akilini kwani shughuli za kupiga muziki kwenye kumbi husimamishwa, madisco hufungwa na vikundi vya muziki haviruhusiwi kufanya  kazi lakini radio huendelea kupiga muziki uleule ambao umezuiwa kwenye kumbi, sehemu za starehe kama baa huendelea kupiga muziki na kufanya biashara zao bila tatizo ila wanamuziki ndio huzuiwa kufanya shughuli zao kwa maelezo kuwa ni kipindi cha maombolezo. Nakumbuka sana misiba  mikubwa ya viongozi wetu ukiwemo wa Baba wa Taifa kwa sababu kubwa mbili, kwanza uchungu wa kupoteza kiongozi wetu na njaa iliyofuatia baada ya hapo.

Saturday, March 18, 2017

AMRI BILA TAFITI ZINAATHIRI SANA SEKTA YA MUZIKI


KATIKA shughuli ambazo watu wengi huona ni rahisi kuendesha na kutoa maamuzi bila utafiti ni soka na muziki. Ukisikiliza mazungumzo baada ya mechi za soka ndipo utakaposikia watu wanavyotoa ushauri au kukosoa wachezaji, kocha refa, chama cha mpira wa miguu, hakika ingewezekana watu hawa wakapata mamlaka, maamuzi yangekuwa ya ajabu sana.
Hali kadhalika kwenye muziki. Kwa mfano ukiuliza,   kwanini muziki wa bendi hauna umaarufu kama zamani? Hakika ukipita kila mtaa utapata majibu, wengine watakwambia kosa la vyombo vya utangazaji , wengine watakwambia wanamuziki wenyewe , wengine watakwambia serikali, na pia utapewa maelekezo mbalimbali ya nini kifanyike. Bahati nzuri majibu haya ya mtaani hayana madhara kwani huishia hapo hapo. Lakini bahati mbaya huja pale ambapo viongozi wenye mamlaka nao hugeuka wataalamu wa muziki na wao kutoa maamuzi kadri ya mtizamo wao, lakini maamuzi yao huwa amri, na amri inapotolewa bila utafiti wa kutosha madhara yake yanaweza kuendelea miaka mingi baadae. Ninaloweza kusema kwa uhakika, ni kuwa muziki wa Tanzania leo ungekuwa katika nafasi ya juu zaidi duniani kama isingekuwa maamuzi ambayo yalitolewa bila utafiti miaka ya nyuma. Labda nitoe mifano kadhaa. Mpaka miaka ya 70, wanamuziki wa Tanzania walikuwa wakienda sambamba na wanamuziki wa nchi nyingine nyingi Afrika, licha ya kutokuwa na miundo mbinu muhimu katika maendeleo ya muziki kama vile kutokuwa na kampuni za kurekodi na kutengeneza santuri. Lakini kimuziki, wanamuziki wa kipindi hiki walikuwa bega kwa bega na wenzao ambao walikuwa na miundo mbinu stahiki. Tanzania tulikuwa na bendi ambazo zilikuwa  zinapiga muziki wa rumba, nyimbo nyingi za wakati huo mpaka leo bado zinasifika na kupendwa katika anga za muziki. Pia tulikuwa  na wanamuziki vijana ambao wengi wao walikuwa mashuleni, hawa wakiwa na mtizamo mpana zaidi wa kutambulika duniani, wanamuziki hawa kama ilivyokuwa sehemu nyingi Afrika walianza kupiga muziki uliojulikana kama Afro Rock, muziki ambao ulichanganya mahadhi ya muziki asili wa Kitanzania na mapigo ya kizungu, wakifuatia nyayo za kundi la Osibisa, na wanamuziki kama Ransome Fela Kuti. Kukawa na makundi kama Afro 70, Trippers, Sun Burst, The Jets na kadhalika kwa kuyataja machache, makundi ambayo yalianza kuingiza muziki wa Tanzania kwenye soko kubwa zaidi la Kimataifa, kwa mfano wimbo wa Weekend wa Afro70 uliingia kwenye Top Ten Nigeria miaka hiyo, wakati huo muziki wa Nigeria haukuwa na umaarufu wowote nchini kwetu.  