Friday, August 12, 2022

HAKIKA DANSI LIMEBADILIKA SANA

 


Kweli dansi limebadilika sana.

Kumbukumbu zangu huwa zinanirudisha Iringa nilipokuwa na umri wa miaka minne hivi. Nadhani ndipo nilipoanza kutambua kuwa wazazi wangu walikuwa wanajitayarisha kwenda dansini, nakumbuka wakituaga na kutumbuambia ‘Haya laleni sisi tunaenda dansini’. Moja ya dansi nakumbuka lilikuwa limepigwa na Cuban Marimba wakiongozwa na Salum Abdallah, nakumbuka kwa sababu kesho yake Mwalimu Nyerere alikuja kuhutubia kwenye uwanja ambapo upo sasa ni uwanja wa Samora. Wakati huo ulikuwa ni uwanja wa mpira wa shule ya Middle School na baba yangu alikuwa Headmaster wa shule ile, na nyumba yetu ilikuwa pembeni tu ya uwanja huo wa mpira.
Siku alipokuja kuhutubia Mwalimu Nyerere, wimbo uliokuwa ukisikika kwenye spika ukirudia rudia, ulikuwa wimbo wa Cuban Marimba na baadhi ya  maneno yake yalikuwa ‘ Tutie jembe mpini, twendeni tukalime’. Mama akatuambia na wadogo zangu kuwa wimbo huo walikuwa wameucheza jana yake dansini. Kwa kweli toka nikiwa mtoto, dansi kwangu ni neno la furaha  kwenye maisha yangu. Nikiwa mdogo  wazazi wangu walikuwa wakituonyesha namna ya kucheza aina mbalimbali za dansi, zikiwemo tap dancing, aina ya dansi ambayo viatu lazima uvigonge sakafuni wakati wa kucheza kufuatia mapigo ya muziki, wazazi walitufundisha kucheza  chacha, waltz na aina nyingine za dansi ambazo sijapata hata  kujua majina yake.
Nyakati hizo na miaka mingi baadae, mtu akiaga anakwenda dansini, jambo la muhimu atakalolifanya huko ni kucheza nyimbo nyingi kadri atavyoweza. Kesho yake mazungumzo kuhusu dansini ni kuulizana nyimbo ngapi zilichezesha. Mpenzi wa muziki kurudi nyumbani akiwa kachoka kwa kucheza ilikuwa ndio dalili ya kufurahia kwa usiku ule.

Miaka mingi baadae hatimae nikaja kuwa mwanamuziki wa muziki wa bendi,  aina ya muziki ambao miaka ya 80 ulianza kuitwa muziki wa dansi, ulipewa jina hili kuutofautisha na aina nyingine za muziki kama vile taarab,  kwaya, muziki wa asili na aina nyingine za muziki. Muziki huu wa dansi ulikuwa ni ule uliopigwa kwa vifaa vya kisasa na kutegemea kuwa lazima utachezwa, tena kwa mtindo maalumu.  
Katika miaka ya hamsini na mwanzoni mwa miaka ya sitini, bendi zilikuwa zikitangaza aina muziki itakaoupiga, kwa mfano kiongozi wa bendi aliweza kutoa maelezo yafuatayo kabla ya kupiga wimbo. ‘ Muziki ufuatao unaitwa Dada Adija, umepigwa katika mtindo wa Cha Cha’. Basi muziki ukianza wapenzi wa muziki huingia uwanjani na kuonyesha umahiri wao wa kucheza ChaCha. Na hivyo hivyo kama wimbo ni Twist, Bolelo, Charanga na kadhalika. 

Utunzi wa zamani

Utunzi wa nyimbo mpya za bendi ulikamilishwa kwa muungano wa mawazo kutoka kwa wanamuziki mbalimbali katika bendi. Mtunzi wa awali aliweza kuleta  mashahiri, mara nyingine yakiambatana na melodia na kuwaimbia wenzie ambao kama wangeukubali, walianza kutunga vipande mbalimbali vya wimbo kupitia  vyombo mbalimbali wanavyovipiga. Tungo nyingi za awali zilianza kwa rumba, na ilipofika katikati mwendo ulibadilika na kuingia katika kile tulichokuwa tukikiita ‘chemka’.
 Chemka mara nyingi ilianza kwa kuimba na kisha kuingia kipande cha gitaa la solo. Hapa ndipo wapiga solo walikuwa wakipimwa kwa umahiri wao wa kutunga na kupiga vipande vya solo ambavyo vingeweza kuwateka akili wasikilizaji na kuwafanya wacheze dansi.
Katika bendi nilizopitia kama vile TANCUT Almasi na Vijana Jazz Band, baada ya bendi kukamilisha wimbo, ulianza kupigwa katika maonyesho mbalimbali, lakini jambo la muhimu ambalo wanamuziki wote tulikuwa tunaliangalia lilikuwa Je, watu wanaucheza wimbo mpya? Ikionekana wimbo  umekosa hamasa ya kuwasimamisha  wachezaji, wimbo huo ulirudishwa mazoezini na kubadilisha vitu tulivyohisi vinafanya watu wasipende kucheza wimbo ule. Na mara nyingine wimbo huo ulitupwa pembeni moja kwa moja kama haukuchezesha, mamia ya nyimbo  katika bendi mbalimbali ziliishia kupigwa kwenye kumbi mara moja tu na hazikurudiwa tena, kwa kuwa tu watu hawakuchangan mkia kuzicheza.
Siku hizi mambo yako tofauti kabisa, unaweza kuingia kwenye onyesho la muziki wa Taarab, muziki ambao kwa asili ulikuwa ukisifika kwa kuwa muziki wa kusikiliza tu, ukakuta wapenzi wakitiririka jasho kwa kucheza nyimbo mbalimbali za Taarab, halafu ukaingia katika onyesho la ‘muziki wa dansi’, ukakuta waimbaji wakitoka mishipa ya shingo lakini hakuna anaeshughulika kucheza dansi hilo. Kama ingekuwa  zamani, hiyo ni dalili ya moja kwa moja kuwa muziki huo hauwafurahishi wapenzi. Lakini hizi ni zama nyingine.

Katika zama hizi, bendi huwa na wacheza show wake au hata waimbaji nao wakatengeneza show, kisha wakawa wanapiga muziki na kucheza wao wenyewe. Sijui nilinganisha na kujitekenya halafu kucheka mwenyewe?
Teknolojia imeleta aina nyingine ya kuonyesha upenzi na unazi wa muziki. Wapenzi wa muziki siku hizi huonyesha upenzi wao wa muziki kwa kuchukua simu na kurekodi video za  bendi zikiimba na kucheza, wao wenyewe wakiwa wamekaa kwenye viti wakiendelea kunywa vinywaji vyao, kisha vipande hivi vya video husambazwa kwenye makundi ya Whatsapp, vikiambatana na sifa kuhusu ubora wa bendi hizi. Ndio namna ya ‘ku appreciate’ muziki zama hizi.
Lakini pia kuna madansi ambayo utakuta wapenzi wamechangamka wanacheza sana, lakini ukiangalia kila mtu anacheza akili inavyomtuma, hakuna tena mpangilio wa kucheza staili maalumu ya muziki. Ile staili ya wapenzi kukumbatiana kwa hisia wakati wa kucheza rumba imepotea, si ajabu kabisa kumkuta mtu na mpenzi wake wanacheza wimbo wa taratibu, lakini kila mtu na staili yake na juu ya hayo kila mmoja anatuma meseji kwenye simu yake.
Hakika dansi limebadilika sana

 

No comments:

Post a Comment