Kwa kuwa vijana hawa wengi walikuwa bado shuleni, na kufuatana na maadili ya wakati ule, wanafunzi hawakuruhusiwa  kushiriki madansa ya usiku, hivyo basi kulikuweko na utamaduni wa madansa ya mchana yaliyoitwa Bugi. Hapo vijana walikusanyika kupiga muziki wao kila mwisho wa wiki, shughuli zikianza saa nane mchana na kuisha saa kumi na mbili jioni. Lakini siku moja kiongozi mmoja akatokea na kupiga marufuku Bugi, hivyo kuwaondoa wanamuziki vijana wengi kwenye muziki kwani wasingeruhusiwa kushiriki madansi ya usiku.  Wakati vijana hao wanaacha muziki, vijana wengine Afrika waliendelea mbele. Hata majirani zetu Kenya na Zambia wakawa na wanamuziki wengi walioweza kuingia katika soko la Kimataifa, wanamuziki wetu walikosa fursa hiyo. Pengo hili linaendelea kuwepo mpaka leo. Kuziba pengo hilo kunahitaji kutafiti tulipojikwaa na kuangalia tunafanya nini kurekebisha hali iliyopo. Swala la kupiga marufuku kazi za muziki si jambo geni katika historia ya muziki, kulikuwa na maamuzi kadhaa ya kisiasa pia ambayo pia hayakuwa na utafiti hivyo kudhoofisha maendeleo ya muziki Tanzania. Kwa mfano kulishawahi kutolewa amri ya kupiga marufuku wacheza show, wakati huo karibu bendi zote kubwa za muziki wa rumba kote Afrika Mashariki na Kati zilihakikisha kuwa zinakuwa na kundi la wacheza show, na waimbaji maarufu kama Mbilia Bel na Tshala Mwana wote awali walikuwa ni wacheza show. Kwa kipindi kirefu kulikuweko na sinto fahamu ya wacheza show na ikalazimika taaluma hiyo irudi kinyemela kwani makundi yote ya muziki kutoka nje yalipokuja nchini yalisindikizana na wacheza show. Nyimbo kadhaa ziliwahi kupigwa marufuku na hatimae kuja kuonekana ni za muhimu katika jamii, ukiwemo wimbo maarufu wa Super Matimila, Mambo kwa Soksi, ambao ulipigwa marufuku na baade kuonekana ni wimbo muhimu kuhamasisha watu kutumia kinga katika zama hizi za balaa la Ukimwi. Upigaji marufuku wa tungo unakwaza watunzi na kuishia kutunga nyimbo nyepesi ambazo zina uhakika wa kutokupigwa marufuku. Katika miaka ya karibuni kumewahi kufanyika maamuzi kadhaa yasiyokuwa na utafiti kwa mfano,  serikali iliwahi kununua mashine iliyoitwa Mastering Mixer kwa gharama ya shilingi milioni 50, kwa maelezo kuwa ndio itakayowezesha kumaliza wizi wa kazi za muziki. Sio siri wizi uko palepale. Hayo yalikuwa maamuzi bila utafiti, ni vizuri kujua hiyo ‘mixer’  iko wapi ili kutathmini ni matokeo ya uamuzi huu uliogharimiwa na serikali. Uamuzi mwingine ulikuwa ni ule wa kutunga sheria ya kuweka stempu za TRA kwenye kazi za sanaa, kwa maelezo kuwa utamaliza wizi wa kazi za muziki na filamu. Si mara moja taarifa imatolewa kuwa serikali ilitoa milioni 20 kwa mtafiti toka ‘Chuo Kikuu’ kuhakiki kuwa njia hiyo ndio itamaliza wizi wa kazi za sanaa, hakuna ‘mtafiti’ anayejitokeza kuwa alipokea fedha na kufanya utafiti huo, wala hakuna nakala ya utafiti huo, ni aina nyingine ya maamuzi bila utafiti na matokeo yake wizi wa kazi za sanaa umeenea kila kona nchini na mauzo halali ya kazi za muziki yamepotea. Ushauri tu kwa viongozi kuwa muziki si shughuli ya kubahatisha ina misingi yake, ni muhimu kwa manufaa ya Taifa, umefika wakati wa kufanya utafiti kwanza kabla ya kutoa maamuzi.

Tuesday, January 31, 2017

URAFIKI JAZZ BAND

Mzee Juma Mrisho aka Ngulimba wa Ngulimba liyekuwa Kiongozi wa Urafiki Jazz Band

Pichani toka kushoto waliosimama-Hamis Nguru-mwimbaji, Marifa Ramadhani-Tumba, Juma Saidi- Maracas, Abas Lulela-Bass, Abasi Said -Saxophone, Fida Said-Saxophone, Mohamed Bakari (Churchill)-rythm, Juma Mrisho(Ngulimba wa Ngulimba)-Mwimbaji na Kiongozi wa Bendi.Waliokaa Michael Vicent-Solo gitaa, Ezekiel Mazando-Rythm, Juma Ramadhani Lidenge-second solo na Ayub Iddi- Bass
Bendi ya Urafiki (Urafiki Jazz Band), ilianzishwa mwaka 1970 na kiwanda cha nguo cha Urafiki kilichopo Ubungo. Jina rasmi la kiwanda lilikuwa ni FRIENDSHIP TEXTILE MILL. Kiwanda kilijengwa kwa msaada wa watu wa Jamhuri ya China na kwa urafiki huo kilipewa jina la Friendship Textile. Bendi ilianzishwa ili kutangaza bidhaa hasa Khanga na Vitenge za kiwanda hiki kwani wakati huo kulikuwa na viwanda vingine kadhaa vya nguo nchini kama vile Mwatex, Mutex, Kilitex, na kadhalika


Meneja Mkuu wa kiwanda cha Urafiki Bw. Joseph Rwegasira aliubariki mpango huo wa kuanzishwa bendi ya dansi ya kiwanda na hivyo aliidhinisha malipo ya hundi ya Shs. 50,000/= kununulia seti ya vyombo vya muziki kutoka katika duka la Dar Es Salaam Music House ambalo mpaka leo lipo katika mtaa wa Samora Avenue – Dar Es Salaam.

Ili kupata kundi lililo bora, Menejimenti ya kiwanda cha Nguo cha Urafiki ilimuajiri Juma Mrisho Feruzi maarufu kwa jina la Ngulimba wa Ngulimba na kumuagiza atafute wapigaji kutoka popote ili kuunda kundi imara.. Katika kuhakikisha bendi hiyo mpya inasimama, Ngulimba alichukua wapigaji watano kutoka Orchestre African Qwillado, bendi ambayo aliipigia kabla ya kuanza Urafiki. Na hii ndio maana nyimbo za mwanzoni za Urafiki Jazz Band zilionekana kama zina mahadhi ya Orch. Qwillado.

Wanamuziki aliowachukua Ngulimba kutoka Orch. Qwillado walikuwa ni Michael Vincent Semgumi, mpiga gitaa la Solo, Ayoub Iddi Dhahabu – Besi, Abassi Saidi Nyanga – Tenor Saxophone na Fida Saidi, Alto Saxophone. Ngulimba yeye akawa Muimbaji na pia Kiongozi wa Bendi.

Wanamuziki wengine wa mwanzo ambao waliungana na hao watano waliotoka Orch. Qwillado ambao tayari walikwisha ajiriwa kiwandani Urafiki, walikuwa – Juma Ramadhani Lidenge – Second Solo, Mohamed Bakari Churchil – gitaa la kati (rhythm), Ezekiel Mazanda – rhythm, Abassi Lulela – Besi, Hamisi Nguru – Muimbaji, Mussa Kitumbo – Muimbaji, Cleaver Ulanda – Muimbaji, Maarifa Ramadhani – Tumba, Juma Saidi – Manyanga (maraccass) na Hamisi Mashala – mpiga drums.

Mtindo walioanza nao Urafiki ulijulikana ‘Mchaka Mchaka’ na baadae ukabadilika na kuwa ‘Chaka Chua’ na hatimae mwisho mwisho bendi inaelekea ukingoni walipiga mtindo wa ‘Pasua’ na ‘Patashika’

Mwaka 1971 Gidion Banda, mwanamuziki kutoka bendi ya Morogoro Jazz alijiunga na kundi akiwa mpigaji wa Saxophone.

Aidha, Bendi ya Urafiki ilipitiwa na wanamuziki wengi baadhi wakiwemo Gideon Banda mpuliza saxophone kutoka Morogoro Jazz wengine wakiwemo Thobias Cosmas Chidumule na Frank Mahulu – Waimbaji waliotokea Western Jazz (Saboso) mwaka 1973 na kuongeza nguvu katika safu ya uimbaji. Waimbaji hao walishiriki nyimbo nyingi baadhi zikiwa Tausi Karuka, Jembe na Panga (Geza Ulole), Kosa la Nani, Mauaji ya Soweto, Rukia Hukusikia, Maonyesho ya Mtu Mweusi n.k.

Pia waliongezeka Mkali na Hidaya kutoka Morogoro wakipuliza matarumbeta, hao walikuja 1973 na Ali Saidi alietokea Cuban Marimba akipiga gitaa la kati (rhythm) na baadae mwaka 1975, Mganga Hemedi kutoka Tanga, akitokea Atomic Jazz, nae alijiunga na kuwa upande wa solo na rhythm.

Urafiki Jazz imetunga nyimbo nyingi, zaidi ya mia tatu zinazoelekeza kwenye siasa, mapenzi, nasaha na mafundisho na pia kukosoa. Baadhi ya nyimbo zake za siasa zilizopata umaarufu ni kama zile Mwenyekiti Nyerere, Mauaji ya Soweto, Jembe na Panga n.k..

Mwaka 1975 Bendi ilishiriki katika mashindano ya bendi za muziki wa dansi yaliyofanyika Mnazi Mmoja – D’Salaam na kushika nafasi ya tatu na Mzee Ngulimba, kama Kiongozi wa Urafiki aliiwakilisha Tanzania pamoja na bendi ya Afro 70 iliyopata nafasi ya kwanza na baadhi ya vikundi vya utamaduni kutoka Tanzania Bara na Zanzibar nchini Nigeria katika maonyesho ya mtu mweusi yaliyofanyika huko.

Saturday, November 12, 2016

RAJABU OMARY KUNGUBAYA APATA MGUU WA BANDIA KUTOKA KWA WAPENZI WA MUZIKI WA ZAMANI


Marehemu Omary Kungubaya
Rajabu Kungubaya
Rajabu Omary Kungubaya, mtoto wa marehemu Omary Kungubaya, mwanamuziki ambaye alipata umaarufu kutokana na wimbo wake wa ‘ Salamu za wagonjwa’ uliokuwa wimbo wa kufungua na kufunga kipindi cha salamu za wagonjwa kilichokuwa kikirushwa na Radio Tanzania, leo amepokea mguu wa bandia ili kumsaidia kutokana na mguu wake wa kulia kuwa umekatwa kutokana na ajali ya bodaboda. Wanamuziki John Kitime na Mjusi Shemboza walimuona Rajabu kwa mara ya kwanza siku walipoenda kumzika Mzee Kungubaya na kuona umuhimu wa kumsaidia Rajabu kutokana na  hali yake ya kutegemea magongo wakati wa kutembea. Kwa kutumia kundi a Whatsapp la ZAMA ZILE, (kundi la wapenzi wa muziki wa zamani wanaosikiliza kipindi cha ZAMA ZILE kinachoendeshwa na John Kitime kupitia EFM 93.7fm kila Jumapili kuanzia saa 2-5 usiku), wanakikundi waliweza kuchanga fedha zilizowezesha kijana huyu kupata mguu wa bandia.
 Rajabu ni mchangamfu anaeonekana kupendwa na kila mtu, kutokana na majirani zake wote kumuunga mkono ikiwemo serikali ya mtaa wake. Mwenyekiti wa serikali ya mtaa akiwa na wajumbe wengine wa serikali ya mtaa wake wote walimsifu kwa tabia yake ambayo walisema ilikuwa ni mfano hasa kwa jitihada zake za kutunza familia yake. Mke wa marehemu Mzee Kungubaya, ambaye ni mama mzazi wa Rajabu alisema yeye alikuwa anategemea kuishi kwa kufanya kazi za kibarua katika sehemu ambazo kuna ujenzi unaendelea, hufanya kazi kama kubeba maji na zege kuwasaidia wajenzi. Marehemu Kungubaya ameacha watoto wakiwemo wadogo ambao mmoja yuko shule ya chekechekea na mwingine darasa la 6, wote hawa wanamtegemea sasa kaka yao ambae ana mguu mmoja. Rajabu alikatika mguu kutokana na gari kuovertake na kumfuata upande wake na kumgonga wakati akiwa kwenye bodaboda, aliyemgonga, jina na namba ya simu ipo aliahidi kumsaidia lakini hajatimiza ahadi zake kwa kijaa huyu aliyempa ulemavu wa maisha.


Saturday, October 29, 2016

EXCLUSIVE- ANGALIA PAMBAMOTO LILIVYOKUWA LIKICHEZWA MIAKA YA 90 -VIDEO

VIJANA DAY kila Jumapili mchana Vijana Jazz Band walikuwa wakipiga katika ukumbi wa Vijana Social Hall Kinondoni na hii ilikuwa mojawapo ya raha ukumbini. Aina ya uchezaji hakika ni tofauti na leo.
 Jukwaani wapiga magitaa
Miraji Shakashia- solo
John Kitime- Rythm
Manitu Musa - Bass
Drums- Juma Choka
Sax Rashid Pembe na Said Mohamed Ndula
Trumpet- Mawazo Hunja na Tuba
Uimbaji
Jerry Nashon, Mohamed Gotagota, na Abdallah Mgonahazelu 

TOA MAONI

Friday, October 21, 2016

MAZISHI YA MZEE KUNGUBAYA

MWANAMUZIKI mkongwe ambaye alipata umaarufu kutokana na wimbo wake Salam za Wagonjwa amezikwa leo katika makaburi ya kifamilia Njeteni Kwembe. Msiba huo ulihudhuria na watu wengi wakiwemo majirani, ndugu, wanamuziki na wapenzi wa muziki wa Mzee Kungubaya.Tatu itakuwa siku ya Jumamosi 22/10/2016.
Jeneza likiwa nje ya nyumba ya marehemu

Mwanamuziki Mjusi Shemboza akiongea na mmoja wa watoto wa marehemu Mzee Kungubaya




Mjusi Shemboza akiwa na Mtendaji Mkuu wa COSOTA wa zamani Mzee Mtetewaunga

Msafara wa kuelekea makaburini



Mazishi ya Mzee Kungubaya

Thursday, October 20, 2016

BURIANI OMARY KUNGUBAYA

kungubaya
Mzee Omari Kungubaya akipiga gitaa siku ya mkesha wa msiba wa Dr. Remmy Ongala
MZEE Omari Kungubaya ambaye atakumbukwa kwa wimbo wake Salam za wagonjwa, wimbo uliokuwa ukiashiria kuanza na kuisha kwa kipindi cha salamu za wagonjwa kupitia Radio Tanzania kwa miaka mingi amefariki leo mchana baada ya afya yake kuwa si nzuri kwa muda mrefu. Msiba wake uko nyumbani kwake Njeteni, Mbezi ya Kimara Habari zaidi tutawaleteeni Mungu amlaze pema peponi